April 7, 2017
Na Saleh Ally
KAULI za viongozi wengi wa klabu zimekuwa tatizo kubwa kabisa. Zinawaamisha mashabiki wao mambo yasiyokuwa sahihi kuhusiana na timu zao na nini kinafuata.


Mfano, baada ya Simba kuwa inaongoza kwa tofauti ya pointi nane katika mzunguko wa kwanza, maneno ya kusema “Simba tayari bingwa” ndiyo yalitawala hadi kwa viongozi.

Mwisho wake, hadi mzunguko wa kwanza unaisha, Simba ilikuwa inaongoza kwa pointi mbili tu baada ya kupoteza pointi sita katika mechi mbili mfululizo ikifungwa bao 1-0 dhidi ya Lyon jijini Dar es Salaam, ikapoteza 2-1 dhidi ya Prisons mjini Mbeya.

Mzunguko wa pili ulipoanza, Simba ikaanza kwa kusuasua Yanga ikapaa kileleni. Baadaye Simba ilijirekebisha na kufanikiwa kurudi na kuongoza kwa tofauti ya pointi mbili.


Ajabu, viongozi wakajisahau na kuanza kupiga kelele zilezile za “Simba bingwa”, wakati wakijua tofauti ni pointi mbili, ukipoteza moja mpinzani akashinda moja maana yake umeshuka.


Hii imetokea kwa Yanga kumshinda Azam FC mechi iliyoonekana ni ngumu sana kwake na Simba kufungwa na Kagera Sugar, huku ilionekana ni mechi rahisi kwake. Hapa inaonyesha Simba wanapaswa kujifunza tena.


Funzo hili kwa Simba litakuwa ni la mwisho msimu huu bila ya kujali matokeo ya mwisho yatakuwa vipi. Kwamba watakuwa mabingwa au la. Soka si mchezo wa mdomoni pekee, unataka vitendo na hesabu uwanjani.


Wachezaji wa Simba, wanachotakiwa ni kuamini wanaweza kubeba ubingwa. Hali kadhalika Yanga wafanye hivyo na mwisho iwe burudani hasa ambayo itainua thamani ya Ligi Kuu Bara.


Watanzania wanataka kuwa na ligi bora. Mechi 10 zilizobaki ndiyo zitakazoamua bingwa. Simba atacheza tano na Yanga tano.


Atakayezicheza vizuri mechi hizo kama karata, basi atafanikiwa. Kwa kuwa hata Yanga hawapaswi kupiga kelele ya ubingwa kwa sasa.


Hakuna mwenye nafasi ya kuamini au kuona tayari amekuwa bingwa. Yanga wanaweza kujifunza kwa Simba walioongoza kwa tofauti ya pointi nane na leo wako chini kwa pointi moja.

Hivyo wao kuongoza kwa tofauti ya pointi moja, hii pia haiwapi sababu ya kuwa wao ni mabingwa tayari. Wanatakiwa kufanya kazi hasa na kuonyesha kiwango bora ili kufikia malengo.

Sitaki kuingilia masuala ya mgomo wa wachezaji ambao umekuwa ukielezwa unataka kutokea Yanga. Wapenda soka wanataka kuona soka na hiki ndiyo kipindi cha kuona timu ipi ni bora.

Kama ilivyo, Yanga na Simba ndiyo wenye nafasi, Yanga na Simba ndiyo wakongwe zaidi. Basi mpira bora umsaidie apatikane bingwa sahihi ambaye kila mpenda soka bila ya kujali ushabiki ataona alistahili.

Viongozi wa klabu zote mbili wapunguze mihemko na mazungumzo yao yawe ya staha au kuangalia hali halisi.
Mazungumzo mengine yamekuwa yakiwatunisha vichwa wachezaji wao, nao kwa kuwa hawajitambui wanaishia kuwaangusha kwa kuwa maneno yanawafanya waamini wao ni nyota kupindukia.

Kipimo cha ubora ni mafanikio, mafanikio ya mwisho wa msimu kwa timu ni vikombe. Hivyo vizuri kila upande ukaonyesha unaweza kupata hayo mafanikio kwa ubora sahihi na si maneno mengi ambayo mwisho yanaishia kwenye hadithi ya “mkono mtupu…..”


Mechi 5 za Yanga
Yanga SC vs Kagera Sugar
Yanga SC vs Mbeya City
Yanga SC vs Toto Africans
Yanga SC vs Tanzania Prisons
Mbao FC vs Yanga SC
*Yanga ana mechi moja nje ya Dar

Mechi 5 za Simba
Mbao FC vs Simba SC
Toto Africans vs Simba
Simba SC vs Mwadui FC
Simba SC vs Stand United
Simb SC vs African Lyon
*Simba ana mechi mbili nje ya Dar

Msimamo:
                               POINTI
1. Yanga SC               56

2. Simba SC               55

1 COMMENTS:

  1. Inaonekana unakurupuka, unachukua maneno ya mashabiki na kuwawekea viongozi mdomoni!! Hii si sawa. Pia unachanganya mada, mambo ya mgomo yanahusikaje!?

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV