February 3, 2017

Na Saleh Ally
NDANDA FC wamesema wanaendelea kusafiri kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kuwavaa Azam FC katika mechi yao iliyopangwa kuchezwa kesho Jumamosi.


Lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema limeisogeza mechi hiyo hadi Februari 7 ili kuipa nafasi Azam FC kucheza mechi yake ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.


Mamelodi ni mabingwa wa Afrika, walikuja nchini kwa ajili ya kucheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya Simba, Yanga na baadaye Azam FC, vigogo hao wawili wakagoma na kuonyesha wanajitambua.


Mwisho Azam FC wakakubali kucheza mechi hiyo ya kirafiki na kufanikiwa kutoka 0-0 dhidi ya mabingwa hao. Mechi ambayo ilihudhuriwa na mashabiki ambao hata 200 hawakufika!


Kocha Pitso Mosimane wa Mamelodi ni rafiki yangu kwa zaidi ya miaka 10 sasa. Urafiki wetu ulianza baada ya yeye kumchukua Selemani Matola wa Simba kwenda kujiunga na kikosi cha SuperSport United cha Afrika Kusini baada ya michuano ya Tusker jijini Nairobi, Kenya.


Mosimane aliniambia wanajiandaa na mechi kadhaa ikiwemo dhidi ya Kaizer Chiefs tarehe 8. Alinieleza wamekuja huku baada ya kuwa wako ‘free’ na hawana michezo inayowabana na walitaka sana kucheza na vigogo hasa Simba ambayo wanaamini inaongoza kwa makombe mengi kwa rekodi walizonazo.


Wao wamekuja huku kwa kuwa ratiba inawaruhusu na hakuna sehemu ambayo wanavuruga ratiba ya ligi. Mechi zao hapa zilitakiwa kuvuruga ratiba ya ligi na mwisho imekuwa hivyo.Kama Yanga na Simba wangekubali kucheza nao, basi huenda ratiba ingevurugika zaidi. Unaona wakati Yanga wanakuwa wa kwanza kukataa na unagundua waliona jambo sahihi, kwani hakuna faida ya kucheza na Mamelodi kipindi hiki katikati ya ligi.


Awali, tulielezwa Simba walikuwa wamekubali wacheze juzi Jumatano, lakini nao wakakataa huenda baada ya kujitathmini au waliona namna ambavyo Yanga walifanya ambalo lilikuwa jambo sahihi. Sijui kama wao wangekubali kucheza, TFF ingesogeza mbele michezo yao?


Azam wamekubali na TFF imesogeza mchezo huo mbele bila ya kujali mipango ya Ndanda FC ikoje. Lazima tukubali kwamba, haki kama unazungumzia katiba au kanuni za uendeshaji ligi kuu, Ndanda FC wana haki na hadhi sawa na Azam FC, kwa kuwa zote ni timu za ligi kuu.


Hakuna kigezo kwa mujibu wa kanuni au sheria yoyote inayoweza kuipa Azam FC ubora au ukubwa zaidi ya Ndanda FC. Kama ni hivyo, basi TFF inapaswa kuziheshimu timu zote za ligi kuu na kuachana na woga usiokuwa na sababu za msingi.


Msimu uliopita, TFF ilikubali kuvuruga ratiba ya ligi kuu, ikawapa nafasi Azam FC kusafiri hadi Zambia kushiriki tamasha la timu kadhaa. Wakati tamasha hilo linafanyika Zambia, ligi yao ilikuwa imesimama kwa kuwa wanaelewa ukubwa na thamani.Walisema lengo ni kusaidia kuiimarisha Azam FC wakati wa ushiriki wa kimataifa. Ilifikia wapi? Wote tunajua na msisitizo tokea huo msimu uliopita nilieleza namna TFF inavyoshindwa hata kuthamini kinachoiweka mjini. Bila ligi kuu yenyewe itatambulika wapi, itakuwa inafanya nini? Viongozi wake kwa nini wanashindwa kulielewa hili na kuona tamasha ni bora kuliko ligi?


Leo wamefikia wanaona mechi ya kirafiki, eti kisa ni mabingwa Afrika, ni bora kuliko ligi kuu? Hawa viongozi ni wa namna gani au ulaini na woga wao kwa Azam FC ni upi?


Wasitake watu tuanze kuamini kupitia ujumlisho wa mambo, kwamba kwa kuwa wanadhaminiwa na Azam TV ambayo pia inamilikiwa na makampuni ya Bakhresa ambao ni wadhamini wa michuano ya Kombe la Shirikisho ikiwa na maana ni wadhamini wa TFF, basi wanashindwa kuwa huru au kuwa na maamuzi sahihi linapofikia suala la Azam FC!


Hii si sahihi, misimu miwili mfululizo TFF inaonekana kujilainisha katika masuala yanayoihusu Azam bila ya kuangalia haki ya timu nyingine zinazoshiriki ligi.


Mimi naiunga mkono na kuipongeza Azam TV kwa udhamini wa michuano ya Kombe la Shirikisho na niseme wanapaswa kuungwa mkono kwa kuwa wameingiza fedha nyingi sana, tena ni chombo cha habari.

Niwe wazi, kamwe hata kidogo bila ya woga siungi mkono tabia za kizabizabina za TFF kama wanazozifanya ambazo zinaonyesha wazi ni waoga, wasio na maamuzi sahihi na huenda wanataka kuwafurahisha wadhamini kwa njia nyingine ambazo si sahihi.


Mwisho wito wangu kwa TFF, wao ndiyo wanatakiwa kuwa watu wa kwanza kuonyesha heshima ya juu kwa ligi kuu na timu zinazoshiriki na wajue, kama hakuna timu za ligi kuu na ligi nyingine, TFF haitakuwepo na wala haitakuwa na fedha za kuingiza kwa kuwa haina hata duka la kuuza mafuta ya taa!

SOURCE: CHAMPIONI


1 COMMENTS:

  1. TFF INAJIDHALILISHA SANA HAWAJUI KANUNI NA TARATIBU ZA LIGI YETU WANAISHUSHA HADHI LIGI YETU TIMU INAKUJA TU ETI BINGWA WA AFRIKA ANAVULUGA RATIBA NI KICHEKESHO CHA MWAKA.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV