April 10, 2017Mashabiki wa Simba, pamoja na baadhi ya viongozi wa timu hiyo wamempa tano beki wa kulia wa Yanga, Hassan Kessy kwa kazi kubwa aliyoifanya juzi uwanjani katika mchezo wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho Afirika dhidi ya MC Alger ya Algeria, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa, Kessy alionyesha kiwango cha juu hali iliyosababisha baadhi ya mashabiki wa Simba waliokuwa uwanjani hapo, kuanza kumshangilia kwa kumpigia makofi huku wakiwataka wenzao waliokuwa wakimponda kuachana na chuki zisizokuwa na tija.

Mashabiki wa Simba walikuwa wakibishana mara baada ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa, hali ambayo ilimfanya aliyekuwa katibu mkuu wa timu hiyo, Mwina Kaduguda kuwataka kuacha chuki binafsi.

“Nawapongeza sana mnaomuunga mkono Kessy kutokana na jinsi anavyoifanya kazi yake ipasavyo uwanjani kwani hivyo ndivyo mchezo wa soka unavyotaka na siyo kumponda kwa sababu tu mna chuki naye.


“Yanga inawakilisha Tanzania kimataifa na Kessy ni Mtanzania mwenzetu na alikuwa Simba, hivyo tumuunge mkono pale anapofanya vizuri, anapofanya vibaya tumshauri na siyo kumponda, hakika Wanasimba wote waliomuunga mkono nawapongeza sana, kwani huo ndio uzalendo,” alisema Kaduguda huku akiungwa mkono na baadhi ya mashabiki wa Simba waliokuwa wakimsapoti beki huyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV