February 17, 2017Na Saleh Ally
ULIANGALIA mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 kati ya Arsenal na wenyeji wake Bayern Munich? Huenda uliona vitu vingi sana, lakini mimi nilikuwa najiuliza kama kweli Phillip Lahm, nahodha wa Bayern Munich amepanga kustaafu soka baada ya miezi mitatu ijayo.


Novemba, mwaka jana, Lahm alitimiza miaka 33, lakini anaonekana kuifanya kazi yake kwa ufasaha na ustadi wa juu, na utendaji wake unaondoa kabisa lile suala la wachezaji vijana kuwa bora zaidi.


Kiungo wa pembeni wa Bayern, Arjen Robben, naye anaonekana kama kinda ukilinganisha na Alex Iwobi mwenye umri wa miaka 20.Hata kama haijashinda, inapokuwa England sifa kubwa ya Arsenal ni pasi za uhakika na soka la kuvutia. Dhidi ya Bayern, pamoja na kupigwa mabao 5-1, wenyeji walipiga pasi 704 zilizofika na Arsenal wakapiga 186 zilizofika.


Kama hiyo haitoshi, takwimu zinazidi kuihukumu Arsenal kwa kuwa msimu wa 2009-10 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ndiyo ulikuwa wa mwisho kwao kwenda zaidi ya hatua ya 16 Bora, maana ndiyo mara yao ya mwisho kutinga robo fainali.


Mara ya mwisho kufika nusu fainali ilikuwa msimu wa 2008-09 na fainali pekee waliyofika ni ya 2005-06.


Baada ya hapo, kuanzia msimu wa 2009-10 hadi sasa, wamekuwa wakiishia hatua ya 16 Bora. Baada ya hapo, wanasubiri msimu unaofuata.


Maana yake Arsenal imebaki katika hatua ya 16 Bora kwa misimu sita mfululizo. Tayari wamelikoroga, wamefungwa mabao 5-1 na wanatakiwa kushinda 4-0 nyumbani ili waepuke kubaki 16 bora kwa misimu saba mfululizo. Wataweza? Maana wanasema mpira una miujiza yake, tusubiri!Kwa shabiki wa Arsenal, hata ungekuwa wewe, jiulize. Kuwa na timu ambayo ubingwa wa England ilitwaa mara ya mwisho mwaka 2003-04, baada ya hapo haijawahi tena na imekuwa ikijivunia kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya bila ya kukosa.


Hata hivyo, ushiriki wake wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ni kama geresha tu. Maana misimu sita sasa, inaishia nafasi ya 16 Bora na haijawahi kujirekebisha wala kuusoma mchezo kwamba imekwama kwa sababu zipi.

Imekwenda na mwendo huo Ligi Kuu England, kwa zaidi ya miaka 10, haijui hukosea wapi na kushindwa kubeba ubingwa.


Sasa ni Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kocha Mkuu, Arsene Wenger “Babu” wa Wana-arsenal, yupo tu na huku nako hajui anapokosea.

Wenger hawezi kujirekebisha, uongozi umeshindwa kuona, kumsaidia au kuamua. Mashabiki nao wanaendelea kulia huku Wenger na Arsenal yake wakiendelea na geresha tu, kuwa walishiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, kumbe hakuna lolote.Mfano, katika mechi sita za kwanza katika hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya, Arsenal imefungwa mabao matatu hadi manne. Vipi Wenger haoni kuwa wamekuwa wakikosea mguu wa kuanza na kubadilisha “Chemistry” yao katika msimu unaofuata wa Ligi ya Mabingwa? Kila msimu unaofuata wanakwenda kama msimu ujao au ulivyokuwa ulioita?


Msisitizo kama nilivyosema awali, Arsenal imekuwa chini ya Wenger na imefanya kazi kubwa lakini sasa lazima ijaribu na ladha nyingine kwa kuwa hii, imekuwa si inayoweza kuleta ladha ya raha kwenye midomo ya Wana-arsenal.


 REKODI:
2009-10
Ilikuwa ndiyo kiongozi Kundi H, ikatinga 16 bora na kupangiwa FC Porto ya Ureno. Arsenal ikasonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 6-2. Hatua ya robo fainali ikakutana na Barcelona na kung’oka kwa jumla ya mabao  6-3. Hii ndiyo ilikuwa mara ya mwisho Arsenal kuvuka 16 Bora.
Bingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya alikuwa Inter Milan.


2010-11
Ilishika nafasi ya pili Kundi H nyuma ya Shakhtar Donetsk, hatua ya 16 Bora ikakutana na Barcelona na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-3. Arsenal ilishinda London 2-1, ikapigwa 3-1 ugenini.
Bingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya alikuwa Barcelona.


2011-12
Walikusanya pointi 11 na kuwa vinara wa Kundi F, hatua ya 16 Bora ikakutana na AC Milan na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-3. Ni baada ya kupigwa 4-0 Milan, halafu ikashinda 3-0 London.
Bingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya alikuwa Chelsea.
  


2012-13
Ilishika nafasi ya pili Kundi B nyuma ya vinara Schalke 04. Hatua ya 16 Bora ikakutana na Bayern Munich, mwisho wa mechi zote mbili ilikuwa matokeo ya jumla 3-3. Bayern ikasonga mbele maana ilishinda 3-1 ikiwa London na Arsenal ikashinda 2-0 ugenini.
Bingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya alikuwa Bayern Munich.


2013-14
Walishika nafasi ya pili Kundi F wakilingana pointi 12 sawa na vinara Dortmund. Hatua ya 16 Bora wakakutana na Bayern Munich, wakachapwa 2-0 London, halafu wakashinda 1-0 ugenini, wakatolewa kwa jumla ya mabao 2-1.
Bingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya alikuwa Real Madrid.


 2014-15
Arsenal ilishika nafasi ya pili Kundi D nyuma ya Dortmund, hatua ya 16 Bora ikakutana na Monaco ya Ufaransa ikiongozwa na Anthony Martial. Matokeo ya jumla yakawa 3-3, Arsenal ikaenda nje kwa hasara ya bao la ugenini.
Barcelona ikawa bingwa mwishoni mwa msimu, likiwa ni taji lake la tano.


2015-16
Walikuwa Kundi F, wakamaliza nafasi ya pili nyuma ya Bayern Munich na hatua ya 16 Bora wakakutana na Barcelona, ukawa mwisho wa safari. Mechi ya kwanza walipigwa 2-0, ya pili wakapigwa 3-1, jumla wakaondolewa kwa 5-1.
Madrid ndiyo walikuwa mabingwa kwa kuwafunga tena Atletico Madrid katika fainali.


2016-17
Wamemaliza wakiwa vinara wa Kundi A wakiwa na pointi 14 na PSG wakiwafuatia wakiwa na 12. Baada ya hapo, wamevuka hadi 16 Bora ambako wamekutana na Bayern Munich na kukaangwa kwa mabao 5-1 katika mechi ya kwanza.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV