July 26, 2017



Na Saleh Ally
NILIWASIKIA mashabiki mbalimbali wa soka kutoka Zanzibar wakilalamika kwenye vyombo vya habari kwamba Shirikisho la Soka Afrika (Caf), halikuwatendea haki kuwavua uanachama wa shirikisho hilo ikiwa ni miezi mitatu tokea liwavishe uanachama huo.

Suala hilo linaonekana kuwakwaza wapenda soka wengi wa Zanzibar wakiwemo baadhi ya viongozi na mfano mzuri ni kutoweka kwa bendera ya Caf katika ofisi za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na kila aliyeulizwa akasema hajui ilipopotelea.

Juzi jioni nikasikia chombo kimoja cha habari kikimnukuu Makamu wa Rais wa Zanzibar, ambaye alikuwa kipa wa Ujamaa ya Zanzibar, Balozi Seif Iddi akisema hawajapokea taarifa hiyo ya kuvuliwa uanachama na wanasubiri watakapoipata, wataifanyia kazi. Ila hawakubaliani na suala hilo hata kidogo kwa kuwa Zanzibar ina masuala yake inayojiendesha licha ya kuwa katika muungano wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Tokea Caf ilipoipa uanachama Zanzibar nimekuwa nikishangazwa na hili jambo. Mara kadhaa nimefuatilia kwa baadhi ya rafiki zangu mjini Cairo, Misri, nao walionekana kutoelewa kitu na wengi akiwemo mmoja wa wanasheria wao alishindwa kunijibu sahihi baada ya kusema hata wao limekuwa likiwachanganya.

Mmoja aliniambia ulikuwa ni ushawishi wa Rais wa Caf, Issa Hayatou aliyeshindwa uchaguzi. Aliamini Zanzibar ingekuwa ni sehemu ya kura yake hapo mbele kwa kuwa alikuwa na uhakika wa ushindi. Lakini alifanya hivyo akijua ni makosa.

Huenda hata viongozi wengi wameshindwa kulichanganua hili na huenda wamekuwa wakilalamika tu juujuu. Naamini wanaweza wakawa hawajui au ni ile hali ya kawaida ya ubinadamu kupenda kulalamika tu.

 Wako wanasema wameonewa, lakini sheria na kanuni za Caf ziko wazi kuhusiana na nani anayepaswa kupata uanachama wa shirikisho hilo. Caf waliikubalia Zanzibar wakiwa wamekiuka kanuni hizo, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), lenyewe likakataa na ndiyo limekuwa chanzo cha kuiamsha Caf kubadili uamuzi kwa kurudi na kuziangalia sheria na kanuni zake.

Ungeweza kutolea mfano wa Uingereza au Great Britain, utaona nchi kama England, Wales, Scotland, Ireland ambazo ni nchi zinazojitegemea kila kitu na hata katika uanachama wa Fifa na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), zinatambulika kama nchi kamili ndani ya umoja wa United Kingdom (UK).

Katika umoja huu wa UK, kila nchi ina jina lake. Umoja huo hautumii jina moja linalozaliwa na muungano. Hivyo tunaweza kujifunza jambo hapa.

Tunajua Zanzibar na Tanganyika ndiyo zimezaa Tanzania. Kutaka nchi zote mbili ziwe na uanachama wa Caf na baadaye Fifa, maana yake kwa badala ya kuwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), tuwe na Shirikisho la Soka Tanganyika (TFF).

Huenda Caf lilikuwa ni suala la Hayatou kuangalia maslahi yake, lakini kwa viongozi wa TFF wakiongozwa na Jamal Malinzi, walifurahia hili lakini bila ya kujua wanauvunja muungano kupitia hilo.

Inawezekana TFF walishiriki kwa kila namna kuona linafanikiwa lakini hawakuwa wametafakari muundo wa serikali ya muungano kwani ni sawa na kuuvunja muungano upande wa michezo.

Kwa sasa Tanzania inatambulika lakini kwa wale wa Zanzibar ambao wamekuwa wakilaumu haitambuliki, hakuna hata mmoja amewahi kuhoji kuhusiana na Tanganyika kuwa nayo haitambuliki!

Caf wameishakataa, Fifa walitangulia kukataa. Viongozi wa serikali wanaosema watalifuatilia suala hilo, naona wanapoteza muda na kutaka kuwakoga wananchi tu kwa kuwa hili jambo haliwezekani ndani ya muungano wa Tanzania.

Kuling’ang’ania ni kulazimisha kuvunja muungano kupitia michezo na huenda wanaolishadadia hawavutiwi na muungano na wanataka kupitia njia ya mkato kuuvunja.
Ushauri wangu katika hili, kama limekwama kwa Caf, Fifa pia. Basi ni wakati mzuri wa kuangalia kile ambacho kinawakwaza Wazanzibar. Mfano wamekuwa wakilalamika hakuna haki katika uteuzi wa kikosi cha Taifa Stars au masuala ya kitaifa katika timu za taifa.

 Kuyafanyia kazi yale wanayolalamikia kwa njia sahihi ni jambo jema. Huenda kuona hayafanyiwi kazi na wenyewe wanaendelea kulalamika tu, mwisho wanaona njia sahihi au rahisi kwao ni kupitia moja kwa moja kwenye uanachama wa Caf na baadaye Fifa.

Lakini nishauri zaidi kwamba, inawezekana malalamiko yao yakaanza kufanyiwa kazi, basi nao wapunguze kulalamika kwenye kila jambo na mengine washiriki kuyafanikisha kwa kuwa kulalamika kupindukia hakuwezi kuwa utatuzi wa jambo.


Kuna haja ya kurejea kwenye kila linaloonekana lina mapungufu ili kuweka mambo sawa na kila upande uone unatendewa haki. 

Lakini nisisitize kwenye hili la uanachama wa Caf, Fifa litaendelea kuwa hadithi na wengine wataitumia kama propaganda tu na matokeo mwisho yatabakia yalivyo kama sasa. Hivyo, tusipoteze muda badala yake tuwekeze nguvu katika masuala ya msingi ili kusaidia maendeleo ya mpira wenyewe badala ya haya “malumbano povu”.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic