May 31, 2017


SINGIDA UNITED

Na Saleh Ally
TIMU tatu zimepanda daraja na msimu ujao zitacheza Ligi Kuu Bara huku kukiwa na hisia za kuwa, utakuwa ni msimu wenye ushindani kwelikweli.

Inaonekana ushindani utakuwa juu zaidi kwa kuwa kuna mambo mengi yamejitokeza msimu huu na hasa suala la ushindani kwa kuwa mambo yalikuwa magumu kwa kila timu.

Aliyekuwa anatakiwa kubeba ubingwa hakuwa na uhakika, pia hakukuwa na uhakika wa kubaki Ligi Kuu Bara kwa zaidi ya timu sita kwa mkupuo hadi mwisho wa ligi.

Pamoja na upungufu mwingi ambao ni madudu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huenda hili ni jambo zuri unapozungumzia kupanda kwa kiwango cha Ligi Kuu Bara.


Kama TFF itaboresha madudu au uongozi mpya utaingia madarakani na kuona makosa yaliyofanywa na wenzao na kuyarekebisha, basi ushindani unaweza kupanda zaidi na kuifanya ligi kuwa bora zaidi.

Timu tatu zilizopanda daraja ni Singida United ya Singida, Lipuli ya Iringa na Mji ya Njombe ambayo inaonekana kuwa ni wageni lakini wanajitegemea hasa.

Nasema wanajitegemea kwa kuwa, Singida na Lipuli si wageni Ligi Kuu Bara, wamerejea baada ya kupotea, muda mrefu uliopita.

LIPULI FC.

Lakini kibaya zaidi, wakati wanarejea Ligi Kuu Bara, wanaonekana tayari wao wana marafiki zao ambao waliwaacha kitambo na huenda kumekuwa na msisitizo kuhusiana na urafiki huo.

Urafiki wa Singida United na Yanga na urafiki wa Lipuli na Simba, hivyo utaona kuna dalili za mapenzi kwa wale wenye urafiki na kina fulani.

Mwendo unavyokwenda ni kama hivi; mashabiki wa Yanga tayari wameanza kuonyesha mapenzi na Singida United ambayo imeamua kutumia jezi za njano na nyeusi huku wale wa Lipuli ambao jezi zao ni rangi ya damu ya mzee, wanaonekana kuwa upande wa Simba.

Kila mara, Singida United wameweka msisitizo, kuwa wao si Yanga na wakikutana nao, wataona. Lipuli pia wamesisitiza kuwa wao si Simba wala hawana urafiki.

Lakini ndani ya klabu hizi mbili, wanaosaidia sana katika usajili na mambo mengine kwa upande wa Singida United ni Yanga, tunajua Mwigulu Nchemba alivyo bize na Singida United lakini anajulikana mapenzi yake na kazi zake na Yanga.

Kwa Lipuli, Zacharia Hans Poppe ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usajili na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba ni mmoja wa wanaosaidia kwa nguvu sana na hata hadi inapanda ligi kuu, alitoa msaada wake mkubwa.

Najua Singida na Lipuli wanaweza kujiongoza wakiamua lakini itafikia siku watatakiwa kulipa fadhila zinazowaumiza. Kumbuka kule Tanga, Coastal Union waliokuwa marafiki wa Simba na African Sports ndugu wa Yanga.

Urafiki wao haukuwahi kuwa na faida sana upande wa timu hizo za Tanga na badala yake ilionekana faida imejaa Dar es Salaam.

Kama haitoshi iangalie Toto African ya Mwanza. Ni maarufu kwa kupanda na kuteremka daraja bila ya kuchoka huku viongozi wakiwa na maneno mengi.

Ina rekodi ya kuchangiwa kuteremshwa daraja na Yanga kwa kuwa mara nyingi inakutana na Yanga ikiwa inapambana kubeba ubingwa na yenyewe inajitahidi kubaki Ligi Kuu Bara.

Lakini inajulikana kama “Toto la Yanga”. Mara zote viongozi wake wamekuwa wakisema hawana uhusiano na Yanga na wakikutana nao, “watakiona”. Lakini wao ndiyo wamekuwa wakidondoshwa.

Ndani ya urafiki huu wa timu za Ilala, Dar es Salaam na timu hizi za mikoani, kumekuwa kuna urafiki wa kinafiki au urafiki wa faida upande mmoja au faida ndogo mikoani na kubwa Dar es Salaam.

Mbona Leicester City siyo rafiki wa Arsenal au Hull City hawakuwa rafiki wa Liverpool? Huu urafiki una ulazima gani na inaonekana kabisa hawa mabwana wa mikoani wamekuwa hawana faida yoyote.

Maneno yanaonyesha hakuna jambo lolote linalowabana kutokana na urafiki. Lakini uhalisia unaonyesha kuna tatizo na hasa suala la ulipaji wa fadhila.

Kwa nini aliye Simba ndiye asaidie Lipuli na aliye Yanga asaidie Singida? Kwani hawa Singida au Lipuli hawana watu wao kabisa ambao watakuwa wao na wafanye mambo yao bila kuwahusisha hata kidogo wale wanaotokea klabu hizo kongwe?

Kuna haja ya kujifunza, kujitegemea bila miguu wala mikono ya Simba au Yanga ili kutengeneza timu imara na isiyokuwa na deni la fadhila ambalo limekuwa sumu kwa timu za mikoani.


1 COMMENTS:

  1. mbona wewe Simba kwani una timu ya ingine ya kuishabikia

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic