June 2, 2017

Na Saleh Ally
TANZANIA imepata ugeni wa wadau wa soka ambao inawezekana kila kiongozi au mchezaji angependa kujifunza kupitia kwao.


Hao ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Everton ya England, Robert Elstone pamoja na mchezaji gwiji wa klabu hiyo, Leon Osman, mmoja wa viungo waliocheza mechi nyingi zaidi wakiwa na Everton.


Osman amecheza mechi 400 akiwa na kikosi cha Everton na yeye pamoja na bosi wake, walikuwa Tanzania kwa siku mbili katika mkutano wao na uongozi wa SportPesa Tanzania.

SportPesa sasa ndiyo wadhamini wakuu wa Everton ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya saba nyuma ya Manchester United na Elstone anaamini wanaweza kujipanga zaidi.

Everton itakuwa nchini Julai 13, kucheza na bingwa wa SportPesa Super Cup ambaye atapatikana baada ya michuano itakayoshirikisha timu za Kenya na Tanzania.Mahojiano maalum kupitia SALEHJEMBE pamoja na Elstone, baada ya hapo alifuatia Osman ambaye alizungumzia mambo kadhaa ikiwemo kuhusiana na wachezaji Waafrika anaowakubali zaidi.


Swali: Baada ya kutua Tanzania umeona mambo kadhaa, nini umejifunza?
Elstone: Kwanza ni tabasamu, watu wenye mapenzi na furaha, lakini wameonyesha wengi wanapenda soka hasa.


Swali: Kuna mjadala kuhusu Everton kusafiri hadi Afrika na hasa Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, watu wanaona kama mmekosea?
Elstone: Sisi tunachukulia kama ni utambulisho wa Everton kwa Afrika Mashariki na Tanzania, kupata mashabiki wapya na kuwaeleza wadau tunafanya nini. Pia tuna nafasi ya kujifunza na ndiyo maana wanaweza kutoa maoni lakini sisi tunaweza kujifunza zaidi.Swali: Kitakuwa ni kikosi kizima cha kwanza?
Elstone: Kocha Koeman ataleta kikosi kizima na tunaamini itakuwa ni furaha kujumuika pamoja.

Swali: Mtacheza na bingwa wa SpotPesa Super, mnaona mambo yatakuwa laini?
Elstone: Hatuamini hivyo, tunaona ni nafasi nzuri kwetu kupambana. Tunaamini kutakuwa na ushindani pia ni jambo zuri kwa SportPesa walioamua kuandaa mashindano kumpata bingwa.

Swali: Baada ya mechi, mtamalizia kambi yenu ya maandalizi hapa Tanzania, au mtaondoka?
Elstone: Hapana tutaondoka kurudi nyumbani, tunakwenda kwenye upande wa pili wa maandalizi. Kumbuka tunajiandaa na sehemu ya mtoano kuwania kucheza Europa League. Pia tuna mchezo dhidi ya Sevilla. Kila siku kwetu ni muhimu na lazima tuitumie vizuri.Swali: Everton inaonekana nafasi yenu ni ya sita, saba. Vipi mnafanya nini siku moja tuone mkiwa mabingwa au angalau namba mbili?
Elstone: Tunapambana sana kufanya vizuri, kila mtu anapambana na lengo ni kubadili mambo. Angalia kuna mwekezaji mpya, anaonekana amepania kufanya vema. Sasa angalia ishu ya uwanja mpya imeanza lakini bado lengo ni kuifanya Everton izidi kuwa bora na bora zaidi.
Tunaendeleza vijana, tuna akademi bora kabisa ambayo tunaamini baadaye ni ukombozi.

Swali: Wewe ni mhasibu kitaaluma, umeona chochote kama biashara mara baada ya kufika hapa?
Elstone: Ninaamini kwa kuungana na SportPesa tutafanya kazi ya kuitambulisha Everton kwa watu wa Tanzania na Afrika Mashariki. Tutazidi kuongeza nguvu kundi la wanachama kupitia hapa. Watu wataijua zaidi klabu yetu, nasi tutajifunza zaidi kuhusiana na ukanda huu na hii ni njia nzuri ya biashara.

Baada ya Elstone, ilikuwa zamu ya Osman, gwiji huyu wa Everton aliyewahi kucheza timu ya taifa ya England na mmoja wa wachezaji wenye heshima kubwa katika klabu hiyo.

Hata hivyo, wenyeji wao waliendelea kushikilia msimamo wa kutowauliza maswali yoyote ya usajili kwa kuwa wasingejibu kama lile la Wayne Rooney kurejea, Lukaku kuondoka au wamepanga kumuacha na kumsajili nani wakitaka zaidi iwe kuhusiana na ziara yao, haikuwa na ujanja.

Osman sasa ana miaka 36 na alistaafu kuichezea Everton msimu uliopita akiwa mmoja wa manahodha. Alifunga mabao 43 akiwa na Everton.

Swali: Mechi 400 katika Premier League si jambo dogo, uliwezaje?
Osman: Siwezi kusema ninajua sana, lakini ni hamu ya mafanikio. Nilitaka kufanya zaidi na zaidi. Nilitaka mechi moja, baadaye nikataka tano na mwisho nikataka kufikisha 400. Kwa kifupi nilitaka mafanikio zaidi.

Swali: Unaweza kutuambia wachezaji bora kutoka Afrika uliocheza kwenye timu yako au Ligi Kuu England?
Osman: Wako wengi lakini Samuel Eto’o na Didier Drogba. Nilicheza na Eto’o, alinipa pasi na kufunga bao langu bora zaidi la Everton. Nitawaeleza baadaye wanangu kuhusiana na hilo.Swali: Vipi kuhusu Steven Pienaar wa Afrika Kusini?
Osman: Mmoja wa wachezaji bora niliowahi kucheza nao. Pienaar alikuwa na kipaji hasa na uwezo wake ulikuwa juu hadi unashangaza.

Swali: Nini unakikumbuka kwake?
Osman: Uwezo uwanjani lakini mtu mwema nje ya uwanja. Nafurahi leo nipo Tanzania si mbali sana kutoka Afrika Kusini kwao Steven (Pienaar).Swali: Hauna umbo kubwa sana, lakini ulikuwa matata na mwenye mafanikio. Vipi uliweza kufanikiwa?
Osman: Ahsante kwa kung’amua kuwa sina umbo kubwa (kicheko). Ni kweli, muda wote naocheza nao walikuwa na maumbo makubwa na niliwaangalia namna hii (anaangalia juu kutoa mfano).

Lakini kawaida ukishindwa njia hii, unatumia nyingine. Nilijaribu kutumia wepesi wangu au kuusoma mchezo haraka kuliko wengine. Nilichotaka ni kufanya vema zaidi ya wapinzani wangu, ndiyo maana nilifika huku kwa kuwa nilitaka kushinda.Mahojiano hayo hayakuwa marefu kwa kuwa walitakiwa kuondoka kuwahi ndege kwa kuwa wanarejea England.

Everton imewahi kubeba makombe tisa ya Ligi Kuu England, matano ya Kombe la FA pia ubingwa wa Ulaya mara moja lakini imekuwa ikipata shida kubeba ubingwa tena. Mara ya mwisho ubingwa England ilikuwa msimu wa 1986-87.


Everton imecheza jumla ya misimu 114 katika ligi ikiwa ni mingi zaidi ya klabu yoyote ile na imecheza misimu 63 mfululizo bila ya kuteremka daraja ligi kuu. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV