June 3, 2017




Na Saleh Ally
FEDHA si kila kitu katika kila kitu, nataka uamini hivyo. Kwamba unaweza ukawa na fedha lakini ukakosa jambo fulani kwa kuwa fedha haina uwezo wa kukupa kila unachotaka!

Mfano wangu mzuri nitaupeleka katika soka kidogo nikianza na Tanzania. Kwamba Azam FC wana fedha nyingi kuliko Kagera Sugar lakini katika ligi, timu hiyo ya Kagera imekuwa ya tatu wao wa nne.

Hata Simba, Yanga na wao bado wao wana fedha nyingi zaidi na huenda walistahili kuwa mabingwa kila msimu!



Katika maisha, fedha ni chagizo, kinachofuata ni akili na moyo na hii inatokea hata Ulaya.

FC Barcelona ndiyo klabu inayolipa mishahara mikubwa zaidi kwa msimu lakini hadi msimu unaisha imeambulia Kombe la Mfalme pekee!

Madrid ambayo inashika nafasi ya nne, imechukua La Liga na leo inacheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Juventus inayoshika nafasi ya 10 kwa mishahara mikubwa.

Moyo ninaouzungumzia ni nia ya kutaka kutimiza ndoto na kutaka kufanya vizuri katika mambo ambayo unashiriki, kuongoza au kuyasimamia.

Ubongo ni akili ya utekelezaji ambayo inajumuisha ubunifu wa mambo ili yaende na kupata majibu sahihi.

Kama ni fedha pekee, halafu hauna moyo na ubongo sahihi, basi utaishia kupata kidogo au kukosa kabisa na mwisho hautaiona faida ya hizo fedha.


1.Barcelona    mil 279
Msimu huu wanajipoza na Copa de Rey pekee. Kwingine mambo si kama walivyotarajia. Angalia Ligi ya Mabingwa Ulaya na La Liga. Unaona kwa msimu wanaongoza kutoa mishahara mikubwa na bado hawapati kila kitu. Hapa ndiyo unaanzia kujifunza.


2. Man United    mil 265
Wana mafanikio makubwa zaidi kipindi hiki lakini utaona fedha ilivyowainua lakini mwisho haikuwapa kila walichotaka kama nafasi nne za Premier League.

Wamebeba makombe mawili Europa na EFL, ‘yes’ ni fedha japo hawajaingia katika Top Four, kupata Kombe la FA, maana yake fedha si kila kitu.

3.Chelsea  mil   256
Wamechukua ubingwa wa England, wameshindwa kubeba Kombe la FA. Fedha imechangia mazuri lakini bado haijawapa kila walichotaka.

4.Real Madrid   mil   250
Unaweza kuona mambo tofauti, wako fainali ya ligi ya mabingwa, wamechukua La Liga, wanazidiwa mishahara na Barcelona, Man United na Chelsea. Hivyo hauwezi kusema mafanikio ya Madrid ni fedha pekee.

5. Man City    mil 248
Baada ya kutua Pep Guardiola pamoja na fedha za kutosha, ikaonekana ubingwa wa Ulaya ni uhakika. Sasa hata nafasi ya tatu ni shida kwao na unaona, wanakosa nini? Fedha ndiyo wanazo za kutosha!





6.PSG     mil  239
Hawa wanatesa wanavyotaka kule Ufaransa, lakini mwisho fedha zao haziwapi kila wanachotaka na mfano mzuri Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ni kati ya wanaoishia njiani licha ya kumwaga fedha nyingi za mishahara.

7. Arsenal  mil 234
Wako wanaolalamika Kocha Arsene Wenger ni mbahili, lakini Arsenal wamemwaga pauni milioni 234 katika mishahara kwa msimu, si kitu kidogo.

Huenda walistahili ubingwa, nafasi ya pili au ya tatu kama ingekuwa fedha pekee ndiyo kila kitu. Soka linaonyesha, hapana fedha si kila kitu.

8.Bayern   mil 225
Wamechukua Bundesliga kama kawaida yao, wametolewa ligi ya mabingwa. Kama ni fedha tu, basi wangechukua nafasi ya Juventus. Inaonyesha baada ya fedha, kuna mengi ya kufanya.

9. Liverpool    mil 200
Kitita cha pauni milioni 200 si kidogo, hawana hata ubingwa mmoja. Sasa wanasherehekea kuingia nne bora jambo ambalo si mategemeo.

Hata hivyo, kufikia hapo imeonekana juhudi kubwa za Kocha Jurgen Klopp na wachezaji ambao mwisho walishindwa kwenda na mwendo wao.

10. Juventus     mil 181
Ndiyo mabingwa wa Serie A, Copa Italia pia wako fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na wana nafasi ya kuwa mabingwa.


Kama Ingekuwa fedha ni kila kitu, basi Arsenal, Man City au Barcelona ndiyo walistahili kuingia fainali na ikiwezekana kuwa mabingwa wa nchi zao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic