March 31, 2017Na Saleh Ally
GUMZO kubwa katika kipindi hiki katika Ligi Kuu Tanzania Bara ni mechi sita ambazo wamebakiza vigogo wa soka Tanzania, Yanga na Simba.

Yanga ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na Simba ni vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 55 wakifuatiwa na watani wao wenye 53.

Kwanza, ili kuweka mambo sawa, hakuna timu hata moja kati ya Yanga yenye nafasi kubwa zaidi ya kubeba ubingwa zaidi ya mwenzake kulingana na hali halisi ilivyo.

Pointi mbili, hata ingekuwa mechi mbili zimebaki, si jambo la upande wowote kuona uko salama. Kama kweli Simba wangekuwa na pengo la pointi nane kama walivyowahi kufanya dhidi ya Yanga wakati wa mzunguko wa kwanza, basi wangekuwa na uhakika kwa asilimia kubwa sana.

Mechi sita zinakuwa na jumla ya pointi 18, ukiangalia pengo ni pointi mbili. Hapa Simba akifungwa, Yanga akishinda mambo yanabadilika kabisa lakini inawezekana hiyo advantage ya Simba ikaanza kuonekana kama Yanga hawatashinda dhidi ya Azam, mfano wapoteze na Simba ashinde.

Faida sahihi ni kuwa na zaidi ya pointi tatu pengo. Maana yake hata kama utapoteza na mwingine akashinda bado anakuwa hajakufikia.

Hivyo kila timu kati ya Yanga na Simba, zote ziko sawa katika mbio za kuwania ubingwa na hili linapaswa kufahamika.

Lakini wakati ligi inakwenda ukingoni, gumzo la chinichini ambalo liko wazi kwa wapenzi wa Simba na Yanga ni timu moja kucheza mechi za timu nyingine.

Ukiwasikia Yanga wamekuwa wakilalama kwamba Simba wanacheza zao, hali kadhalika Simba nao wanalalamika kuwa Yanga wanacheza zao ili kuhakikisha mmoja anafanikiwa.

Kucheza kunaweza kuwa kwa njia nyingi lakini nijuavyo ni hivi. Yanga wakiona Simba inacheza na Kagera, wanaweza kwenda kutoa motisha, kwamba Kagera wapambane ili kuhakikisha wanaizuia Yanga. Hapa Simba wanaweza kutoa ahadi au vinginevyo.

Kuna lawama ya kwamba, kuna timu moja inaweza hadi kwenda kuwahadaa waamuzi au wachezaji fulani kuhusiana na kuhakikisha timu fulani inapoteza.

Advantage hapa inakuwa hivi, kama timu itapoteza, mfano iwe Simba, basi Yanga itafanya juhudi kushinda na kukaa kileleni. Kwa Simba ikifanikiwa hivyo halafu ikashinda, basi itatanua pengo.

Haya mambo yamekuwa yakionekana kama hadithi za mtaani tu lakini kiuhalisia yapo na viongozi wa klabu za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza Bara pia wanaweza kuwa shahidi katika hili.
Najua huenda msingependa kulizungumzia kwa kuwa linawagusa moja kwa moja. Si jambo zuri, si jambo la kujivunia, naweza kusema ni ubunifu dhaifu ambao unaonyesha ukosefu wa fikra sahihi.

Kama unakwenda kuwapa fedha kama motisha wachezaji wa timu pinzani inayocheza na mpinzani wako, kwa nini usiwape wachezaji wako kama sehemu ya motisha ili wapambane zaidi?

Kama wewe ni kiongozi, mnafanikiwa kubeba ubingwa kwa “kucheza mechi” za wenzako, unajifikiriaje? Unawezaje kuidanganya nafsi yako kuwa kweli mlikuwa na kikosi bora?

Pia kama wewe ni kiongozi, timu yako imebeba ubingwa mara kadhaa huku mambo yakiwa yalifanikishwa kwa “kucheza” mechi za kina nanihii, vipi utaona mlisajili wachezaji bora na kuajiri kocha sahihi?

Kipimo cha ubora wa kazi unazofanya ni usahihi na uaminifu. Kwenye soka, timu bora inajengwa na wachezaji bora, kocha sahihi na uongozi wenye mwenendo sahihi katika kipindi husika.

Kuna kila sababu ya viongozi kama bado mnaendelea kufanya hivi hasa kwa kuwa ligi kuu inakwenda ukingoni. Basi itakuwa vizuri sana kila mmoja “akicheza” mechi zake ili mpime ubora wenu kwa mzani sahihi.1 COMMENTS:

  1. Well say,lakini Saleh ni vema tujue Kunakazi kubwa sana kuondoa hilo.hiki unachokiona ni matokeo.na kamwe hatuwezi kutibu matokeo,tatizo kubwa ni mentality,ambayo imefungwa kwenye packege ya historia.jambo kama hl halihitaji mtu mmoja kulibadili,tunaswa kuwekeza mtazamo mpya kwa vijana kwa mfumo wa uongozi ambao ufahamu wao utaweza kutenga kasumba na malengo,ujinga na sifa bila kuondoa ladha ya utani wa jadi wa nchi yetu.kwa hy kuwa watani wa jadi kutatumika Kama katalist na sio eneo la udumavu

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV