July 14, 2017Na Saleh Ally
UONGOZI wa Klabu ya Everton uliamua kushusha kikosi chake kizima kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, mechi iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo imepigwa kwenye uwanja wetu wa Taifa ukishirikisha timu mbili zote kutoka ugenini kwa kuwa Yanga, Simba, Jang’ombe Boys na Singida United zilishindwa kubeba ubingwa wa SportPesa Super Cup.

Baada ya hapo hakukuwa na ujanja zaidi, kwani tayari ilishaelezwa kuwa bingwa wa SportPesa Super Cup angecheza mechi dhidi ya Everton FC ambayo kweli imekuja.

Limekuwa jambo zuri kabisa kwamba Everton FC wametua nchini wakiwa na mchezaji nyota zaidi England kwa kipindi hiki, huyu ni Wayne Rooney.

Rooney amejiunga na Everton kwa mara nyingine akitokea Man United ambayo alijiunga nayo akitokea Everton FC akiwa kinda wa miaka 18 tu.

Kuwepo kwa Rooney katika kikosi cha Everton imeongeza mvuto wa hali ya juu na kufanya kila mmoja anatamani kwenda uwanjani au kupata nafasi ya kuwaona wachezaji wa Everton.

Kitu kizuri zaidi, Everton licha ya kwamba wako katika maandalizi ya msimu mpya. Walipanga ratiba nzuri na iliyokuwa rafiki kwa mazingira ya Tanzania ukilinganisha na timu kadhaa ambazo zisingekubali kufanya hivyo.

Wachezaji wa Everton walitumia wasaa wao mdogo kuitimiza ratiba hiyo ikiwa ni sehemu ya kutaka kuonyesha wao ni rafiki na Tanzania.

Angalia walifika kuwatembelea Albino, walifika kuwatembelea watoto wenye matatizo mbalimbali kama kutosikia, kutoona na kadhalika katika Shule ya Msingi Uhuru jijini Dar es Salaam.

Wachezaji hao walionekana kweli wamesafiri umbali mrefu sana kutoka Liverpool nchini England hadi Dar es Salaam, lakini walipofika moja kwa moja walianza safari ya kutembelea vituo na kuwaona watoto hao.

Saa kadhaa kabla ya mechi, wachezaji wengine wakiongozwa na Rooney walipata muda wa kuzungumza na Wamaasai na kujua historia ya kabisa hilo sehemu ya nembo ya taifa letu. Wakapiga picha wakiwakabidhi jezi, jambo ambalo pia lilionyesha upendo.

Hakuna asiyejua Everton ni timu kongwe na maarufu katika Ligi Kuu England ‘Premier League’ na duniani kote. Huenda tungetamani kuwa na wachezaji wa Tanzania wanaocheza katika kiwango hicho kama ilivyo kwa Yannick Bolasie kutoka DR Congo na uliona Wacongo walivyokwenda kwa wingi uwanja wa ndege kuwapokea.

Kawaida tumekuwa tukisubiri hadithi watu wakosee na baada ya hapo kuanza kulaumu lakini vizuri wakati mwingine kusifia angalau kwa mazuri yanayofanyika na ikipatikana nafasi ya kukosoa basi tunafanya hivyo.

Wenyeji wao SportPesa, ambao ni wadhamini wakuu wa timu hiyo. Hakika wanastahili pongezi kwa ziara hiyo na kama mwanzo nilivyowahi kuandika makala kwamba tunaweza kujifunza mengi kupitia wachezaji hao, ninaamini tutakuwa tumejifunza.

Suala la kucheza kwa Everton, lilionekana ni dogo sana. Ushiriki wao mkubwa kwa mambo ya jamii ulikuwa juu. Jambo ambalo ningependa kuona siku nyingine, Yanga, Simba na timu nyingine zinafanya tena na tena hata kama ziliwahi kufanya hivyo.

Angalia namna mambo yalivyokwenda kwa mpangilio na namna wachezaji wanavyoheshimu maofisa wa klabu zao bila kujali wao ni nyota.

Kuna haja ya kujifunza mambo kupitia wageni hao na pale tunaona walikosea, basi tujifunze kutofanya kama wao.

Ikitokea mtu akasema hatukujifunza, basi mimi nitashangazwa sana na kuona huenda ana jambo jingine. Kama itakuwa ni kusema kwa kurekebisha mambo, katika jambo zuri pia si mbaya lakini msisitizo wangu, ujio wa Everton ulikuwa na funzo kubwa.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV