March 31, 2017
Na Saleh Ally
LIGI Daraja la Kwanza nchini England ni ngumu sana na wakati mwingine wapo ambao wamekuwa wakiamini ni ngumu hata kuliko Premier League.

Kwanza ina mechi nyingi zaidi kwa kuwa timu kumaliza ligi, inatakiwa kucheza mechi 46, si kidogo.

Ukiachana na hivyo, ushindani wake uko juu, mechi zipo karibukaribu na utaona timu kama Leicester City imeweza kupanda na kwenda kubeba Ligi Kuu England, moja kwa moja.

Wakati Leicester walifanya hivyo, kuna wabishi wanaitwa Brighton & Hove Albion FC ambao wana nafasi kubwa ya kuingia Ligi Kuu England msimu ujao.

Brighton & Hove Albion FC kwa sasa wako katika nafasi ya pili kwenye Championship wakiwa na pointi 37, nyuma ya Newcastle ambao ni vinara wenye pointi 38.Katika mechi sita, wamepoteza tatu na kushinda tatu, lakini unaweza kushangazwa na kuwaona wakiwa katika nafasi ya pili wakiwa na tofauti ya pointi moja na vinara Newcastle inayofundishwa na Rafa Benitez, mmoja wa makocha wakubwa duniani.

Zimebaki mechi kama nane ambazo zitaamua mwisho nani amepanda na kawaida ni timu mbili tu zinatakiwa kupanda moja kwa moja, halafu inatafutwa timu moja katika mechi za mtoano.

Awali, Newcastle ilikuwa ikipewa nafasi kubwa lakini Brighton & Hove Albion FC inayoongozwa na Kocha Chris Hughton inaonekana kuwa na mwendo wa kuwatisha wengine.

Bado haina nafasi lakini aina ya wachezaji wake kujituma, mfumo uliotengenezwa kwenye kikosi hicho kuifanya timu hiyo kuwa kama familia moja isiyotaka kushindwa, inaonekana hakuna wa kuwazuia kupanda Premier League msimu ujao.

Hughton ni kocha mzoefu, kwani amewahi kuzinoa Tottenham na West Ham United kwenye Premier League na sasa anaonekana kupania kurejea akiwa na Brighton & Hove Albion FC.Wanahitaji kushinda mechi nne kati ya nane, zitakuwa zimewahakikishia kwa asilimia 88 kupanda Ligi Kuu England. Kikubwa ni kulinda kupoteza zaidi ya mechi tatu, kitu ambacho kinaonekana wanaweza.

Brighton & Hove Albion FC maarufu kama The Seagulls au Albion ni timu iliyoanzishwa Juni 24, 1901 yaani miaka 115 iliyopita katika Mji wa Brighton na Hove, Sussex Mashariki, England.

Uwanja wa nyumbani wa Brighton unaitwa Falmer na una uwezo wa kuchukua mashabiki 30,750 lakini kutokana na udhamini wa American Express, sasa uwanja huo unaitwa American Express au Amex.

Baada ya kuanzishwa mwaka 1901, Brighton ilianza kucheza ligi ndogondogo ikiwemo Ligi ya Ukanda wa Kusini hadi ilipoanza kucheza ligi ya juu mwaka 1920.

Klabu hii ilipata mafanikio makubwa kati ya mwaka 1979 na 1983 ilipocheza Ligi Daraja la Kwanza na kufanikiwa kufika fainali ya Kombe la FA mwaka 1983 dhidi ya Manchester United.

Katika fainali hiyo ya FA, Brighton ilifungwa na Man United mabao 4-0 katika mechi ya marudiano baada ya awali kutoka sare ya mabao 2-2 na msimu huohuo ikashuka daraja kutokana na matatizo ya kiuongozi.

Ikajitahidi kurejea katika ligi za juu na kufanikiwa tena lakini ilibaki kidogo ishuke daraja kati ya mwaka 1997 na 1998 kutokana na tatizo la uongozi kwa mara nyingine. 

Kilichowaokoa ni kitendo cha bodi ya timu hiyo kuamua kuiongoza timu moja kwa moja na tangu iliporejea Ligi Daraja la Kwanza mwaka 2002, haikuwahi kushuka madaraja ya chini zaidi ya kuishia daraja la kwanza na la pili hadi sasa.

Katika miaka hii ya 2000, Brighton iliamua kurudi nyuma na kutumia nembo yake ya zamani ikiwa ni kuheshimu kitendo chao cha kurejea kwenye uwanja wao wa nyumbani walipouacha tangu mwaka 1997.

Uwanja wa Amex ambao sasa unaitwa American Express, ulianza kutumiwa tena katika msimu wa 2011/12 dhidi ya Doncaster Rovers, ambayo pia ilikuwa timu ya mwisho ya upinzani kucheza uwanjani hapo mwaka 1997.

Msimu wa 2015/16, Brighton ilicheza mechi 22 bila kufungwa hadi Desemba 19, 2015, walipofungwa na Middlesbrough mabao 3–0 na kutibuliwa harakati zao za kupanda ligi kuu.KOCHA CHRIS HUGHTON
Brighton sasa ipo chini ya Kocha Chris Hughton, 58, ambaye alichukua mikoba ya nyota wa zamani wa Liverpool, Sami Hyypia aliyeachia ngazi Desemba 2014, na tangu hapo amekuwa na mafanikio klabuni.

Katika mechi yake ya kwanza Brighton, Hughton aliifunga Brentford mabao 2-0 katika mchezo wa Kombe la FA. Katika mechi yake ya kwanza ya ligi, Brighton iliifunga Charlton bao 1–0. Katika msimu huo wa 2014/15, Brighton iliepuka kushuka daraja na ikamaliza ligi katika nafasi ya 20.

Hughton si kocha wa masihara kwani enzi zake alikuwa akicheza nafasi ya beki wa kushoto na kufanya vizuri katika klabu za Tottenham Hotspur (1977-1990), West Ham United (1990-1992) na Brentford kati ya mwaka 1992 hadi 1993.

Pia Hughton amewahi kuwa kocha wa muda katika klabu za Spurs mwaka 1997, Newcastle (2008) na kutokana na utendaji wake akawa kocha mkuu Newcastle mwaka 2009 hadi 2010, Birmingham City (2011-2012) na Norwich City mwaka 2012 hadi 2014 alipojiunga na Brighton.Matokeo ya Brighton LLWWL
MECHI TANO ZA MWISHO
28/02/17    Brighton 1 – 2 Newcastle United
04/03/17    Nottingham Forest 3 – 0 Brighton         
07/03/17    Rotherham United 0 – 2 Brighton
10/03/17    Brighton 3 – 0 Derby County      
18/03/17    Leeds United 2 – 0 Brighton        

MECHI TANO ZIJAZO
Kesho Jumamosi Brighton v Blackburn Rovers               
04/04/17    Brighton v Birmingham City                 
07/04/17    QPR v Brighton          
14/04/17    Wolverhampton v Brighton
17/04/17    Brighton v Wigan Athletic  

MSIMAMO
                             P       W      D       L       GF    GA    GD    Pts   
1. Newcastle         38      24     6       8       70     32     +38   78    
2. Brighton           38      23      8       7       63     33     +30   77
3. Huddersfield     37      22     5       10     47      43      +4     71    
4. Leeds               38      21      6       11     52     36     +16   69FIN.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV