Na Saleh Ally
YANGA imetangaza kukatisha mkataba wake na Mkurugenzi wa Ufundi, Hans va der Pluilm raia wa Uholanzi.
Kabla Pluijm alikuwa kocha wa Yanga kipenzi cha mashabiki wengi wa kikosi hicho. Alikuwa ndiye kocha alionekana mkombozi wa kikosi hicho.
Kama unakumbuka, ameifikisha Yanga katika hatua ya makundi Kombe la Shirikisho na kweli kilikuwa kikosi bora hadi kufikia hatua hiyo.
Wakati Yanga inavuka ikitokea Angola, ilikuwa vita hasa na Waangola walipanga kuidhulumu, lakini ubora wa kikosi chake na juhudi za viongozi ziliisaidia Yanga kuvuka, haikuwa rahisi.
Lakini wakati inafikia huko, Yanga ilikuwa imebeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho, pia halikuwa jambo rahisi pia. Hivyo hauwezi kusema wewe ni mpenda michezo halafu hauijui kazi ya kocha huyo ambaye maisha yake ni nchini Ghana ambako ameoa na ana watoto wawili.
Mwisho Yanga iliamua kumchukua George Lwandamina kwamba ilitaka kujiongeza zaidi kwa kuwa kocha huyo raia wa Zambia alifanikiwa kuifikisha Zesco mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Walisema mbali lakini unaweza kusema ni hatua sawa na Yanga, hatua ya makundi. Ila hadhi inakuwa juu kwa kuwa hii ni Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya Yanga ni Kombe la Shirikisho, sawa na Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa Cup.
Hadhi inaweza kujengwa kwa hisia na mtazamo au hali halisi kwa kuwa hii inaonekana kubwa na ile ndogo. Hii ni kutokana na hadhi zilizopewa kifedha na mfumo. Lakini uweli timu yoyote inaweza kushiriki huku au kule na ikakutana na ugumu uleule au ukapishana kidogo sana.
Kazi waliyoifanya hawa makocha wawili, kwangu kama mtazamo haikuwa na tofauti kubwa sana na kama Yanga waliitaka hiyo tofauti, basi ilikuwa ndogo sana na hawakupaswa kuwa na papara zaidi.
Kuamua kumchukua Lwandamina, sikuona ni kama jambo lenye afya sana. Lakini walipoamua kumbakiza tena Pluijm, ndiyo nikaona hawakuwa wabunifu, walinishangaza na kama unakumbuka nililizungumzia hilo.
Kubaki kwake, ilikuwa ni kitu cha ajabu kwa kuwa huyu uliyeona anahitaji mtu kusonga mbele. Unamleta mtu halafu yule mtu anakuja kuwa chini yake, kilikuwa kichekesho fulani hivi, nilieleza.
Nilisema wazi kuanzia mwanzo, ilikuwa ni lazima Yanga wamtokea mmoja wao. Waamue kubaki tena na Pluijm au aende zake ili Lwandamina apate nafasi kubwa ya kufanya kazi zake.
Utaona, kila kibaya kilichokuwa kinatokea, kiligeuka na kuwa “mali” ya Pluijm. Yale mambo ya Donaldo Ngoma au Vincent Bossou, kila mtu alikuwa na nafasi ya kuhisi.
Maneno yalikuwa mengi, “unajua yule anafanya vile kwa kuwa anampenda sana Pluijm.” Au “unajua yule amekasirishwa sana na Pluijm kuondolewa ukocha?” Basi ilikuwa ili mradi kila mmoja ana lake la kusema na kocha huyo Mholanzi alitumika kama sehemu ya chupa yenye mafuta ambayo ilitumika kupoza kila jambo la fulani aliyekosea.
Hata kama Yanga ilipokosea, yeye ndiye alitumiwa kama chupa inayoteleza mgongoni. Kwamba Lwandamina hayupo huru ndiyo maana. Ikishinda, hakuna aliyesema alisaidia kushinda.
Lakini kulikuwa na mgawanyo wa bila kukusudia. Maana wako wanaoamini Lwandamina anaweza hana nafasi ya kutosha na wengine waliona Pluijm ni mwisho wa maneno. Ikawa ushindani wa “namba” kwa makocha!
Lakini sasa, ameondoka na imekuwa ni jambo zuri na ninaamini tutarudi kwenye kile nilichokuwa nakitaka hapo awali. Kwamba abaki Lwandamina akiwa huru ili awape Yanga kile ambacho walikuwa wanakihitaji.
Safari hii itakuwa vizuri sana kwa kuwa Yanga wakiharibu, wataangalia wapi pa kurekebisha na wataendana na ukweli na si kuanza kumuwaza Pluijm ndiye chanzo au sababu.
Sasa ni wakati wa kujua Lwandamina ana nini na anahitaji nini kama ni msaada au vinginevyo.
Aumuzi wa kumuacha Pluijm ni mzuri na utakuwa msaada mkubwa kwa Yanga kujua nini walichonacho na kama kimepungua ni kiasi gani na si kila siku, “ni kwa sababu ya Pluijm” . Sasa acha tuone na tupime kitaalamu na vurugu.
0 COMMENTS:
Post a Comment