Simba leo Jumamosi inacheza na Mbeya City mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, klabu hiyo imesema wapinzani wao wamekuja wakati mbaya kwao.
Kocha wa Simba, Joseph Omog, raia wa Cameroon, amesema Mbeya City imekuja kipindi ambacho timu yake inataka ushindi kwa lazima ili wawe katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Omog alisema pia Mbeya City inakutana na beki Juuko Murshid ambaye hakuwepo kikosini tangu kuanza kwa mwaka huu. Juuko, raia wa Uganda, Januari, mwaka huu, alikuwa Gabon akiiwakilisha nchi yake katika Kombe la Mataifa ya Afrika.
Simba ina pointi 54 kileleni mwa ligi hiyo ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 52, wakati Mbeya City ikiwa nafasi ya nane na pointi 29 huku Mtibwa Sugar ikiwa na pointi 33 katika nafasi ya tano.
“Wapinzani wetu wamekuja wakati mbaya sana, kwani sisi tunasaka pointi tatu kwa juhudi zote ili wasipotee katika mbio za ubingwa, pili ni kurejea kwa beki wetu Juuko.
“Safu yetu ya ulinzi imeimarika kuweza kupambana na timu yoyote.”
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri, raia wa Malawi, alisema: “Tumejipanga kushinda mchezo huu, kikosini tuna nyota wengi wenye uzoefu, tutawatumia kuifunga Simba.”
0 COMMENTS:
Post a Comment