March 25, 2017
Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga leo atakaa kwa mara ya kwanza kwenye benchi la ufundi la timu hiyo huku akiwa na kombinesheni mpya ya safu ya ushambuliaji ya Mbwana Samatta na Ibrahim Ajibu.

Mayanga alikabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi hicho hivi karibuni akimrithi, Boniface Mkwasa ambaye hivi sasa ni katibu mkuu wa Yanga.

Kocha huyo, anakaa benchi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana utakaopigwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mayanga alionekana akitengeneza kombisheni  kwenye mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Taifa mapema wiki hii.

Katika mazoezi hayo, Mayanga alitengeneza vikosi viwili na kucheza mechi ya mazoezi na kuwapanga pamoja Samatta na Ajibu walioonekana kucheza kwa kuelewana huku wakifuata maelekezo yake.

Ajibu ameingia kwenye kombinesheni ya Samatta baada ya kukosekana mshambuliaji, Thomas Ulimwengu anayekipiga AFC Eskilstuna ya Sweden. Ulimwengu ana majeraha.

Kikosi kingine alichokipanga Mayanga, safu ya ushambuliaji walicheza, Mbaraka Yusuph wa Kagera Sugar na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting ambao ni ingizo jipya Taifa Stars.

Wakati mazoezi hayo yanaendelea, Mayanga aliwajaribu Mbaraka na Abdulrahman kwenye kombinesheni ya Samatta kabla ya Ajibu kuonekana ndiye anayefaa zaidi.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV