Awali kulikuwa na taarifa za madereva wa magari ya usafirishaji mafuta ya kampuni ya ZHP inayomilikuwa na Mwanasimba, Zacharia Hans Poppe kutekwa nchini DR Congo.
Hakukuwa na uhakika sana lakini sasa SALEHJEMBE imepata uhakika ni kweli madereva sita walitekwa na baadaye kuokolewa.
Hans Poppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, amezungumza na SALEHJEMBE kutoka nchini DR Congo na kuthibitisha hilo.
"Ni kweli, mimi nimesafiri kwa emergency kuja huku baada ya tatizo hilo na kweli imetokea.
"Walishambuliwa kwa risasi wakiwa njiani kuja huku Congo kuleta mafuta. Baadaye madereva sita walitekwa lakini tayari wamekombolewa, sasa wako salama," alisema Hans Poppe kutoka nchini humo.
Baadaye mawasiliano yalikatika lakini haijajulikana chanzo cha utekaji huo kama watekaji hao walitaka fedha.
Kuna picha zinaonyesha madereva hao wakionyesha baadhi ya majeraha baada ya kuteswa na watekaji hao.
Wakati mwingine, madereva wamekuwa wakitekwa ili watekaji wafaidike na fedha zao wanazopewa kwa ajili ya matumizi wanapokuwa safarini.
Barabara za DR Congo zimeelezwa kutokuwa salama sana.
0 COMMENTS:
Post a Comment