April 5, 2017Mshambuliaji Donald Ngoma na kiungo Thabani Kamusoko juzi Jumatatu walifufua matumaini ya Yanga baada ya kuanza mazoezi mepesi.


Wazimbabwe hao, waliukosa mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC kutokana na majeraha ya goti yaliyowaweka nje ya uwanja akiwemo na Mrundi, Amissi Tambwe ambaye naye ameanza tayari.

Nyota hao, wamerejea uwanjani ikiwa ni siku chache kabla ya mchezo wa kwanza dhidi ya MC Alger ya nchini Algeria watakaovaana kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Daktari Mkuu wa timu hiyo, Edward Bavu, alisema wachezaji wake majeruhi wote wamepona na wameanza mazoezi isipokuwa mgonjwa mpya Mzambia, Justine Zulu aliyeumia katika mechi dhidi ya Azam FC.


Bavu alisema, Zulu yeye jana Jumanne asubuhi alitarajiwa kupeleka hospitali kwa ajili ya kusafishwa kidonda chake kabla ya kutolewa nyuzi na kuanza mazoezi mepesi.
"Ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga kusikia wachezaji wetu ambao ni muhimu kwenye timu wakirejea uwanjani katika mechi muhimu ambayo tunahitaji ushindi katika uwanja wetu wa nyumbani.

“Ngoma na Kamusoko wamepona majeraha yao na leo (juzi) jioni walianza mazoezi mepesi ya binafsi, baada ya kumaliza programu ya gym na matibabu yao."Niseme kuwa, wachezaji hao wapo chini ya uangalizi kwa siku hizi mbili kabla ya kuanza mazoezi magumu ya pamoja na wenzao katika kujiandaa na mechi na Alger,” alisema Bavu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV