April 10, 2017


Na Saleh Ally
NARUDI nyuma kidogo, nataka kukumbusha namna ambavyo niliwahi kuandika kuhusiana na namna ambavyo mwanamuziki Nasibu Abdul, maarufu kama Diamond, kwamba ameanza kukosea vitu kadhaa, hasa kuiga video za wasanii wengine.


Nilieleza kwa mifano ya picha namna ambavyo Diamond aliiga karibu kila kitu kutoka katika video ya msanii mmoja, kuweka kwenye video yake. Halafu akarudia namna hiyo baadaye, jambo nililoliona ni la kustaajabisha kabisa kwa kuwa wimbo huo aliouiga haukuwa hata na miaka miwili sokoni!

Baada ya kuandika, nikaweka kila kitu kwa mifano. Kilichofuata ni baadhi ya watu walio na Diamond kuanza kulalama kwamba ninamsakama.

Mbaya zaidi, mwandishi mmoja wa Mwananchi ambaye ni kati ya watu niliowafundisha namna ya uandishi bora wa uandishi wa burudani alinifuata na kuhoji mbona “natumiwa”, kumsakama Diamond. Nilimuuliza maswali kupitia makala niliyoandika, hakuna alichojibu!

Baadaye niligundua ameingia kwenye mkumbo wa zile “Team”, jambo ambalo ni baya kabisa kwa mwandishi.

Lakini hivi karibuni, Diamond alikosolewa kwa nia njema kabisa kuwa vizuri akawa anafanya shoo za nyumbani kwa ajili ya watu wake ambao ndio wanaomfanya leo asikike kote duniani.

Mhamasishaji na mjasiriamali, Eric Shigongo alishauri hivyo akitaka Diamond na uongozi wake, kupunguza bei za shoo kwa mapromota ili nao watoze viingilio vya chini kwa Watanzania. Nalo hilo likawa kosa, Meneja wake Babu Tale, akacharuka kwamba kazi yake inaharibiwa akiamini eti, Diamond anashambuliwa!

Baada ya hapo akaanza vitisho eti atamuandika vibaya Shigongo mtandaoni, kwa madai yeye ni maarufu huko mtandaoni kwa kuwa ana watu milioni 1 wanaomfuatilia! Akafanya hivyo, hakukuwa na faida yoyote kwake, zaidi ya yeye kushambuliwa, watu wakiamini hakuelewa!

Tale hakuwa amejibu hoja hata kidogo kuhusiana na kilichoandikwa kama ilivyokuwa awali, zaidi ya kusema maneno mengi akitoa data za uongo huku akitengeneza filamu eti katishiwa kuuawa.

Hii inaonyesha kiasi gani Diamond amezungukwa na watu wanaoweza kumtengenezea mazingira ya kuwa hawezi kushauriwa, hawezi kuhojiwa, ni mtu anayejua sana na wao wanajua kila kitu cha muziki wakati rekodi zinaonyesha waliofaulu zaidi ni waliokubali kukosolewa.

Picha inayotengenezwa, kumueleza jambo Diamond kwa nia nzuri ni kumshambulia. Picha inayotangulizwa, chochote atakachofanya Diamond aachwe, “yeye ni yeye.” Mimi ninaamini hilo halitakuwa na nafasi na kwa kuwa ni msanii wa Tanzania, ataambiwa na mimi safari hii naendelea kumuambia bila ya hofu ya huo mtandao wa watu milioni moja wa Babu Tale na vizuri atakayetaka kuzungumza na mimi, twende kwa hoja ili tujenge.

Kutishiana mtandaoni eti watu watakutukana ni mambo ya kipuuzi ambayo wakati mwingine hupaswi kuyasikia yakizungumzwa na mtu unayeamini amefikia kiwango cha kuitwa kiongozi.
Diamond ametoa wimbo mpya uitwao “Acha Nikae Kimya”. Tayari mashabiki wengi wa muziki wameanza kumshambulia Diamond mitandaoni.

Nimeona wakishambulia katika hali ambayo inaonyesha wazi kuwa wamekerwa na uamuzi wake wa kutoa wimbo ambao ukiusikiliza kwa makini umelenga kumsafisha mkuu wa mkoa ambaye yuko katika sakata la vyeti.

Lengo ni kuona mkuu wa mkoa huyo anarejea katika heshima aliyopewa na wananchi hapo awali, lakini baadaye wakaichukua wananchi hao baada ya kuona hawastahili kumpa hasa baada ya kushindwa kulimaza suala walilohoji naye akashindwa kujibu na zaidi ikawa ni kutishiana tu.

Ndani ya wimbo huo unaoonyesha wazi unalenga kutengeneza mazingira ya kupoza hali iliyopo mfano, kama kile kipande anachosema: “Nyumbani nafungua geti, niende kwa Mangi kununua supageti, napewa za chini ya kapeti, kuna redio imevamiwa eti.”

Najua ukimuuliza atasema alikuwa anatafuta vina, lakini baada ya redio imevamiwa, neno eti, linamaanisha hakuna uhakika.
Hii yote ni kuonyesha kuwa hakuna redio iliyovamiwa kama ambavyo wengi wamekuwa wakifikiria. Kwa waliovamiwa na walio karibu yao au waliounganisha machungu katika hili ni sawa na kuwatonesha kidonda.


Najua ndani ya waandishi wenyewe wako walio tayari kugawanya machungu. Lakini ukweli mwenye akili timamu hakuna anayeweza kuunga mkono chombo cha habari kuvamiwa kwa visingizio visivyokuwa na msingi. Hata Diamond, amekuzwa kufikia alipo na vyombo vya habari hata anavyovidharau akaamini vinazidiwa na mtandao, ndiyo vilimpa nafasi watu wakamjua!
Kama hiyo haitoshi, kuna sehemu anaimba hivi;

“Napita kwenye magazeti, nakuta rundo la watu wameketi, badala ya kutafuta senti, wanabishana tu mambo ya vyeti. Acha nikae kimyaaa.”

Hii ni kuonyesha kwamba hakuna sababu ya watu kubishana mambo ya vyeti na yeye anawashangaa.

Lakini hakumshangaa kiongozi ambaye ameshindwa kuweka vyeti vyake hadharani baada ya kuonekana kuna walakini. Kiongozi ambaye ameshindwa kuonyesha ni kiongozi thabiti ambaye alipaswa kuwa wazi na kuwathibitishia wananchi wake wanachohoji.


Kama unataka watu wawe safi, unataka watu wafuate taratibu, kanuni na sheria. Vipi wewe umeshindwa kuthibitisha unavyo, uonyeshe? Vipi Diamond anakubali kujiangusha aonekane anafurahia visivyo sahihi? Uko wapi uongozi wake na unashindwa kuona hili? Kwa nini unaachia haya yapite na kunipa mimi nafasi ya kuandika ili kesho wadai ndiye nilimshusha Diamond?
Je, Diamond yuko tayari kuwakandamiza wananchi wote ambao ndiyo wamekuwa wakimsapoti yeye miaka yote kwa ajili ya kumfurahisha mtu mmoja?


Wale wanaomshambulia mitandaoni ni kuonyesha kuwa ni kosa kubwa kuamini una akili nyingi kuliko kila mtu.
Alichotakiwa Diamond ni kukemea vyanzo vya tatizo na si kuwakemea au kuwashangaa wale wanaotaka kuchukua chanzo cha tatizo.


Kama Diamond ameamua kuingia kwenye “siasa nyepesi”, vipi Babu Tale haoni kuwa anaharibu biashara yake? Vipi halalamiki au naye hayuko katika kampeni ya kushika taulo na kufanya usafi wa waliojichafua wenyewe?

Halafu jiulize, huu mjadala si ulifungwa? Sasa Diamond anapouamsha anataka nini? Naye anatumika?
Mimi nataka kuwa huru, nataka kuwa mwandishi ninayesema ukweli bila ya hofu ya kutekwa au kuwekwa ndani eti kwa kuwa nimemuambia mtu fulani ukweli.

Nataka kuwa huru na kusema ukweli kwa lengo la kuweka mambo sawa na kurekebisha taifa langu bila ya kuogopa eti mtu mzima mwenye akili zake atanitishia kuniweka nitukanwe mtandaoni.

Nasema sitaogopa kwa sababu viongozi wa mikoa waliopewa dhamana ya kutuongoza wanataka kututisha kwa kuwa wana uwezo wa kukuweka ndani mwandishi hasa wale wanaoonyesha si wapambe wao.

Diamond aachane na “siasa nyepesi”, anatakiwa kuusoma upepo na kuwa “intelligent” badala ya kukubali kutumiwa kusafisha mkono wa wenzake huku wa kwake ukijaa masizi.


Kuna ule msemo wa sanaa usemao hivi: “Music expresses that which cannot be said and on which it is impossible to be silent.”. Muziki unaweza kufafanua kile ambacho hakiwezi kuzungumzwa, tena katika kipindi ambacho haiwezekani kuwa kimya.
Huenda ulikuwa wakati mzuri kwake Diamond kuchagua kukaa kimya kweli, kuliko kusema yuko kimya huku akijaribu kuonyesha Watanzania hawawezi kuelewa.


Badala ya kukimbilia udhaifu ili kufurahisha nafsi ya mtu, kama angetaka kusema, angeonyesha ni imara kueleza kile ambacho hakielezeki katika kipindi ambacho watu wako kimya.
Wanaokasirika wanajua wanataka kufanywa wapuuzi. Waliolalamika wanakasirishwa na kuonyesha wanacholalamika wao ni kazi bure.


Mimi nashangazwa na Diamond anayetaka kubomoa matofali ya ukuta wa nyumba yake aliyoijenga kwa shida huku akitaka kujenga ukuta wa jirani aliyeubomoa wa kwake baada ya kulewa sifa.


Muziki kila mmoja ana mwisho wake, hakuna aliyewahi kutamba milele. Nimepata bahati ya kuwaona wanamuzi wengi maarufu nikiwa mwandishi chipukizi na mwandishi bora wa burudani wa nchi hii.

Nakumbuka ufalme wa Mr 2, wakati huo tukimuita 2Proud, usimsahau Profesa Jay. Nakumbuka ufalme wa miaka ya Juma Nature, baadaye makundi ya TMK na East Coast. Nakukumbusha umalkia wa Lady Jaydee. Najua hautakuwa umemsahau Mr Nice.


Ufalme unaweza kuwa wa muda mrefu au ukaporomoka haraka kulingana na mmiliki wa ufalme mwenyewe. Ninaamini siku moja atakuja mfalme mpya au kipenzi kipya cha Watanzania. Lakini ni vizuri Diamond akaepuka kuharibu kazi ya Babu Tale na ikiwezekana kuhakikisha anajenga misingi mizuri ili ukifika wakati wa kuondoka, aondoke kwa heshima. Wakati huo, Watanzania watakuwa wakiendelea na mfalme mwingine na hayo ndiyo maisha bora.

SOURCE: CHAMPIONI2 COMMENTS:

  1. HATA WEWE UNATUMIWA AU NI UTIMU UMEKUPOFUA

    kuhusu suala la shigongo kutaka kupunguzwa bei kwa shoo sio suala la ushauri ni mgongano wa kimaslahi kila mtu akivutia kwake
    na kwenye acha nikae kimya ni suala la kuruhusu mawazo tofauti usitake kila mtu awe na mawazo yako tu

    ReplyDelete
  2. Nilikua nakuheshim sana bro jembe,lakini una chuki isiyo dhahiri kwa diamond kila MTU anayo haki ya kuzungumza na kuamini chochote ila asivunje sheria...diamond kaimba ujinga wake kwa uelewa wake na wewe umeandika ujinga wako kwa mile unacho kiamini diamond katumia sauti wewe kalam kwa ujinga wangu mie nakuona wewe kama yeye tu

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV