April 24, 2017





Na Saleh Ally
APRILI 13, mwaka huu kamati ya Saa 72 ilikaa na kuamua mchezaji Mohamed Fakhi ana kadi tatu za njano. Ikachukua pointi tatu za Kagera Sugar na kuipatia Simba iliyokaa kileleni mwa Ligi Kuu Bara.

Uamuzi huo wa Kamati ya Saa 72, hadi leo umekuwa hauna uhakika kwa kuwa Kagera Sugar ilikata rufaa katika Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji. Tokea siku hiyo, hadi leo hakuna uhakika kuwa kadi hiyo ilitolewa au la.

Zimepita siku 11, Shirikisho la soka Tanzania (TFF), liko katika wakati mgumu kupata uhakika kama kadi hiyo ya tatu ya njano ya Fakhi ipo au la.

Simba walisema kadi hiyo ipo, wakakata rufaa. Kagera wakasema haikuwepo kwa kuwa kadi ya tatu ya Fakhi ilikuwa dhidi ya African Lyon kwenye Kombe la Shirikisho. Lakini ikabainika timu hizo hazijakutana katika Kombe la Shirikisho.


TFF na Bodi ya Ligi, ndani ya siku 11 ambayo ni saa 264, wako ‘busy’ wanaitafuta kadi moja tu ya njano. Tayari kamati mbili zimekaa na kila zinapokutana wajumbe hulamba posho zao zinazokadiriwa kuwa Sh 400,000 kwa kila mmoja.


TFF na Bodi ya Ligi, wameshindwa kuuthibitishia umma kwamba ni kweli Fakhi ana kadi ya njano au la. Wamemuita hadi yeye kumuuliza, wamemuita aliyetoa kadi, aliyefanyiwa faulo na wengineo ambao isingekuwa na ulazima wowote wa kufanya hivyo kama wangekuwa ni watu makini.


Hii kadi ya njano ya Fakhi “inawavua nguo” TFF, inaonyesha kiasi gani mpira unaongozwa na watu wasiokuwa makini hata kidogo, vipi tutegemee mafanikio au maendeleo kama ambavyo tumekuwa tukiaminishwa?

MOHAMED FAKHI

Napenda nikukumbushe kila kamati unaona imekaa, inaitwa na TFF na TFF kupitia uongozi wa juu unaoongozwa na rais ambaye ni Malinzi ndiyo wanaoziteua.


Kamati hizi zinaitwa huru, lakini zinafungia na kutoza faini kwa faida ya TFF. Kwa kuwa ni kamati za TFF, ni rahisi kupata uhakika wa jambo kupitia kwa baba huyo wa mpira wa Tanzania.


TFF ni baba asiye na mipango, asiye na plani za baadaye za maendeleo ya familia yake kwa kuwa anaongozwa na watu wanaotamani kuendelea wao na si wanaopenda au wadau wa mpira kwa ajili ya maendeleo ya mpira kwa nchi.


Kama TFF imeshindwa kujua au kupata uhakika wa kadi tu ya njano ya mchezaji kwa siku 11 hadi jana, inaweza vipi kutuhakikishia kwamba itaeleta maendeleo katika nchi yetu.


Kitu kibaya zaidi, pamoja na kushindwa kuipata kadi hiyo, imekuwa ikiitafuta bila ya mafanikio. Jiulize baada ya kuhojiwa aliyefanyiwa faulo, aliyeitoa ambaye ni mwamuzi, aliyepigwa kadi, kamisaa, waamuzi wasaidizi, viongozi wa timu na kadhalika. Nani anatakiwa kuhojiwa baada ya hapo?
Je, kamati hiyo ya TFF inataka kuuhoji mpira uliochezewa? Au wanataka kuwahoji mashabiki waliokuwa katika mchezo huo au wanaitafuta kadi iliyotolewa ndiyo waihoji?


Kuendelea kushindwa kusema kadi ilikuwepo, Simba wachukue pointi tatu na mabao matatu au haikuwepo na haraka pointi zirudi kwa Kagera kwa nini inakuwa vigumu? TFF inataka kutengeneza majibu yake, inataka kulazimisha mambo au inataka kufanya jambo kwa faida ya nani?

Angalia suala la Haji Manara, limemuudhi Malinzi na TFF, amewasema, inawezekana amekosea kadhaa na amepatia mengi. Siku tatu tu, adhabu tena na faini ya Sh milioni 9. Hiki ni kichekesho kabisa! Fedha hiyo ni kukomoana, TFF haipaswi kukosolewa, haiwezi kuonya na vipi kadi haipatikani?

Kadi ya Fakhi ipo wapi? Kwa nini TFF haina rekodi? Wakusanya rekodi ambao ni waamuzi ni chini ya TFF na bodi ya ligi, wanaohifadhi rekodi za kadi na michezo yote ni wao, vipi haijulikani?

Serikali imechoka na mlolongo na ubabaishaji wa mambo, imekasirika na kuamua kutangaza kuhakikisha TFF inafanya mambo yake kwa weledi na kutaka kuona uamuzi unafanywa kwa kufuata haki, jambo ambalo nna hofu nalo kama kweli litafanyika.

Haki ni kuwaridhisha walio kwenye madaraka, ndiyo maana kadi haijulikani ilitoka au haikutoka. Hili ni jambo ambalo ndiyo picha halisi kwenu nyote ambao mmekuwa mkichagua watu kwa kuangalia sura au furaha na amani ya mioyo yenu na si maendeleo ya soka.

Unawezaje kunishawishi mimi kwamba kuna mabadiliko yanakuja kwa TFF hii inayoshindwa kujua kadi moja ya njano ilipo na kumaliza mjadala huu. Siku nyingine tutaiamini vipi TFF ikisema kuna kadi au haipo?

Mtihani tunaokwenda nao ni mkubwa, mgumu na lazima tukubali viongozi wa mikoa ndiyo mlioleta matatizo haya na inawezekana mtaendelea kutuletea tena kwa kuwa katika uchaguzi, mtaangalia furaha yenu.

Kadi ya njano ya Fakhi inatafutwa na kamati ya Katiba, Sheria na hadhi za Wachezaji. Lakini haijulikani ilipo hata ndani ya Bodi ya Ligi na TFF? Au ni kutaka kuendelea kuwavuruga tu wadau?

Mimi naamini TFF imefeli. Najua inajificha kwenye kivuli cha Serengeti Boys ambako ilikuta imetengenezwa mazingira na uongozi uliopita na ndiyo maana baada ya kumuondoa Kim Poulsen walifeli hadi walipomrudisha.

Ligi yetu duni, yenye kashfa rundo za kupanga matokeo, yenye uonevu na malalamiko rundo kuliko wakati mwingine wowote. Na sasa kadi ya njano imetafutwa bila mafanikio hadi serikali imeingia na ndiyo utasikia imepatikana!


SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic