April 14, 2017



Na Saleh Ally
USHABIKI wa michezo ni furaha, ukiuendekeza mara nyingi unavuka mipaka kutoka katika furaha na mwisho unakuharibia mambo mengi sana ya muhimu.


Ushabiki wa michezo na hasa soka, umewagombanisha wengi na rafiki na ndugu zao. Umewajengea wengi uadui na wengine, umeanzisha misigano na kutoelewana kwa wengi.


Wapo waliopoteza kazi zao au hata kuingia katika migogoro kwa majirani au familia zao lakini yote yanatokana na migogoro inayotokana na ushabiki wa kupindukia.


Hakika ushabiki haupaswi kuwa wa kupindukia na kufikia kujenga uadui au makundi yanayoeneza chuki na kupoteza kabisa maana ya ushabiki wenyewe.



Labda nikukumbushe Rwanda baada ya kupita katika mauaji ya kimbari mwaka 1994 waliutumia mchezo wa mpira kuwakutanisha wananchi wake, safari hii wakijulikana kama Wanyarwanda na kwa pamoja wakafuta yale mambo ya makabila matatu, Watutsi, Wahutu na Watwa.


Unakuta Mtutsi na Mhutu kwa pamoja wanashabikia APR na Mtusi, Mtwa na Mhutu wanashangilia Rayon. Kwa pamoja wanaungana na taratibu wakaanza kusahau machungu na kuondoa visasi, watu wakasameheana na kuanza kuishi maisha mapya.


Nchi nyingi zimetumia njia hiyo kuhakikisha zinarejea katika mstari sahihi kwa kuwa furaha ya michezo inayojenga ushabiki inaweza kuwa furaha na faida badala ya hasara.


Juzi, mashabiki wa Borussia Dortmund ya Ujerumani walifanya kitu kingine kinachoweza kukumbukwa kwa muda mrefu hasa tunapozungumzia faida ya ushabiki.


Mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Dortmund na AS Monaco ya Ufaransa ilitarajiwa kuchezwa Jumanne mjini Dortmund, Ujerumani. Lakini wakati basi la wachezaji wa wenyeji likiwa njiani, lilishambuliwa na milipuko mitatu, hivyo kusababisha mechi kusogezwa mbele.


Hatua hiyo ilivuruga ratiba ya mashabiki wa AS Monaco ambao walijua wangeondoka usiku baada ya mechi na wengine alfajiri kurejea Ufaransa. Lakini sasa walilazimika kusubiri hadi Jumatano kwa kuwa mechi ilisogezwa ili waondoke Alhamisi. Gharama ikaongezeka kwao na bajeti ikavurugika.



Iliwezekana wangeanza kurejea Jumatano bila kuona mechi kwa kuwa hawakuwa na ujanja. Lakini mashabiki wa Dortmund walitaka wenzao waone mechi yao na walichofanya ni kuzungumza, wakajiunganisha na kuanza kuwaalika.

Karibu kila familia yenye mashabiki wa Dortmund ilialika mashabiki kadhaa wa Monaco ambao bajeti yao ilikuwa imevurugika, wakala nao, wakanywa nao na hata wengine wakalala katika majumba yao.


Juzi Jumatano, mechi ikachezwa na wenyeji wakalala kwa mabao 3-2. Wana deni watakapokwenda Monaco, Ufaransa kuhakikisha wanawashinda wenyeji wao ili wasonge mbele. Lakini mashabiki wao wanaingia kwenye rekodi ya kuwa moja ya mashabiki wa aina yake.


Mashabiki wa Dortmund wameonyesha ushabiki ni zaidi ya furaha kwa timu, badala yake ndani yake kunaweza kuwa na urafiki, undugu na kuthamini au kujali furaha ya mwingine.
Vipi wewe shabiki wa Simba, unampiga yule wa Yanga  bila kosa kwa kuwa tu amevaa nguo za njano kwenye jukwaa la upande wa Simba? Ukimuelekeza na kumueleza si sehemu sahihi kwake, tatizo ni nini?

Ukiingia uwanjani wewe shabiki wa Yanga, ukashangilia kwa juhudi na kufurahi na wenzako bila kumtukana matusi ya nguoni yule wa Simba, hasara yako ni ipi?


Mashabiki wengi hasa wa soka hapa nchini wanataka kuonyesha mchezo wa soka si wa kiungwana, ni mchezo wa kibabe, mchezo wa wahuni au watu wasio na mpangilio. Jambo ambalo si kweli hata kidogo, badala yake ni nguvu ya wapuuzi wachache wenye nguvu inayowapa ruhusa kuonyesha upuuzi wao mbele ya wengine.


Unaweza kufurahia au kusherehekea bila kuumiza wengine, bila kuwabugudhi au kuwadhalilisha. Somo la mashabiki wa Dortmund, linatoa funzo kwa mashabiki wengi wa soka duniani lakini wale wa Yanga na Simba, hili ni lenu na ndio mnahusika hasa, jifunzeni.


SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

  1. "Kijinga"..mbona mnapenda sana kulitumiw hili neno hata katika sehemu lisipo hitajika?...simba na yanga ni watani kama ilivyo barca na Madrid then unaweza kuwalinganisha na Dortmund na monaco???.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic