June 2, 2017
Hii ni nyingine mpya kuwa, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo ni taasisi ya serikali, limezuia nyasi bandia za Klabu ya Simba zilizopo kwenye bandari ya Dar es Salaam.


Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu Simba wazilipie nyasi hizo bandia ambazo awali zilitangazwa kupigwa mnada na kampuni ya mnada ya Majembe Auction Mart iliyopewa tenda na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Simba ilitumia shilingi milioni 80 kuzikomboa nyasi hizo kwa kile kilichoelezwa kukaa bandarini kwa siku 60 na kusababisha kusimamisha ujenzi wa uwanja wao uliokuwepo Bunju jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Ujenzi wa Uwanja huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Zacharia Hans Poppe, ameiambia SALEHJEMBE kuwa hawataendelea na shughuli za ujenzi wa uwanja huo kwa sasa na amekata tamaa kwa kuwa anaona hawatendewi haki kabisa.

Hans Poppe alisema TBS ndiyo wamesababisha shughuli hizo kutokana na kudai kibali halali lakini wao wanacho cha nakala ‘photocopy’.

Hans Poppe alisema kwa mujibu wa wakala wa nyasi hizo, yeye tayari amethibitisha ubora wa nyasi na kuwapatia kibali cha kivuli ambacho wameonyesha kwa TBS lakini kikakataliwa na kuhitajika halisi ambacho wao hawana.

Aliongeza kuwa, TBS wameruhusu kuzitoa nyasi hizo bandia hadi watakapolipa shilingi milioni 37 kama hawatakuwa na kibali orijino.

“Mimi nimeona nisitishe hilo zoezi la ujenzi wa Uwanja wa Bunju kwa hivi sasa, kwani nimechoshwa na haya mambo.


“Kitu cha kushangaza wakati tunajiandaa kuzitoa bandarini tukapewa taarifa na TBS kuwa nyasi hizo zisitolewe hadi tutakapoonyesha kibali orijino cha ukaguzi kutoka tulipozinunua, kwa bahati mbaya hatukuwa nacho orijino tulikuwa na ‘copy’, wamegoma, wanataka tulipe shilingi milioni 37 ndiyo zitoke, hivyo tumeziacha,” alisema Hans Poppe.

Salehjembe


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV