June 3, 2017



Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesikia taarifa za yeye kusaini Simba na kusema: “Simba, thubutu mnajidanganya nyie, mimi bado mchezaji wa Yanga!”


Kauli hiyo ya Niyonzima imekuja siku moja baada ya taarifa kuzagaa kuwa, kiungo huyo mwenye mbwembwe nyingi ndani ya uwanja, amesaini mkataba wa miaka miwili Simba.

Niyonzima sasa ni mchezaji huru anayeruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine yoyote itakayomhitaji kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kwani mkataba wake unaisha mwezi ujao.

Akizungumza kutoka Rwanda, Niyonzima ambaye yupo katika kambi ya timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, alisema hajasaini wala kufanya mazungumzo yoyote na Simba.

Niyonzima alisema: “Ni ngumu kuchukua maamuzi hayo mimi binafsi bila ya kuishirikisha Yanga kwani kanuni zinanibana.”

Kiungo huyo alisema, kama kuna klabu inamhitaji hivi sasa, ni vizuri ikafuata kanuni za usajili kwa kuifuata Yanga ambao ndiyo waajiri wake kwa ajili ya mazungumo kabla ya kumfuata yeye.

“Nikuhakikishie tu wallah! Sijazungumza na kiongozi yeyote wa Simba kwa ajili ya kusaini na hizo zinazoendelea ni tetesi tu pekee ambazo hazina ukweli wowote.

“Timu niliyofanya nayo mazungumzo ni Yanga na tumefikia makubaliano mazuri ya mimi kuongeza mkataba mwingine wa kuendelea kubaki Jangwani.

“Kwanza ninashindwa kuelewa ni nani anayesambaza hizo taarifa, kwa sababu ni ngumu mimi kusaini mkataba Simba nikiwa bado nina mkataba wa mwezi mmoja Yanga.

“Niseme tu kuwa klabu inayonihitaji ni lazima ifuate kanuni za usajili kwa kuwafuata viongozi wangu wa Yanga kwanza kuzungumza nao, halafu ndiyo waje kwangu kwa baraka za uongozi.

“Niwatoe hofu viongozi na mashabiki wangu wa Yanga kuwa, mimi bado ni mchezaji wao na kwa sasa nipo nyumbani Rwanda nikiwa kwenye majukumu ya timu yangu ya taifa,” alisema Niyonzima.

Juzi Alhamisi, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, akizungumza katika Kipindi cha Spoti Hausi cha Global TV Online, alisema anafurahishwa na uchezaji wa Niyonzima, Donald Ngoma na Obrey Chirwa wote wa Yanga.

“Ngoma, Chirwa na Niyonzima wote wana nafasi ya kucheza Simba, mimi binafsi ningependa hawa wacheze Simba kama inawezekana,” alisema Hans Poppe.


Niyonzima ni mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara wa 2016/17.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic