February 27, 2017



Na Saleh Ally
USHINDI wenye furaha iliyochanganyikana na shangwe isiyo na kipimo kwa mashabiki wa Simba, unaweza kugeuka na kuwa tatizo kwao kama hakutakuwa na usimamizi wa kutosha kwa maana ya kujithibiti.

Simba imeifunga Yanga kwa mabao 2-1, tena ikionyesha soka safi na la kuvutia jambo ambalo kihistoria ndilo linapendwa zaidi na mashabiki wa Simba.

Mashabiki wengi wa Simba wanavutiwa zaidi na soka la gonga nyingi na kutandaza gozi. Hata kama timu yao itashinda mabao matano, kama soka si la kuvutia, basi furaha yao inaweza isiwe juu sana.

Katika mechi ya juzi dhidi ya Yanga, mashabiki wa Simba walijumuishiwa mambo yote mawili. Mabao yaliyozaa ushindi lakini soka safi na la kuvutia.

Simba imeshinda mabao 2-1 baada ya kuwa nyuma kwa bao moja kuanzia dakika ya tano. Dakika ya 66, ndiyo Laudit Mavugo akasawazisha na hapo wakaamka na kuanza kuinyanyasa Yanga watakavyo kabla ya kufunga bao la ushindi katika dakika ya 81 kupitia Shiza Kichuya.

Furaha kwa Wanasimba ilikuwa kubwa, hakuna ubishi katika Ligi Kuu Bara katika kipindi cha miaka mitano, Yanga imekuwa mbabe wa Simba na imekuwa ikiitwanga mara nyingi.

Simba iliyokuwa ikitamba miaka mitano sita iliyopita iliporomoka. Baada ya hapo, Yanga ikaendelea kutawala tena na tena. Hivyo ushindi wa juzi lazima utakuwa ni shangwe kuu kwa Wanasimba.

Unapowataja Wanasimba unajumuisha mashabiki lakini wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwa pamoja. Kila mmoja lazima atakuwa na furaha na ataendelea kusherehekea.

Ambacho nakiona wengi wanaona kama Simba tayari imeshatwaa ubingwa, jambo ambalo linaweza likageuka na mwisho wakaishia kulaumu.

Nawajua mashabiki wa Yanga, Simba walivyo. Timu inaposhinda, inakuwa ya wote na ikifungwa, basi lazima wawe na mtu wa kumuangushia lawama na inaonekana kuwa wao wameonewa au vingine vyovyote. Simba haijamaliza ligi na wala haijawa bingwa, wala haijakaribia kuutwaa ubingwa.

Simba imejiweka katika nafasi nzuri ya kuwa mgombea ubingwa namba moja. Yanga haipo mbali sana kwa kuwa sasa ina pointi 54, Yanga iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 49. Kama itashinda mchezo mmoja ilionao mkononi basi itafikisha pointi 52 tu. Kama Simba atateleza, basi wao watatakiwa kushinda mchezo wa pili na kukaa kileleni.

Baada ya mechi ya juzi, Simba inatakiwa kushuka dimbani tena Machi 4, itakapowavaa Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kuna siku sita katikati ambazo zinajumuisha mapumziko na maandalizi ya mechi inayofuata dhidi ya Mbeya City, kumbuka hii si mechi rahisi kwa Simba. Hii inaonyesha kuwa Simba wanatakiwa kuendelea kusherehekea kwa muda mfupi sana hasa kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi.

Huenda suala la sherehe lingebaki zaidi kwa mashabiki. Ushindi kwa upande wa wahusika wa timu utumike kama sehemu ya morali na marekebisho mapya ya kuepusha kosa lililojitokeza awali, kukaa kileleni kwa tofauti ya pointi nane halafu mwisho wakapitwa na Yanga.

Wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wanapaswa kujiuliza kama walipitwa kwa tofauti ya pointi nane, vipi wanashindwa kupitwa kwa tofauti ya pointi walizonazo sasa.

Kuna kila sababu, sherehe za Simba zikawa na makundi kwa maana ya kundi linalotakiwa kusherehekea kwa muda mfupi sana. Na kundi la pili linaloweza kuamua kupumzika kusherehekea au kuendelea kama linataka na hili ni lile la mashabiki.


Simba bado ina kibarua kigumu, kumbuka inakutana na Mbeya City, baada ya hapo Machi 11, itakuwa Kagera kucheza na wenyeji wake kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba. Hivyo kuendelea kusherehekea sasa bila kuchoka, ni kujitengenezea majonzi hapo baadaye.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic