February 27, 2017
 Na Saleh Ally
TOFAUTI ya mabao mawili waliyofunga Simba wakati wakiivaa Yanga jana ni dakika 15 tu. Lakini Shiza Kichuya alicheza kwa dakika 39 na kufanikiwa kufunga bao la ushindi huku akitoa pasi kwa lile la kusawazisha.

Kwa mashabiki wa Simba walijua wamekumbwa na balaa jipya baada ya Novaty Lufunga kumuangusha Obrey Chirwa katika dakika ya 3 tu, penalti ikapigwa dakika ya 5 na kuzaa bao lililofungwa na Simon Msuva.
Huenda mashabiki wa Yanga walijua kazi imekwisha mapema na walichotakiwa ni kuongeza bao moja ili kumaliza kazi, lakini haikuwa hivyo, licha ya kwamba walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja.

Kocha Joseph Marion Omog alionekana akitembea na chaki muda wote, hakutaka kukaa akijua mambo yameharibika na hakika kama angepoteza, kibarua chake kingekuwa katika hatihati.

Lakini kazi yake dakika 6 tu ndiyo ilibadili mambo na kumaliza kabisa nguvu ya Yanga, hali ambayo ilisababisha Simba kuibuka na ushindi ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja.
Omog alitakiwa kuwa jasiri sana ili kuibuka shujaa hapo baadaye kama ilivyokuwa. Kuna mambo yalitokea katika mechi hiyo ambayo ilikuwa ni lazima akubali lawama kama angeshindwa.
Ilikuwa ni lazima kujitoa mhanga lakini kwa hesabu za uhakika, utaona katika dakika ya 27, mara tu baada ya kuona Simba ikiwa imezidiwa mfululizo kwa zaidi ya dakika 15 huku Justine Zulu, Thaban Kamusoko wakifanya wanavyotaka, alimtoa Juma Liuzio na kumuingiza Said Ndemla.
Aligundua alifanya kosa na Yanga walijaza viungo watatu wakongwe au wazoefu. Hivyo alihitaji kiungo mwenye kipaji au mpishi. Mwenye uwezo wa kukaa na mpira na kufanya uchambuzi yakinifu ni kipi cha kufanya.
Liuzio hakuwa ameharibu. Lakini kumbuka amelazimika kucheza pembeni kama sehemu ya kumjaribu hiyo ikiwa ni kama mechi ya nne. Lakini bado Omog angeweza kumpeleka Mo Ibrahim pembeni kushoto na Liuzio akaingia ndani, lakini akamtoa.

Hiyo ilikuwa ni kipindi cha kwanza ambacho Simba iliweza kupunguza kasi ya Yanga na kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao moja. Utaona sub ya Ndemla ilisaidia Simba kutofungwa bao la pili, maana ingekuwa hivyo, Yanga ingekuwa imemaliza mchezo mapema.
Kipindi cha pili, ilikuwa Simba ni lazima ifanye linalowezekana kutafuta bao la kusawazisha. Kimahesabu hii ni kuanzia dakika 15 hadi 20 za mwanzo. Hapa unaona Omog anajitoa mhanga na kumtoa Lufunga katika dakika ya 51 na nafasi yake inachukuliwa na Shiza Kichuya. Alichokuwa akitaka hapa ni bao. Lakini kumbuka Lufunga alikuwa tayari na kadi ya njano, hapa alipunguza hatari ya kadi nyekundu.

Besala Bokungu anaingia katikati kuongeza ulinzi lakini dakika nne baadaye, yaani dakika ya 55, analambwa kadi nyekundu baada ya kumuangusha Chirwa aliyekuwa anakwenda kumuona Daniel Agyei.
Lilikuwa ni kama pigo kuu kwa Omog na linababaisha. Lakini anatulia kabisa na dakika mbili baadaye, yaani dakika ya 57, anamtoa Mo Ibrahim ambaye alionekana amenoga au anawasumbua Yanga na kumuingiza kiungo mkabaji, yaani Jonas Mkude.
Hapa kumbuka, Omog alikuwa nyuma kwa bao 1-0 na kikosi chake kilimtegemea Mo katika kusukuma mashambulizi na James Kotei ndiye alikuwa injini akitembea. Analazimika kurudi kucheza namba tano, Abdi Banda akibaki namba nne.

Dakika sita tu za mabadiliko ya Omog ndizo zilizobadili kila kitu. Yaani tangu dakika ya 51 alipomuingiza Kichuya na dakika ya 57 alipomuingiza Mkude.
Unagundua mabadiliko yalianzia kipindi cha kwanza kumtoa mshambuliaji, akamuingiza kiungo. Halafu kipindi cha pili akamtoa beki wa kati akamuingiza kiungo na mwisho akamtoa kiungo mshambuliaji akaingia kiungo mkabaji.
Kichuya aliyeingia katika dakika ya 51, alipata zaidi ya nafasi ya kucheza baada ya kutoka kwa Mo. Lakini difensi ya Simba ikawa inacheza na viungo wakabaji watatu kiasili yaani Kotei, Mkude na Banda pia. Lakini kukawa na kiungo mkabaji mmoja, yaani Mzamiru Yassin ambaye alikuwa akicheza kama namba nane lakini kwenye kukaba, anarudi haraka kuungana na wenzake.
Hapa unaona inakuwa vigumu tena kwa Yanga kuongeza bao na inatoa nafasi kwa Simba kuutawala mchezo kwa kiasi kikubwa sana.

Kichuya ndiye aliyetoa pasi ya bao la kusawazisha la Mavugo katika dakika ya 66 na yeye akamaliza kazi kwa kufunga la ushindi dakika ya 81.
Utaona Kichuya ameumaliza mchezo ndani ya dakika 39 tokea aingie uwanjani. Lakini ndani ya dakika 15 tu alikuwa ametoa pasi iliyozaa bao la kwanza na yeye kufunga la pili.

Utaona mabadiliko ya Omog yaliimarisha kiungo na kuidhoofisha Yanga, halafu mabadiliko hayo yakaimarisha ulinzi na kuizuia Yanga kufunga bao. Lakini tatu, mabadiliko yake yalizaa mabao mawili na kuimaliza kabisa Yanga.

Mabadiliko matatu ya Omog yaliisha katika dakika ya 57 alipoingia Mkude. Ungeweza kuona ni kama mabadiliko ya haraka sana na huenda Omog alipaswa kusubiri. Lakini yeye alikuwa tofauti na mwepesi kufanya mambo sahihi katika wakati mwafaka.

Kocha wa Yanga, George Lwadamina ndiye amekuwa mkali wa sub, lakini juzi alionekana kupwaya kwa kuwa mabadiliko yake matatu hayakuwa na manufaa kwake.

 Lakini kwa Omog, ilionekana mchezo ulikuwa mkononi mwake na aliweza kufanya vilivyo sahihi na mwisho kumaliza akiwa shujaa tena kwa kupiga ndege watatu kwa jiwe moja. Kwanza kuendeleza rekodi ya kutofungwa na Yanga, pili kuwafunga watani na tatu, kujiweka vizuri kileleni, kwamba hata kama Yanga watashinda mchezo ujao na kulingana michezo na Simba, hawatakuwa wamewafikia.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV