August 4, 2017
Na Saleh Ally
MTANZANIA Simon Happygod Msuva kwa sasa ni kati ya Watanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchini yetu na kama atajituma atakuwa sehemu ya wale wanaoweza kuitangaza nchi yetu vizuri.

Msuva amejiunga na timu ya Difaa Al Jadid ya Morocco, timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Timu hiyo ilishika nafasi ya pili katika ligi ya nchini hiyo msimu uliopita.

Tunajua Morocco iko juu kisoka ukilinganisha na hapa nyumbani. Pia ni nchi ya Afrika inayopakana kwa ukaribu zaidi na Bara la Ulaya, hali ambayo imesaidia kuchangia maendeleo yao kisoka kusonga mbele kwa kasi kubwa.

Msuva kufikia alipo, si jambo dogo ingawa sote tunajua ana mtihani mkubwa kuendelea kutoka alipo. Leo nimekuwa ni jambo la kujivunia kwa Watanzania wote wanaopenda mpira kwa kuwa hakuna anayeweza kukataa huyo ni Mtanzania mwenzetu na kweli, kinachotakiwa kumuombea zaidi na zaidi afike mbali.

Kipindi cha Spoti Hausi ambacho hurushwa na runinga ya mtandaoni ya Global TV Online kila Alhamisi, baba mzazi wa Msuva alisema mambo mengi sana huenda yanaweza kuwa chachu kwa familia nyingine kuwasaidia watoto wao.

Happygod Simon Msuva ndiye baba mzazi wa Msuva. Huyu ni shabiki mkubwa wa Simba, lakini alimuunga mkono mwanaye kwa juhudi kuu wakati akicheza Yanga.

Alikuwa akipata machungu kumuona akiendelea kuisaidia Yanga wakati Simba ikiyumba. Ingawa awali alipenda kumuona akiichezea Simba, lakini alipenda kumuona akifanikiwa akiwa na Yanga.

Katika mahojiano hayo, mzazi huyo alieleza namna walivyomtanguliza Mungu na kwenda kanisani mara kwa mara wakimuomba Mungu amsaidie mtoto wao.

Pia alielezea namna walivyowahi kuoga matusi kutoka kwa mashabiki wa Yanga wenye hasira kali. Hawakuwahi kuacha kumuunga mkono mtoto wao kuhakikisha anafanikiwa na kutimiza ndoto zake.

Lazima tukubali, kwamba katika hatua aliyofikia Msuva hadi anasajiliwa Difaa Al Jadid lazima kuna machungu ya kila aina ambayo yaliwahusisha wazazi wake pamoja na familia yake lakini wanaonyesha hawakuwahi kuchoka kumuunga mkono kwa kuwa walitaka afanikiwe au kufikia kile ambacho alitamani kukifanikisha.

Unapoungwa mkono na unaowapenda, suala la kukata tamaa huwa lina nafasi ndogo sana. Msuva anaweza kujivunia mengi kama juhudi, lakini sapoti ya wazazi wake imempa hatua kubwa kufikia alipo.

Tukubaliane hata kama mtakuwa hampendi au hamkubali, familia nyingi kwa sisi Watanzania huwa hatuna nafasi ya kuwasikiliza wadogo au watoto zetu wanataka nini au kufanya nini watakapofikia wakati fulani wanataka kufanya jambo fulani.

Wazazi au walezi wamekuwa wakitaka kuwaona watoto wao wakifanya kile wanachoona wao ni bora na si kile ambacho kinaweza kuwa katika mawazo yao kama ndoto. Hata kuna sehemu ambayo ingeweza kuweka mjadala wa wahusika wawili au watatu kupata kitu kimoja. Suala la amri kutoka kwa mkubwa hutawala.

Ukisikia mahojiano ya Spoti Hausi ya Global Tv Online na baba yake Msuva, unaweza kujifunza jambo jema kabisa kwamba suala hilo la kuwasikiliza watoto si lazima liwe la Ulaya tu hata hapa Afrika linatakiwa na linawezekana.

Familia ya Msuva, ilimsikiliza mtoto wao, ikaamua kumuunga mkono na ikavumilia machungu yake kwa kuwa yaliwaunganisha kama familia na mwisho unaona kuna hatua kubwa amepiga.

Iko haja ya kuanza leo kubadilika, si kila mtoto Tanzania hii anaweza kusoma na kuwa na digrii. Wengine wamepata bahati ya vipaji ambavyo vinaweza kuwapa mafanikio kupitia njia nyingine.


Tuamini kwenye vile ambavyo wengine hawakuwahi kuviamini kupitia msaada na imani ya mioyo na ubongo utuongoze kufanya mambo sahihi. Tuwaunge mkono vijana wetu kwa kuwasikiliza kwanza wanataka nini. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV