July 29, 2017Kiungo mkabaji wa Mbabane Swallows ya Swaziland, Papy Kabamba Tshishimbi, jana asubuhi aliondoka nchini kurudi kwao DR Congo, lakini ameiachia mzigo mzito Yanga iliyofikia makubaliano naye ya kumsajili.

Hali hiyo, imekuja ikiwa ni siku chache tangu kiungo huyo atue nchini na kufanya mazungumzo na Yanga kwa ajili ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja waliokubaliana naye.

Tshishimbi raia wa DR Congo, tayari amefanyiwa vipimo vya afya na Yanga ambavyo vimeonyesha amefuzu, hivyo yupo kamili kwa ajili ya kuichezea timu hiyo bingwa wa Ligi Kuu Bara.

Taarifa za kuaminika kutoka Yanga zinaeleza, kiungo huyo amemalizana kila kitu na klabu hiyo lakini kilichobaki ni Yanga kumalizana na Mbabane kwani Tshishimbi bado ana mkataba nao wa miezi minne.

Imeelezwa kuwa, kiungo atarejea nchini kujiunga na Yanga mara baada ya pande hizo mbili kumalizana katika mkataba wake wa miezi minne aliyoibakisha Mbabane.

Yanga imedai makubaliano na Mbabane yatafikiwa muafaka hivi karibuni kutokana na klabu hiyo ya Swaziland kuonyesha nia ya kumuachia Tshishimbi baada ya kumruhusu aje nchini kufanya mazungumzo na Wanajangwani.

“Kila kitu kimekamilika kwa Tshishimbi kwa maana ya dau la usajili, mshahara na mahitaji mengine anayoyataka tumekubaliana naye, alikuja kwa ajili ya kazi hiyo pekee ambayo tayari tumekamilisha.

“Alikuja kwa ruhusa ya viongozi wake na sisi baada ya mazungumzo akaondoka kwenda kwao, kazi iliyobaki ni sisi kuzungumza na Mbabane ili tumalizane nao.

“Ninaamini tutafikia makubaliano mazuri na timu hiyo ambayo imeonyesha nia ya kumuachia Tshishimbi kuja kuichezea Yanga, kwani mkataba wake umebakia miezi minne pekee, tunataka kuvunja mkataba wake,” alisema bosi mmoja wa Yanga.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV