Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, yupo kwenye mtego mkali wa kuhakikisha anafanikisha timu yake kushinda katika mechi ya watani wa jadi, Yanga, inayotarajiwa kuchezwa Februari 25 ili kuweza kutetea kibarua chake.
Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Februari 25 kwenye Uwanja wa Taifa jijini kwenye mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na mbio za ubingwa walizonazo ambapo hadi sasa hakuna timu iliyojihakikishia ubingwa.
Awali, Simba ilikuwa na nafasi kubwa ya kuweza kutwaa ubingwa wa ligi kutokana na kuongoza pointi nane mbele kabla ya kuzipoteza na kupitwa na Yanga, hivyo kusababisha wapishane pointi moja.
Bosi kutoka Simba amesema kuwa macho na mtazamo wa viongozi wa timu hiyo hivi sasa ni kuona wanashinda mechi dhidi ya Yanga kwani wanataka kuona matokeo ya mechi hiyo inakuwaje, iwapo watashinda ama la na kudai kuwa kibarua cha kocha huyo kimeshikiliwa na mechi hiyo.
“Viongozi wamepatwa na kigugumizi juu ya kubadili makocha kila kukicha kutokana na matokeo ambayo tumekuwa tukiyapata lakini mtazamo wa viongozi ni kwenye mechi ya watani ndiyo itakayokuja kutoa taswira ya makocha hao kuendelea kuitumikia Simba.
“Kumekuwa na mabadiliko sana katika kikosi kutokana na kocha kupenda kuangalia zaidi suala la ulinzi na si kushambulia jambo ambalo linasababisha timu kushindwa kufanya vizuri,” alisema bosi huyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment