June 2, 2017MAENDELEO YA TIMU ZA VIJANA
Ndugu zangu, leo nimewakaribisheni ili kwa niaba ya Shikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) niweze kutoa shukrani zetu, pongezi na pia kutoa mwelekeo wa timu zetu za vijana kuelekea Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 (FIFA WORLD CUP 2026).

SHUKRANI.
Kama tunavyofahamu timu yetu ya vijana umri chini ya miaka 17 ilishiriki kwa mara ya kwanza katika Fainali za Afrika (Afcon U17) nchini Gabon, fainali hizi  zilichezwa kuanzia tarehe 14-28 mwezi Mei mwaka huu.

Timu yetu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys ilishiriki katika fainali hizi na kutolewa hatua ya makundi. Katika hatua hii ilitoa sare ya 0-0 dhidi ya Mali, ikaifunga Angola bao 2-1 na kutolewa kwa sheria ya uwiano wa matokeo (head to head) baada ya kufungwa bao moja kwa bila na Niger.

Ni jambo la kutia moyo kuwa bingwa wa mashindano haya Mali timu pekee ambayo hawakuweza kuifunga ni Tanzania na timu nyingine zote walizokutana nazo walizifunga ikiwemo na Ghana ambayo Serengeti Boys walitokana nayo sare hapa Dar es salaam.

Hakika mashindano haya yameonyesha kuwa kumbe Tanzania tunao uwezo mkubwa wa kushindana katika mashindano makubwa.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linapenda kutoa shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu, Waziri  Mkuu Mh Kassim Majaliwa ambao kwa umoja wao walihakikisha timu inawezeshwa kikamilifu na kuwa na nguvu kubwa ya kushindana.

Tunamshukuru sana Mh Dk Harrison Mwakyembe Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na watumishi wa Wizara kwa ushirikiano na jitihada kubwa walizozifanya kuhakikisha timu inapata maandalizi mazuri.

Tunawapa hongera na kuwashukuru wachezaji wa Serengeti Boys kwa jitihada na ukomavu wao katika kipindi cha maandalizi na cha fainali zenyewe. Pongezi nyingi na shukrani kwa benchi la ufundi la timu na uongozi wa timu unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF Ndugu Ayoub Nyenzi, Kamati ya Utendaji ya TFF wakati wote ilikuwa karibu naye na ilimpa nguvu sana. Hongera pia kwa wafanyakazi wa TFF waliohakikisha wanaratibu shughuli za timu kwa ufanisi mkubwa.


TFF inawashukuru sana wajumbe wote wa Kamati ya Uhamasishaji ya Serengeti Boys iliyoongozwa na Bw Charles Hilary. Uhamishaji wao ulikuwa ni mkubwa sana na uliamsha ari ya Watanzania kuhamasika na kushangilia timu. Shukrani sana kwa wadau wote waliochangia timu na shukrani sana kwa waandishi wa habari na wasimamizi wa blogu mbalimbali na ma admin wa makundi mbalimbali ya mitandao waliohamasisha na kuichangia timu.

MPANGO WA BAADAYE WA SERENGETI BOYS.

Kikosi hiki cha Serengeti Boys kilichoshiriki fainali hizi sasa kimebadilika na kuwa rasmi timu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 20 NGORONGORO HEROES. Timu hii mwaka kesho itashiriki katika hatua hatua za kufuzu kucheza fainali za Afrika umri chini ya miaka 20 Afcon U20. Fainali hizi zitafanyika mwaka 2019. Benchi la ufundi la timu hii linaandaa program ya maandalizi ya kikosi hiki ambayo itahusisha kambi na mechi za majaribio ndani na nje ya nchi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV