June 1, 2017

MKUDE AKIMUAGA SHOSE.


Mashabiki, wanachama na viongozi wa Simba wameungana kuuaga mwili wa shabiki Shose Mshaluwa Fidelis aliyefariki katika ajali ya gari alilokuwemo nahodha wa Simba, Jonas Mkude.

Lakini mashabiki wa timu nyingine, wakiwemo wa Yanga wameonyesha upendo kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki shughuli za kuaga mwili wa Shose.

Uongozi wa klabu ya Simba kwa kushirikiana na baadhi ya mashabiki wake, umetoa Sh milioni 4.2 kama sehemu ya rambirambi ya binti huyo aliyezaliwa mwezi Mei na kufariki Mei.

Shose alifariki akiwa njiani kurudi Dar es Salaam akitokea Dodoma ambako alikwenda kuisapoti Simba iliyoshinda kwa mabao 2-1 dhidi Mbao FC na kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho.

Wakati wa kumuaga marehemu Shose katika Kanisa Katoliki Magomeni jijini Dar, leo Alhamisi, Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu, alisema ni pigo kubwa kwao kuondokewa na shabiki wao huyo ambaye alikuwa akijitahidi kuambatana na timu hiyo popote ilipokwenda.

“Marehemu alikuwa mtu wa michezo, hivyo kuondoka kwake ni pigo kwetu na kwa wanamichezo wote kwa jumla, hii ni mipango ya Mungu,” alisema Kaburu.

Naye Rais wa Simba, Evans Aveva, amesema: “Familia ya soka, wadau na Simba imepata pigo kutokana na kifo cha Shose, sisi kama Simba tumempoteza mtu shupavu ambaye alikuwa akifanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya klabu.”

Marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho Ijumaa mkoani Kilimanjaro.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV