February 20, 2017
Na Saleh Ally
WAKATI mwaka 2009, Godfrey Bonny anajiunga na Yanga alikuwa ameamua kuitupilia mbali kazi yake ya askari magereza ili ajitangaze zaidi kisoka.


Kawaida mchezaji anapojiunga na timu kubwa kama Yanga au Simba kwa hapa nyumbani, matumaini yake huwa ni suala la maslahi makubwa zaidi.


Mara nyingi nimesikia wachezaji wakitaka kulipwa ada kubwa ya uhamisho kwa kuwa wanajua wanapoteza maslahi yao ya uzeeni baada ya kuacha kazi.


Bonny, maarufu kama Ndanje, hakuwa wa kwanza, wapo wengi kama akina Herry Morris aliyejiunga na Yanga miaka hiyo au Primus Kasonzo aliyetua Simba.


Nina imani kubwa, wengi waliojiunga na timu hizo kubwa wakiacha kazi zao za uaskari, waliishia kujuta kwa kuwa soka si mchezo wa muda mrefu hasa pale unapoanza kucheza na kupata maslahi makubwa.Nawaelewa kwa kuwa tamaa ya mafanikio katika jambo unalolipenda huwa na nguvu kuu. Maana yake hivi, kwa anayecheza soka hapa nchini, kwa asilimia 98, naamini kila mmoja angetamani kuichezea Yanga au Simba. Ndiyo maana inakuwa vigumu kukataa inapotokea nafasi na inafikia wahusika wanakuwa tayari kupoteza wanayoamini ni mafanikio ya baadaye.


Kwangu niwakumbushe wengine wanaotaka kujiunga na Simba au Yanga halafu wao ni askari, basi vizuri wakajipima na kuangalia mengi zaidi na hesabu zao ziwe za uhakika. Lakini wanaweza kuwatafuta waliowahi kufikia katika wakati huo, wakawapa ushauri au kuwaeleza walikopitia ili wakichukua uamuzi tayari uwe na maandalizi.


Bonny ametangulia mbele ya haki na juzi mchana amepumzishwa, Mwenyezi Mungu amrehemu. Wakati wa mazishi amepewa heshima kwa jeneza lake kupambwa kwa bendera ya Yanga lakini chini yake ile ya taifa kwa kuwa alikuwa shujaa wa taifa letu. Lakini nimeumizwa na namna mambo yake yalivyokwenda.Wakati akiwa mgonjwa, nilipopata taarifa tulijaribu kutaka kumchangia. Lakini ajabu tuliambiwa mambo yake yalikuwa siri, mzazi wake hakufurahia suala la watu kwenda mara kwa mara nyumbani na hata alipopelekwa hospitali.


Tulituma mwandishi hadi Rungwe, nako ilikuwa shida na hakupata ushirikiano pia. Wakati huo niliendelea na kushangazwa na Klabu ya Yanga kuwa kimya na kutokumbuka lolote kuhusiana na Bonny. Hakuna kiongozi aliyezungumzia kuhusiana na michango au kumsaidia kiungo huyo aliyewahi kutwaa mataji na Yanga.Kama hiyo haitoshi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), halikuonyesha ushirikiano wowote na mwisho likaishia katika umahiri wake wa utoaji rambirambi kupitia Rais Jamal Malinzi. Utaona, “Rais Malinzi atuma rambirambi msiba wa Bonny”. Hiki ndicho kikuu wanachokiweza lakini si uhamasishaji wa michango au kufikisha misaada sahihi katika wakati mwafaka. Mimi nauona huu ni unafiki mkuu.Wapo Yanga waliojitolea, mmoja wao ni nahodha wa zamani wa Bonny, Shadrack Nsajigwa. Hakika anastahili pongezi hadi mwisho wa Bonny askari magereza wa zamani.


Ukiachana na ushauri wa kwanza kuhusiana na walio na ajira zao halafu wanatakiwa kujiunga na Yanga au Simba na kuachana nazo, sasa ni wale wachezaji wa zamani ambao wamekuwa hawathaminiki kabisa.


Wapo wengi hata sasa wanaougua. Wapo sasa wamepofuka, kama mnamkumbuka Allan Shomari hawana msaada wowote. Yupo Arthur Mwambeta amekatwa miguu, nawakumbusha Jela Mtagwa na Athumani Chama ‘Jogoo’, hawa wanaumwa kiharusi na hakuna anayewajali na wote tumekaa tunasubiri siku ya rambirambi ili tujitokeze kwa wingi na klabu; iwe Yanga au Simba, na TFF ndiyo zianze kuelezea majonzi.

Kuna unafiki wa hali ya juu miongoni mwa viongozi wa mchezo wa soka. Zimepita siku chache, mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali alikuwa mgonjwa, aliugua kwa wiki mbili akiwa ndani. 


Hakuna kiongozi wa Simba aliyemkumbuka na alipopona, anaonekana anafaa kuendeleza msaada wa klabu hiyo. Hii ni hatari sana na tunapaswa kujua sote ni wanadamu na kama leo ni kwa mwenzako, kwako pia inawezekana ikawa kesho, tuache unafiki.Mwisho ni funga kazi, Yanga na TFF wameonyesha kiasi gani wana uwezo mkubwa wa kusahau kila kitu kwa mchezaji ambaye ataondoka mbele ya macho yao. Mapenzi yenu kwa wachezaji yamejaa unafiki na ubabaishaji mkubwa.


Yanga ilicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Ngaya ya Comoro ikiwa ni siku moja kamili tokea kifo cha Bonny. Kabla ya hapo, hata rambitambi haikuelezwa au kutangazwa.


Lakini kama ilikuwa hivyo, basi halikuwa jambo lililofika kwa wengi. Kwa kuwa hawakuchangia, rambirambi ya salamu tu halikuwa jambo muhimu, basi hata kuvaa vitambaa vyeusi kuonyesha wana msiba!


Wachezaji kama Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, hawa wote walicheza na Bonny, wao pia walishindwa kukumbusha umuhimu wa hilo kama heshima kwa askari aliyewahi kuipigania Yanga kitaifa na kimataifa?Waungwana kweli mnaweza kuzungumzia mapenzi ya dhati au kila mmoja anajisahau kwa kuwa sasa mambo yanakwenda vizuri?Lakini jiulize, TFF ndiye msimamizi mkuu wa mchezo wa soka, wao walishindwa kumsaidia mchezaji aliyewahi kuichezea timu ya taifa, tena ile katika kipindi ikifanya vema chini ya Marcio Maximo. Ikafikia nikawa najiuliza au kuna Taifa Stars ya Tenga na Taifa Stars ya Malinzi na hizi mbili hazihusiani?Bonny ana mchango mkubwa katika soka hapa nchini kwa kuwa amecheza kivitendo katika ngazi zote kubwa hapa nchini. Anawazidi viongozi wengi sana waliopo sasa TFF kama utazungumzia mchango wa maendeleo.Hivyo TFF ilishindwa kusimamia hilo, kwamba kutakuwa na dakika moja ya kumpa heshima na kumuombea Bonny. Naamini hili si gharama ya fedha au vyovyote zaidi ya maagizo tu kutoka kwa viongozi na bahati nzuri wengi ni mashabiki wa Yanga.


Hii ni kengele kuu ya uamsho kwenu wachezaji mnaocheza sasa. Kuwa mjiandae na mjue mnafanya kazi na watu wanaowapenda wakati wakiwa nanyi tu. Baada ya hapo hakuna anayeweza kuwakumbuka au kuwajali tena na kibaya zaidi hata nyie wenyewe ni wanafiki, hamuwezi kuungana na kuwa na nguvu moja.


Mmestaafu lakini hamna ukaribu, mmejaa majungu, mnakorofishana na kuombeana mabaya na hii inachangia mwanya kati yenu kuwa mkubwa na unawaruhusu viongozi wa soka kuingia katikati yenu na kufanya haya wanayoyafanya.


Chaguo ni lenu, mkiamua kubadilika mtabadilisha mambo na kuinua thamani ya utu wenu. Mkiamua kuendelea, basi endeleeni mnavyotaka ili muendelee kubaki kama ilivyo sasa na mwisho itafikia thamani yenu itaangukia kwenye ziro.


SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV