Mwenyakiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, amefunguka kuwa, lazima wawafunge wapinzani wao Yanga katika mechi ya Jumamosi kwani wapinzani wao hao si lolote wala chochote, wapo kama pilipili hoho ambayo haina makali.
Simba ambayo ina pointi 51 katika msimamo wa ligi, inatarajiwa kukutana na Yanga yenye pointi 49 ikiwa na mchezo mmoja mkononi siku ya Jumamosi katika Dimba la Taifa ambapo katika mchezo wa awali wa mzunguko wa kwanza, timu hizo zilipokutana matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1, hivyo mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na kila timu kuwania ubingwa wa ligi hiyo kwa sasa.
Dalali amesema hata kukiwa na mgogoro wa kiasi gani katika timu hizo, lakini linapokuja suala la mechi ya watani wa jadi lazima kuwe na umoja kuhakikisha wanafanya vyema na kudai kuwa kwa upande wao wanaichukulia Yanga kama pilipili hoho ambayo haina makali yoyote.
“Linapokuja suala la mechi ya Simba na Yanga hata kama kunakuwa na mgogoro wa aina gani huwa mambo yanakaa pembeni lakini tunachoangalia hapa ni kuwapiga wapinzani wetu, kwani Yanga ni kama pilipili hoho, haiwashi kwani hata mtoto mdogo anakula, tunachokihitaji hivi sasa ni kuhakikisha timu yetu inafanikiwa kushinda mchezo huu.
“Simba ya sasa siyo kama ile ya miaka miwili iliyopita, ya safari hii ina nafuu kutokana na uwezo wanaouonyesha wachezaji uwanjani, hivyo tutafanya vyema kwenye ligi na hatimaye tuweze kutwaa ubingwa.
“Kinachohitajika kwa sasa ni ushirikiano na mshikamano kuanzia kwa viongozi, wanachama na wachezaji mbalimbali waweze kutoa mchango wao ktika timu ili kuweza kuimarisha timu zaidi ili iweze kuwa nzuri hadi mwisho wa ligi,” alisema Dalali.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment