June 9, 2017Na Saleh Ally
HADI sasa Yanga ndiyo mabingwa wa Ligi Kuu Bara, maana yake wao ndiyo wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kumekuwa na hofu kidogo kuhusiana na kama kweli Yanga watawakilisha au la kwa kuwa watani wao Simba, wamekata rufaa kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), wakipinga Kagera Sugar kurejeshewa pointi tatu kama ilivyofanya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.

Hofu hiyo inawezekana ipo au haipo lakini kwa Yanga wanachopaswa kufanya ni maandalizi ya ambacho wameshinda mapema.

Kama Simba watapewa pointi tatu basi watakuwa na nafasi ya kuchukua nafasi ya Yanga na isipokuwa hivyo, basi Yanga wataendelea kuwa wawakilishi wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Maana yake wanachotakiwa kufanya sasa Yanga ni kuendelea na maandalizi ili kupata uhakika kwa kuwa kama hawatajiandaa halafu Simba wasishinde rufaa yao basi watakuwa katika wakati mgumu.

Yanga wanastahili kufanya chochote ambacho ni bora kwani hata kama watakosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, basi watakuwa wameimarisha kikosi chao.

Wakati wakifanya usajili, jambo kubwa hasa ambalo wanatakiwa kuliangalia ni kufanya mambo kisayansi.

Kinachoonekana wakati wa usajili Yanga wanakuwa ni kama watu walioshitukizwa au kuna jambo fulani hawakuwa wamejiandaa.
Nasema hivyo kwa kuwa kawaida kumekuwa na kamati ya ufundi ambayo inafanya usajili, lakini kwa sasa hali ilivyo ni kama vile hakuna mfumo huo na anayefanya usajili hajulikani.
Mbaya zaidi, inaonekana kuwa kifedha ni kama Yanga hawakuwa wamejipanga hasa baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji.

Umesikia kwa sasa taarifa kadhaa baadhi ya viongozi wa zamani wa Yanga wakisema hawahusiki kama ambavyo imekuwa ikielezwa kuwa wako katika usajili.

Hii inatokana na kwamba, hakuna mpangilio mzuri ndani ya klabu hiyo na hakukuwa na maandalizi au watu sahihi wanaohusika na usajili hawajulikani ni kina nani.

Nasisitiza Yanga kujipanga kwa kuwa pia kuna uwezekano mambo yakarejea kuwa yale ya kimtaani kama ilivyokuwa pale awali.
Kabla ya ujio ya Manji katika klabu hiyo, mambo yalikuwa yakienda katika mpangilio ambao haukuwa sawasawa.
Baada ya kuingia, ilionekana vitu vikipelekwa katika mpangilio uliokuwa sahihi na wahusika waliokuwa wakifanya kazi ya usajili walikuwa wakijulikana ni watu fulani baada ya ripoti ya kocha kutolewa.
Mfumo wa usajili wa klabu zetu umekuwa si ule ambao unakwenda kwa mpangilio bora na hii inatokana na watu kadhaa kuwa na maslahi yao ndani ya usajili unapokuwa unafanyika.
Wanaokuwa na manufaa, ni wale wanaofaidika na usajili huo kwa maana ya kuingiza kiasi cha fedha baada ya mchezaji aliyesajili kulipwa.
Hawa hufanya mambo yawe magumu kwa mchezaji mwenye uwezo halafu akawa na msimamo na wana uwezo wa kumfanya mchezaji mwenye kiwango cha kawaida kuonekana ni mzuri zaidi na usajili wake ukawezekana.

Mwisho faida inakuwa kwa maslahi ya watu na si maslahi ya klabu. Hii itachangia kuidhoofisha Yanga na mara nyingine hutengeneza uadui kati ya watendaji na wachezaji.

Kama utatengenezwa uadui mwanzoni, basi hata mwendelezo wa maisha ya wachezaji na watendaji baadaye hayatakuwa yale mazuri yanayoweza kufanya kuwe na amani wakati wa mapambano.

Kumbuka usajili ni awali tu lakini baada ya hapo ni mapambano ya msimu mzima yanayotaka ushirikiano, ukaribu na umoja wa hali ya juu.


Pia Yanga wakumbuke, usajili bora ambao wao wanahitaji marekebisho kwa umakini ndiyo dira ya mwendo wao wa baadaye. Wakiboronga mwanzo basi huko mbele, watatembea kwa kubahatisha.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV