March 29, 2017Na Saleh Ally
KAMA ni mtu unayefuatilia burudani hasa muziki wa kizazi kipya, basi utakuwa unakumbuka ule wimbo wa ‘Shika Adabu Yako’ wa Nay wa Mitego.

Nay ambaye jina lake halisi ni Emmanuel Elibariki, alitoa wimbo ukiwa unataja majina ya wasanii wenzake na wengi aliwadhalilisha kwamba wamenunuliwa magari au waliazima na kadhalika.


Hakika ulikuwa ni wimbo ambao unaonekana hata yeye Nay alitaka kupata kiki kwa kupitia migongo ya wasanii wenzake.


 Nay amechagua aina yake ya uimbaji, huenda haiwafurahishi wengi kwa kuwa amekuwa akiwagusa moja kwa moja. Ni sehemu ya sanaa, lakini hakuna kinachoweza kubadilika zaidi ya msitari sahihi wa kufuata maadili.


Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), waliamua kuufanyia kazi na mwisho wakaufungia, naye akitwangwa adhabu. Ninaamini hakuna aliyelalamika kwa kuwa lilikuwa jambo sahihi.


Ingawa inaonekana walikasirishwa kwa kuwa Nay amekuwa akiwagusa pia na kwa kuwaeleza wazi waache tabia tu ya kufungia nyimbo za wasanii.


Hapo ndipo nilipoanza kufuatilia kutaka kujua kama angalau Basata wamekuwa wakifanya kazi ya kuwaambia wasanii kurekebisha nyimbo wanazotoa na zikaonekana kuwa na walakini!


Mfano kufuta baadhi ya mistari au kuboresha lugha au suala fulani la maadili. Kikubwa sana wanaamini ni kwenye kufungia, huenda kuwa mkali zaidi kunaweza kuwa suluhisho kuliko ubunifu wa uboreshaji. Huenda tunafikiri tofauti.


Basata huenda imepitwa na wakati na sasa inakwenda kwa mwendo wa rimoti, inaangalia jamii inaangalia wapi, imekasirishwa na nini au kufurahishwa na kipi, nayo inajificha katika kichaka hicho.


Kama Basata ni wataalamu wa sanaa, lakini ukweli hawaonyeshi hivyo. Ni wale watu wanaofuata upepo wa wanajamii au viongozi wa serikali.

Hawana maamuzi yao sahihi yanayoweza kwenda tofauti na jamii na wakatoa ufafanuzi. Wanakariri mambo na huenda uamuzi wa Rais John Pombe Magufuli kusema wimbo mpya wa Nay wa ‘Wapo’ unapaswa kuboreshwa zaidi na ulivyo sasa ni mzuri tu, itakuwa sehemu ya kubadili mwenendo duni wa Basata ambao wamekuwa wakipita katika njia walizopita kwa kipindi sasa.


Viongozi wa Basata walianza kusema mapema siku ya Ijumaa iliyopita, kuwa siku hiyo waliusikia wimbo huo. Jumamosi na Jumapili hawakuwa kazini, wanatarajia kukaa Jumatatu na kuufungia.


Walijua wataufungia, wakachagizwa zaidi baada ya kusikia Nay amekamatwa na Polisi Morogoro akiwa njiani kwenda Dodoma. Taarifa za awali zilieleza lilikuwa ni agizo la mkuu wa mkoa, haikuelezwa wa wapi! Baada ya hapo, Jumatatu, Basata wakapitisha panga.

Wao waliamini wana uwezo wa kuufungia bila kuangalia hata chembe ya ujumbe kwamba kuna mambo yenye faida na jamii na huenda kumpa muda Nay afanye marekebisho, la sivyo ufungiwe.

Wamewahi kujaribu kuwashauri wasanii hivyo huko nyuma? Lakini wanaonekana kufungia ndiyo imekuwa “kauli mbiu” kwao na si jambo sahihi.


Muda mfupi baada ya kuufungia, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, akatangaza kuruhusu uendelee kupigwa na kueleza Rais Magufuli amevutiwa nao na ameshauri mambo kadhaa kuboreshwa kama vile kuingiza wakwepa kodi…WAPO, na kadhalika.


Rais Magufuli si mtendaji wa Basata, lakini anaweza kujua kuwa wimbo una ujumbe hata kuliko wataalamu wa Basata!
Najiuliza, Basata hawajui kuwa kuna viongozi wanaofanya kazi kwa kutafuta kiki? Viongozi wa serikali waliofoji vyeti? Wanawake wanaosagana au wanaume wanaolelewa?


Viongozi wavuta bangi? Wasanii mateja? Lile la malinda sikulielewa, tuwaachie wenyewe! Lakini najua Basata wanajua mastaa wanajiuza, tena wakiwa ni watu wenye heshima mbele ya jamii!


Kosa la Nay kubwa lilikuwa ni kumuulizia Bashite? Nani asiyemjua na imeandikwa mara ngapi? Kwa nini Basata walikubali kuingia kwenye ile tabia mbaya inayozidi nafasi, ya kuwatisha watu wanaokosoa, kuwajengea chuki na kuwafanya waonekane maadui kwa kuwa tu wanakosoa?

Nchi hii haiwezi kuendeshwa kwa mawazo ya watu wawili watatu, haiwezi kuendeshwa kwa watu fulani kuona wanajua kila kitu. Lazima kuwe na nafasi ya wananchi kutoa maoni yao au mawazo.

Basata inapaswa kujua, hata huo wimbo ulioruhusiwa na Rais Magufuli, bado una walakini na kwa kuwa ndiye mkuu wa nchi, hawawezi kupinga, lakini wanaweza kumshauri Nay kuboresha baadhi ya sehemu ambazo wanaona zinakiuka maadili ili ukitoka, uwe unakidhi na kufiti kwa jamii.

Ujumbe wa wimbo wake ni mkubwa na ulistahili kufikishwa. Naweza kusema “meseji sent”. Lakini sehemu ambazo zinaonyesha zinauzuia kusikilizwa na watoto na wadogo zetu zibadilishwe ili kutanua wigo wa usikilizwaji wake.Lakini msisitizo wangu, Basata sasa waamke, waache kufanya kazi kwa kufuata upepo na badala yake kuonyesha ni wataalamu ambao hata kama jamii itataka tofauti, wao waonyeshe wanachoona ni sahihi na wasiwe inavyokwenda ndiko wanakoelekea. Wajiondoe huko, maana katika viongozi wanaofanya kazi kutaka kiki, “Basata Wapo”.

SOURCE: CHAMPIONI.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV