April 21, 2017



Na Saleh Ally
HIVI karibuni beki wa kati wa Simba, Abdi Banda alimtwanga ngumi kiungo mkongwe wa Kagera Sugar, George Kavila. Hii ilikuwa ni katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Katika mechi hiyo, Kagera Sugar waliishinda Simba kwa mabao 2-1, lakini gumzo la Banda kumpiga ngumi Kavila likachukua nafasi zaidi, hasa katika mitandao ya kijamii.

Banda alikuwa amerudia jambo hilo ndani ya miezi kadhaa, alimpiga kiwiko kiungo Said Juma ‘Makapu’. Jambo ambalo nililikemea pia, kwamba halikuwa la kiungwana.

Wakati lilipotokea hili la Banda na Kavila, niliendelea kulikemea lakini kuna mambo kadhaa yalijitokeza ambayo nafikiri ni vizuri kuyaongelea leo ili tuweze kujifunza zaidi kwa wale ambao watakuwa waelewa.

Mashabiki wengi wa Yanga au Simba, huamini kuzikosoa timu hizo ni kuzionea. Tena wengi, huwa hawajadili hoja unayoiweka mezani na badala yake kukumbushia matukio kadhaa ambayo huenda yanafanana na hilo unalolielezea au la.

Mfano, wakati nikikemea kuhusiana na tabia ya kipuuzi ambayo alifanya Banda, wengi walikumbusha lile tukio la Amissi Tambwe kumvuta sehemu za siri beki Juuko Murshid au Donald Ngoma alipompiga kichwa kwa makusudi, Hassan Kessy wakati huo akiwa Simba.
Wapo ambao niliwaona ni vilaza waliokuwa wakisema mbona haujawahi kulizungumzia, nawaita vilaza kwa kuwa nililizungumzia suala hilo zaidi ya mara nne. Ninakumbuka mashabiki wa Yanga waliniita “Wewe Simba”, kwa kuwa nilitaka Ngoma aadhibiwe.

Wengine walionyesha pia si wafuatiliaji wakaendelea kusema mbona hukuweka picha ya Tambwe akimvuta Juuko sehemu za siri. Wana uwezo mdogo wa kukumbuka, kwamba picha waliyoiona ilitoka kwenye gazeti hili la Championi na baadaye ikasambaa kwingine.

Hata hilo la Tambwe nilikemea na kuwakumbusha TFF kuchukua hatua kupitia kamati zake. Usahaulifu wao au kukurupuka kukawasahaulisha.

Sasa hawa wengine, walikuwa wakiniita “Wewe Yanga tu njaa”. Kisa nilitaka Banda aadhibiwe ili kukomesha matukio ya kijinga yaliyojaa hisia za kipuuzi na hasa kwa mchezaji mwenye kipaji anayechipukia kama yeye.
Kilichonifurahisha hadi kufikia kuandika leo si suala la Banda kupewa adhabu. Ni namna Banda alivyoonyesha uungwana na kuonyesha ni mtu ambaye ameweza kuamka na kukumbuka kwamba alikosea.

Pamoja na kuwa ni mkosaji lakini kawazidi akili wengi ambao hawakuwa wakosaji. Wale ambao hawakutaka yeye akosolewe kwa ubaya aliokuwa ameufanya kwa sababu ya ushabiki.

Banda alimuomba msamaha Kavila na nimeelezwa, alifungiwa mechi mbili tu kwa kuwa alikuwa ameonyesha uungwana, alijutia kosa lake na aliwaeleza wajumbe kwenye kamati kwamba anajuta na ameahidi kutorudia.

Jiulize wale ambao hawakutaka Banda akosolewe wanajisikiaje? Wanakuwa ni wazazi ambao hawakutaka kukosoa mabaya ya mtoto wao, hawakuwa na fikra chanya zinazoweza kujali marekebisho ya jambo au kitu kwenda kwenye ubora.

Nafikiri kuna kila sababu ya kujifunza na kuachana na tabia ovu kwa sababu ya ushabiki. Naamini ushabiki haumzuii mtu kuwa bora katika nyanja nyingine.

Vizuri kwa mtu anayejitambua asikubali kuficha maovu sababu ya ushabiki na kuipenda timu yako, haina maana utalazimika kuunga mkono hata maovu yake.

Banda akijirekebisha anaweza kuwa bora zaidi. Kama unavyoona sasa, Simba ilimkosa katika mechi mbili na huenda angekuwa msaada mkubwa kama angecheza.

Kumuacha aendelee kufanya maovu huku ukiamini unamsaidia sababu ya ushabiki ni kuonyesha kutojitambua na vizuri kujiwekea kipimo na ujiulize, kwani ushabiki ni nini?


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic