February 17, 2017

MAKONDA

Na Saleh Ally
GUMZO kwa sasa ni suala la vita dhidi ya madawa ya kulevya ambayo inaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.


Tayari Rais John Pombe Magufuli ametoa kauli kuhusiana na hilo na kusisitiza kwamba wanaofanya biashara hiyo washughulikiwe. Vita hii si ya hawa wawili tu.


Vita dhidi ya madawa ya kulevya inamhusu kila mmoja wetu kuanzia ngazi ya familia kwa kuwa athari zake si kwa makundi, badala yake ni kutoka katika familia moja baada ya nyingine.

Kila familia inayoathirika na madawa ya kulevya inajua ugumu wake. Mimi ninaweza kuwa shuhuda baada ya mtoto wa shangazi yangu kuingia kwenye janga hilo na hakika ni jambo baya ambalo linamfanya mtu asijitambue.

Ufikiri unakuwa duni, uthubutu unakuwa hafifu kwa kuwa mlengo unakuwa ni kwenye urahisi wa watu kama kuiba, kudhulumu, kukaba na kadhalika na si ujenzi wa ubunifu kwa ajili ya uzalishaji kuanzia ngazi ya familia kwenda mtaa, kitongoji, wilaya, mkoa hadi taifa.

Hivyo niseme naunga mkono vita hii ingawa msisitizo uende ukiwa umelenga suala hilo, “Vita dhidi ya Madawa ya Kulevya” na si kuingia kwenye siasa na ikatumika kama sehemu ya kuwaadhibu “Wasio na Heshima”.

Kikubwa ambacho ninaweza kushauri katika hilo, pia ni kupunguza nguvu kila sehemu ndani ya vita hiyo kuhusiana na masuala ya madawa ya kulevya.

Vita haiwezi kuendeshwa kwa vitisho pekee, haiwezi kuendeshwa kwa kuonyesha nguvu pekee, ingawa kuna sehemu kweli zinatakiwa kufanyika namna hiyo.

Lakini wapo wale waathirika ambao tumeelezwa kwamba wameathirika, tunajua. Hatuwezi kuwasaidia kwa kuwafunga au kuwaacha gerezani.

Walioathirika wanahitaji kusaidiwa kwa kuwa wanakuwa hawajiwezi. Kuwaadhibu ni kuwamaliza kabisa, ndiyo maana umeona nchi nyingi zinafanya programu maalum kwa ajili ya ukombozi wa maisha yao.

Makonda au yeyote ambaye anasaidiana naye katika vita hii lazima ajue hii si vita ya wiki, mwezi au miezi. Inatakuwa endelevu na ikiwezekana milele hata baada ya wao na sisi.

Vita hii si ya kitoto kwa kuwa mtandao wa madawa ya kulevya ni mkubwa, umejisimika hasa chini na una nguvu kubwa sana sehemu zote duniani.

Michezo inaweza kutumika kama sehemu ya muendelezo baada ya kuwa mapambano yameendelezwa sehemu mbalimbali. Lazima kuwe na hesabu au kujiuliza, wale ambao wameingia kwenye madawa na wameathirika baada ya kuwakomboa watakuwa wakifanya nini.

Watanzania wengi hatupendi mazoezi au michezo kwa maana ya ushiriki. Lakini asilimia kubwa waliofanikiwa kushiriki michezo wamefanikiwa kuepuka hili janga.
Unaposhiriki michezo, baada ya mazoezi unakuwa hoi, umechoka na zaidi ungependelea kupumzika. Muda huo asiyeshiriki michezo, angeona abaki na kushiriki katika matumizi ya madawa kama sehemu ya furaha yake.

Waathirika wakubwa ni vijana na sasa asilimia zinakwenda zinashuka, kwani hata watoto wameingia kwenye kundi la watu walioathirika.

Kama leo watoto wataandaliwa viwanja vya kutosha kwa ajili ya michezo, kukawa na kampeni za kuwanunulia vifaa na kuwapa nafasi ya kushiriki michezo wanayoitaka iwe riadha, sarakasi, judo, kikapu, soka, netiboli, ngumi na kadhalika, kwao itakuwa ni furaha na faraja nyingine ya moyo na watakuwa hawahitaji kwenda kutafuta furaha kwenye madawa ya kulevya.

Serikali ina uwezo wa kuandaa programu bora ambazo zitakuwa rafiki na shirikishi ili kupambana na tatizo hili ambalo haliwezi kuwa la siku mbili tatu na haliwezi kumalizwa bila kuandaa misingi bora ya kupambana nalo leo, baadaye na wakati ujao.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic