Na Saleh Ally
TUZO za Ligi Kuu Bara zimekamilika na kuonyesha kuna mabadiliko kupitia kamati ya tuzo ambayo mara nyingi imekuwa ikitengeneza malalamiko mengi sana.
Wachezaji, waamuzi na makocha walioshiriki Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika wiki iliyopita wameitwa na kutuzwa baada ya kujumuika pamoja.
Kawaida, malalamiko ni jambo la kawaida kunapokuwa na ushindani wa jambo lakini unaweza kupima usahihi wa unachokifanya kulingana na wingi wa malalamiko yenyewe.
Msimu wa 2016-17, inaonekana kabisa kwamba hakukuwa na malalamiko mengi kwa kuwa kamati ya tuzo chini ya Alhaji, Msafiri Mgoyi imeonekana kufanya kazi yake vizuri zaidi kiweledi.
Malalamiko yanapopungua, maana yake kunakuwa na umakini umeongezeka. Hii inaonyesha kamati imejifunza kutokana na makosa yaliyotokea huko nyuma kulingana na hali halisi.
Hili ni jambo jema la kusifia, lakini bado inaonekana kuna mambo madogo yamekuwa yakiendelea kila tuzo hizo zinapofanyika.
Mfano pale ukumbini, maandalizi yanaonekana kutoboreka katika kiwango ambacho kinaonekana vitu vimepiga hatua na hasa katika suala la uwasilishaji.
Kwa kuwa tuzo hizo zinaonyeshwa moja kwa moja na runinga, ni lazima kulenga ile hali kuwa ile ni shoo sahihi ambayo inapaswa kuonekana katika mpangilio bora kabisa.
Hakuna chenye ugumu kwa kuwa mambo mengi ni ya kawaida kabisa na kama ni suala la mabadiliko basi ni kidogo yanaweza kubadilishwa na kuwa mambo bora kabisa.
Mfano, anapoitwa mtu kwenda kukabidhi tuzo, anatajwa jina, anaanza kupanda pale juu akitokea sehemu waliyokaa watu. Baada ya hapo, aliyeshinda naye anapanda. Hili ni jambo la kizamani na lilishapitwa na wakati. Tunajua kuwa washindi na wanaotakiwa kukabidhi hutokea “back stage”. Wanafika pale mbele na baada ya kukabidhi na kupokea, wanarudi tena nyuma ya jukwaa.
Maana yake, wanapaswa kuandaliwa mapema na kuwa nyuma ya jukwaa. Akiitwa fulani kukabidhisha anatokea nyuma ya jukwaa. Baada ya hapo anayekwenda kukabidhiwa naye anafuatia.
Unapozungumzia zile picha za video za wachezaji mbalimbali zilipokuwa zinaonyeshwa, nyingi zinaonekana hazikuandaliwa vya kutosha na mfano mzuri ni ile ya beki wa Simba, Mohamed Hussein Zimbwe maarufu kama Tshabalala.
Ndiye mchezaji bora, lakini haikuwa imeandaliwa wala hakuwa ikionyesha hata mambo muhimu matatu aliyoyafanya uwanjani zaidi ya kona aliyopiga, hiki ni kichekesho.
Kuna suala la shukurani ambalo linaweza kurekodiwa kwa dakika moja. Mchezaji akafuatwa hata kwake na kuzungumza jambo ambalo watu walio ukumbini na wanaoangalia mubashara nao wakashuhudia vizuri.
Jiulize, Azam TV ndiyo wadhamini wa ligi kuu, wana wataalamu kibao wa kutengeneza mambo mazuri na picha za video wanazo kwa kuwa wameonyesha mechi nyingi mubashara. Sasa tatizo nini kila kitu kinazidi kuonekana hakina maandalizi bora wakati wa shoo kubwa kama hiyo.
Wachezaji wakongwe, utamuona mtangazaji katika hafla hiyo akijaribu kuwazungumzia. Si kwa kina kwa kuwa ana mambo mengi yanamwandama. Iko wapi shida kukiwa na picha fupi angalau dakika moja na nusu ikimzungumzia Kitwana Manara au Sunday Manara kwa msaada wake mwenyewe na watu wakatulia wakishuhudia kabla ya yeye mwenyewe hajatokea jukwaani.
Kweli kuna kujifunza na hilo ni jambo jema. Inaonekana tunapokwama ni sehemu ambayo haina hata ugumu wa kung’oka. Mazoea na kwa kuwa waandaaji huenda wanaona mambo yanakwenda, basi hawawezi kujali.
Kizuri ni gharama na hii haina maana ya gharama kwa fedha tu, unaweza kugharamia jambo kwa kutumia muda na akili yako na kufanya kitu bomba maradufu.
Ningependa kuchangia hivi, kwamba msimu ujao, basi kuna haja ya kufanya kitu kizuri zaidi ambacho pia kinatoa nafasi kubwa ya shukurani kwa wadhamini ili kuwashawishi na wajione wako katika mikono salama.
0 COMMENTS:
Post a Comment