February 3, 2017



Baada Yanga kuwa kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, winga wa timu hiyo, Simon Msuva, amewaambia Simba kuwa endapo watapoteza mchezo wao dhidi ya Majimaji, basi wafute kabisa ndoto za kuwania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.


Yanga kwa sasa ndiyo inayoongoza ligi ikiwa na pointi 46 mbele ya Simba yenye 45, ambapo leo Ijumaa Yanga itacheza na Stand United huku Simba ikitarajiwa kucheza kesho.


Msuva alisema kutokana na mikakati ya timu yao na benchi zima la ufundi, wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi katika kila mchezo wao, jambo ambalo litawafanya wachukue ubingwa kirahisi.


“Hakika kikosi chetu kiko salama kiasi kwamba tunachowaza sasa ni kuendelea kushinda kila mchezo ili tuweze kutwaa ubingwa kwa mara nyingine tena, tunajua tuko kileleni kwa zaidi ya pointi moja, hivyo hatutaki tena kuruhusu uzembe wowote ambao utaweza kutugharimu kushuka chini.


“Wapinzani wetu Simba wameenda kucheza Songea na si rahisi kwao kupata ushindi, ninachoweza kuwaambia ni kwamba wajue kuwa wakizidi kuteleza tu basi safari yao itakuwa imeishia hapo, maana sisi hatutakuwa na nafasi tena ya kupoteza chochote.



“Najua wapinzani wetu hao nao wana mawazo ya kutwaa ubingwa ila watambue tu kuwa endapo watashindwa kupata matokeo kwenye mchezo huo, basi wasubiri msimu ujao kwani sisi tutazidi kupaa kileleni hadi mwisho,” alisema Msuva.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic