March 15, 2017Beki wa pembeni wa Yanga, Hassan Kessy, ameiangalia fiziki yake na kugundua haipo sawa, fasta akachukua maamuzi ya kukimbilia gym kwa ajili ya kuiongeza.

Kauli hiyo, aliitoa mara baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ya Zambia kumalizika kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Beki huyo, hivi karibuni alirejea kwenye kikosi cha kwanza cha Mzambia, George Lwandamina baada ya kusota kwenye benchi muda mrefu kabla ya kucheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara na moja ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na Zanaco.

Kessy amesema katika mechi dhidi ya Zanaco, ndiyo amegundua ana tatizo la fiziki kutokana na wachezaji wenye maumbile makubwa na kasi.
Kessy alisema fiziki yake imepungua baada ya kupunguza mazoezi ya binafsi aliyokuwa akiyafanya awali kutokana na benchi alilokuwa anakaa kabla ya kurejea uwanjani katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting.

Aliongeza kuwa, alichopanga hivi sasa kila siku atakuwa anafanya mazoezi ya binafsi ya gym na kukimbia barabarani kwa ajili ya kurejesha fiziki yake iliyopotea.

"Mechi na Zanaco ndiyo imenifanya nigundue vitu vingi vilivyojificha kwangu ikiwemo kupungua kwa fiziki, kiukweli sina kabisa fiziki ya kutosha.

"Hivyo, ninahitaji kuiongeza katika kipindi hiki ambacho tayari nina nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na ninachokifanya ni kuingia gym na kukimbia barabarani (road work).


"Unajua kipindi kile ambacho sipati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, nilipunguza mazoezi ya binafsi niliyokuwa nayafanya, niliona kama najichosha ninapofanya mazoezi magumgu wakati nikiwa sina nafasi katika timu," alisema Kessy.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV