Na Saleh Ally
GUMZO la mechi ya watani wa jadi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam linazidi kupanda kwa kiwango cha juu sana.
Kila upande unaona una nafasi ya kufanya vizuri ingawa Yanga wamechukua upande wakitaka kujionyesha ni kama wanyonge lakini wanaonyesha wazi kuna kitu wanakitaka kukitumia kama vile kuibuka ghafla.
Yanga wameamua kufunga mdomo, hawataki kuzungumza sana na wamefanya wengi waamini ni wanyonge na kama Simba wataamini hivyo, basi watakuwa wamekosea sana.
Wakati upande wa Simba, unaonekana kujiamini sana na suala la kuifunga Yanga wanajipa asilimia 80. Jambo ambalo ni kosa jingine badala yake lazima wajue ni lazima kushinda ili kupata matokeo wanayoyataka au wanayoyatarajia.
Wakati gumzo linazidi kupaa juu, kumekuwa na gumzo kubwa la baadhi ya wachezaji hasa wale wapya ambao wamejiunga na timu moja au nyingine wakitokea sehemu fulani.
Mfano kwa Yanga, utaona Ibrahim Ajibu ambaye amejiunga na Yanga akitokea Simba amekuwa ni gumzo kubwa, kila mmoja akimtegemea kuwa atafanya yake, jambo ambalo kweli linawezekana kama Ajibu atatuliza akili yake kwa kuwa akijichanganya kidogo, ni rahisi sana kupoteza.
Katika mechi hiyo, Ajibu anahitaji utulivu wa hali ya juu na huenda ndiyo mechi itaonyesha ukomavu wake na anapaswa kujua akipotea katika mechi hiyo, kurudi itakuwa kazi kubwa.
Angalia kiungo Papy Tshishimbi, ametua siku chache zilizopita lakini tayari amebeba tumaini kubwa la Wanayanga kwa kuwa wanajua tatizo kwa Yanga lilikuwa ni kiungo mkabaji. Ni hatua kubwa kwa Yanga lakini bado Mcongo huyo hawezi kuwa kila kitu pekee na ujue anakwenda kucheza kwenye mfumo mpya katika mechi yenye presha. Uzoefu unaweza kumsaidia kutulia ana advantage moja, Yanga ina wachezaji wenye uzoefu, hivyo wanaweza kumfanya atulie na kucheza katika kiwango chake.
Simba nao wanawazungumzia Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima, pia wana John Bocco, kipa Aishi Manula, beki Erasto Nyoni na Salim Mbonde.
Lakini bado kuna wachezaji ambao wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri wakipewa nafasi na hawazungumziwi kabisa.
Shiza Kichuya kwa upande wa Simba, ataendelea mfalme katika mechi hiyo kwa kuwa katika mechi zote alizocheza alionyesha utulivu mkubwa, uliozaa mchango wa juu. Huyu ataisumbua Yanga ingawa hatajwi.
Kama kocha atamuamini Laudit Mavugo, hata kama ataingia kipindi cha pili, angalau apewe hata dakika 20, atawashangaza wengi hasa ambao wamemsahau na kutomzungumzia kabisa kutokana na upya mwingi katika kikosi cha Simba.
Hujamsikia mtu anazungumzia Mohammed Ibrahim “Mo”, ambaye sasa yuko katika kiwango cha juu kama ilivyo kwa Said Ndemla na utaona wanafanya jambo kama watapata nafasi ya kucheza katika mechi hiyo.
Hali kadhalika katika upande wa Yanga, mchezaji kama Emmanuel Martin, si rahisi kusikia shabiki au watu wa soka wakimzungumzia kwamba ana nafasi.
Lakini kama kocha wake atamuamini hasa katika kipindi cha kwanza. Atakuwa tatizo kubwa kwa Simba kwa kuwa ana uwezo wa kupangua hata watu watatu, ana uwezo wa kupiga mashuti pia ni mtulivu anapokuwa katika eneo la hatari.
Kumkaba Martin kunahitaji akili ya ziada kabisa kwa kuwa ni mchezaji aliyekamilika na ana uwezo wa kumvuruga beki wa aina yoyote ile.
Achana na Martin, unamkumbuka Amissi Tambwe? Huyu ndiye mchezaji mwenye uwezo wa kulenga lango na kutumbukiza mpira wavuni kuliko wote kwa misimu minne sasa.
Raia huyu wa Burundi, tokea amejiunga na Yanga akitokea Simba, ndiye mchezaji ambaye ameonyesha utulivu mkubwa kila anapokutana na timu yake ya zamani ikiwemo ni pamoja na kufunga.
Hivyo Tambwe ana nafasi ya kufanya surprise nyingine leo na mabeki wa Simba wanaijua kazi yake, hivyo wanapaswa kuwa makini kweli.
Makinda kama Baruani Akilimali kama watapewa nafasi pamoja na kutokuwa na uzoefu, pia wanaweza kusababisha shida upande wa Simba.
Mchezo wa leo, ni lazima mtu afungwe, hakuna sare. Hii maana yake ni lazima upande mmoja uwe na furaha na mwingine majonzi, hata kama itakuwa kwa mikwaju ya penalti na hii inazidi kuonyesha presha kubwa zaidi.
Kikubwa ni kuomba tu, presha hii isichangie kusababisha kuwepo kadi nyekundu za mapema au haraka na kuchangia kuharibu utamu wa mchezo ambao Watanzania wengi wapenda mpira hata wasio mashabiki wa Yanga na Simba, wangependa kuona soka linapigwa hasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment