March 24, 2017Akiwa amebakisha mechi sita za Ligi Kuu Bara sawa na dakika 540 za kuichezea Simba, beki kiraka Abdi Banda amegomea saini ya miaka miwili ya kuichezea timu hiyo.

Viongozi wa timu hiyo hivi sasa wanahaha kuipata saini ya beki huyo pamoja na mshambuliaji wa timu hiyo, Ibrahim Ajib ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu wa ligi kuu.

Banda alitua kuichezea Simba msimu wa 2015 kipindi hicho akiwa anaichezea klabu ya timu ya vijana ya U20 (Ngorongoro Heroes) na Coastal Union.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa kutoka kwenye Kamati ya Utendaji ya timu hiyo, viongozi tayari wamemuandalia na kumpa mkataba baada ya mazungumzo ya awali kufanyika lakini baadaye aligoma kusaini.

Mtoa taarifa huyo alisema beki huyo amegoma kusaini mkataba wa mwaka miaka miwili aliyopewa na viongozi wa timu hiyo huku yeye akiutaka wa mwaka mmoja wa kuendelea kukipiga Simba.

Aliongeza kuwa uongozi wa timu hiyo unaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha wanamuongezea mkataba mwingine wa miaka miwili ya kuichezea timu kwa kumpa dau zuri la usajili.

“Uongozi hivi sasa upo jitihada za kuhakikisha tunawasajili wachezaji wote ambao mikataba nayo inamalizika mwishoni mwa msimu lakini kwa vigezo maalum na kikubwa kikiwa ni kiwango na msaada na anaoutoa kwenye timu, ”alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Banda kuzungumzia hilo alisema: “Nisingependa kulizungumza hilo kwa hivi sasa kwani ninaogopa kujichanganya, hivyo tusubirie mechi hizi sita nilizozibakisha zimalizike za ligi kuu ndiyo ntakuwa kwenye sehemu nzuri ya kuongea.


“Naomba niishie hapo na kuhusu kitu kingine chochote kinachohusiana na mkataba, basi aulizwe meneja wangu ataweza kuweka wazi kila kitu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV