March 24, 2017




Na Saleh Ally
NAPE Nnauye aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwangu namuita ni mwalimu.
Nape ni mwanahabari ambaye alipata nafasi ya kuiongoza wizara hiyo kwa mwaka mzima katika kipindi cha awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli.


Kuondoka kwa Nape ambaye nafasi yake ameteuliwa Dk Harrison Mwakyembe kumezua mijadala mingi. Lazima tukubali ingekuwa hivyo kwa kuwa Nape alionyesha mifano mingi ambayo waliopita hawakuweza kufanya.

Nape alikuwa jembe hasa, alikuwa kiongozi asiyechoka aliyepigania tasnia ya habari, utamaduni, sanaa na michezo kwa mifano ya utendaji na si maneno.

Huenda wengi kama mimi waliona anaendana na kasi ya serikali ya Magufuli ya “Hapa Kazi Tu”. Inaonekana huenda tuliona tofauti lakini siwezi kukubali kumuacha aende bila ya kumuaga na kumpongeza kwa kazi nzuri wakati wa kipindi chake cha uongozi.


Wasanii aliowasaidia wakiwemo wale aliowaombea hadi nafasi za kufanya video zao Afrika Kusini, aliowaombea udhamini wa kuwasafirisha. Aliyefanya nao mikakati ya kupambana na wezi wa kazi zao na kadhalika watakuwa wanamkumbuka.


Kwa wanahabari mnajua wala siwezi kuwakumbusha kwa kuwa hadi anaondoka alikuwa katika harakati za kupigania haki ya Wanahabari baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia kituo cha utangazaji cha Clouds TV akiwa na askari wenye mitutu.


Nape aliahidi kuwatetea wanahabari, akasisitiza heshima na uhuru wao. Ndiyo maana nasema kwangu ni mwalimu kwa kuwa amenifunza kuendelea kupambana kwa ajili ya nchi yangu bila ya woga. Amenifunza upendo baina ya wanatasnia wenzangu na wasio wanatasnia.


Wanamichezo mnajua mengi, mabadiliko aliyoyafanya, mikakati aliyoweka na kadhalika. Tunajua amesaidia kubadilika kwa mambo mengi sana katika tasnia ya michezo, mambo ambayo awali yalionekana kama hayawezi kubadilishwa.


Mnakumbuka alivyofunga safari hadi Multichoice Tanzania kumuombea udhamini mwanariadha Felix Simbu ambaye baada ya kuanza kulipwa kila mwezi pamoja na kambi ya maandalizi, aliibuka na kushinda Olimpiki ya Mumbai na kuleta medali ya dhahabu, jambo ambalo nchi yetu liligeuka na kuwa nadra tena kutokea.


Waziri wa aina ya Nape, ni mtu aliyeonyesha uzalengo kwa watu wake na ndiyo maana ya utaifa. Najua ana nafasi bado ya kuwatumikia wananchi wa Mtama waliompa ubunge. Mimi nitaendelea kuheshimu kazi zake ambazo zilikuwa msaada kwenye tasnia ya habari, kwenye sanaa na utamaduni na pia vita ya kuikomboa michezo.


Magufuli alituletea Nape na tukamfurahia kutokana na ubora wa kazi yake. Sasa ametuletea Dk Mwakyembe ambaye pia ni mwanahabari. Kinachotakiwa sasa kwa wote ni kumpa ushirikiano wa kutosha.


Nape alipata ushirikiano mkubwa kwa kuwa alikuwa tayari kutoa ushirikiano kwa wale walioonyesha ushirikiano na hata ambao hawakutaka kumpa ushirikiano.

Dk Mwakyembe ni mwanahabari na mwanasheria, mimi namkaribisha na kumshauri kukaa na Nape ikiwezekana amueleze alipoishia na baada ya hapo katika mwendelezo, kama ana ubunifu wake, basi tumuunge mkono ili kuendelea kufanya mabadiliko katika njia iliyo sahihi kwa lengo la kuboresha na kufanikisha. 

Nimshauri pia kuendeleza ushirikiano kwa wanatasnia kwa kuwa wizara yake ni pana.


Kila mmoja anamjua Dk Mwakyembe ni mchapakazi na hakuna hofu ya yeye kushindwa jambo. Ushirikiano ni njia sahihi ya kuongeza kasi ya utendaji wake ili atusaidie kuondoa magugu rundo katika upande huu.
Hata angekuwa bora vipi, Dk Mwakyembe hataweza peke yake. Kama tutamuunga mkono lazima atafanikiwa na kutusaidia. Hakuna haja ya kufikiria tofauti zaidi ya kuungana naye.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic