Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amesema kwa maandalizi waliyofanya wana uhakika wa kuifunga Lesotho, hivyo amewataka mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kuwashangilia.
Taifa Stars baada ya kukaa kambini Misri kwa wiki moja, leo Jumamosi saa 2:00 usiku inacheza na Lesotho mechi ya Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2019 kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Kabla ya mchezo huo, Taifa Stars chini ya Kocha Salum Mayanga huko nyuma ilicheza mbili za kirafiki na kushinda dhidi ya Botswana na Burundi.
Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji, amesema wanauchukulia ‘siriazi’ mchezo huo na kikubwa kwao ni kushinda ili kujiwekea nafasi nzuri ya kufuzu.
“Hii ni mechi muhimu kwetu, tunaichukulia kwa umakini mkubwa na nia yetu ni kupata ushindi ambao naamini utatuweka katika nafasi nzuri ya kufuzu.
“Hatuwezi kuwadharau wapinzani wetu kwa kuwa nao wamejiandaa kwa ajili ya kupambana na sisi, nawaomba Watanzania waje kutuunga mkono ili tuweze kufikia malengo yetu,” alisema Samatta.
Kocha wa Taifa Stars, Mayanga yeye alisema; “Tumejiandaa kushinda na kwa bahari nzuri tumefanya mazoezi kwenye uwanja wa nyasi bandia na nyasi za asili, hivyo tutafanya vizuri.”
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Lesotho, Moses Malieh, alisema; “Hatukuja kutafuta sare, tumekuja kupata ushindi na hatutajali wenzetu wanachezaje.”
Kwa upande wake, nahodha wa Lesotho, Bokang Mothoana alisema: “Tumekuja kuiwakilisha nchi yetu na malengo yetu ni kupata ushindi kwa sababu tutacheza kwa kushambulia ili kufikia malengo tuliyojiwekea ingawa tunawaheshimu wapinzani wetu.”
Taifa Stars itawakosa nyota wake wawili ambao ni majeruhi, Jonas Mkude na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
0 COMMENTS:
Post a Comment