Na Saleh Ally
EMMANUEL Martin hakuwahi kuwa katika mipango ya Yanga kabisa kupitia benchi la ufundi wala Kamati ya Usajili na ile ya Ufundi kwa ajili ya usajili.
Lakini msimu uliopita, kiungo huyo wa pembeni mwenye kasi alisajiliwa na Yanga akitokea JKU ya Zanzibar na hiyo ilikuwa ni baada ya mechi ya kirafiki wakati Yanga ikijiandaa na msimu mpya.
Yanga iliondoka uwanjani na kipigo na Martin alikuwa kati ya wachezaji waliofunga na kutengeneza bao. Tena alikuwa mshambulizi aliyewalaza na viatu mabeki wakongwe na mahiri wa Yanga.
Walichofanya Yanga ilikuwa ni uchangamfu wa mambo na hapa unaona kama ile historia ya Cristiano Ronaldo alivyotua Manchester United akitokea Sporting Lisbon iliyomkuza kisoka kwao Ureno.
Baada ya mechi ya kirafiki, Man United ikiwa imelala kwa mabao 3-1, Kocha wa Man United, Alex Ferguson hakulaza damu. Mara moja alianza mazungumzo na Sporting Lisbon na kila kitu kikawa kimekamilika. Lakini wachezaji wa Man United nao waliona kwamba Ronaldo alipaswa kuchukuliwa na klabu yao.
Wakiwa katika ndege walianza kuimba kwamba wanamtaka Ronaldo, ukiwa ni ujumbe kwa Ferguson. Kama haitoshi, waliona wamtume “kaka mkubwa”, Ryan Giggs ambaye angeweza kusikilizwa na Ferguson akamueleze lakini Giggs alipofika, Ferguson akamueleza siku mbili zinazofuata Ronaldo atatua Manchester kusaini mkataba kwa kuwa walishamalizana na Sporting Lisbon. Basi ndani ya ndege ikawa ni shamrashamra.
Yanga nao hawakulaza damu kwa Martin na hakika licha ya kuwa mgeni katika kikosi cha Yanga, hakuonyesha ugeni kila alipopata nafasi katika kufunga na kutengeneza mabao. Unaweza kusema nafasi yake ilikuwa finyu kwa sababu ya Saimon Msuva.
Msuva alikuwa ndiye staa wa Yanga na kweli inakuwa vigumu kwa kocha kumuweka benchi mchezaji kama Msuva timu inapokuwa inataka matokeo. Lakini ukiangalia mechi alizocheza Martin unagundua ni mchezaji hatari na anaweza kuwa msaada mkubwa kwa timu.
Tokea ameondoka Msuva kwenda kujiunga na Difaa Al Jadid ya Morocco, Yanga wameonekana kama kuanza kuhaha kumtafuta mbadala. Lakini inaonekana bado benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha George Lwandamina halijajenga uaminifu wa kutosha kwa Martin.
Kwa maana ya skills, au mbinu. Martin ana uwezo mkubwa kuliko Msuva, ni mwepesi na ana uamuzi wa haraka sana unapofikia wakati wa kufanya mambo mawili katika ya kuachia mkwaju au kutoa pasi.
Uwezo wa Msuva huenda ulimchanganya Lwandamina na wasaidizi wake. Lakini utakumbuka hadi Msuva anafikia alipo, alipewa nafasi nyingi za kutosha kupitia Kocha Kim Poulsen akianza nao katika timu ya vijana ya taifa.
Lakini Kocha Mholanzi, Ernie Brandts naye akaonyesha uvumilivu mkubwa kwa kumpa Msuva na Frank Domayo nafasi kubwa sana ambayo iliwafanya kuwa bora baadaye. Utaona wakati Hans van der Pluijm anakuja Yanga, tayari Msuva na Domayo walikuwa tegemeo na yeye akaendelea kuwapa nafasi nao wakaendelea kufanya vizuri na kuiva zaidi.
Kwa uchezaji wa Martin anaonekana wazi hahitaji kupewa nafasi ya muda mrefu ili kuweza kuonekana. Kama ataendelea kujiamini kama ilivyo sasa, huenda mechi tano hadi kumi zinaweza kutosha sana kwake kuonyesha alichonacho.
Huenda kwa kuwa anatumika kama kiungo wa kushoto, inampa hofu Lwandamina. Lakini duniani hakuna mchezaji anacheza namba moja au upande mmoja. Martin kama anatumia sana mguu wa kushoto anaweza kuwa hatari zaidi akicheza kulia kama ambavyo inakuwa kwa Lionel Messi na Barcelona au Cristiano Ronaldo na Real Madrid.
Kikubwa kinachotakiwa kwa Martin ni kutobadili aina yake ya uchezaji na kufanya kile anachokiona kilicho sahihi.
Wachezaji wengi sana wamefeli walipotaka kuonyesha kuwa wanaweza kubadili aina ya uchezaji kwa kuwa wamejiunga na timu kubwa au maarufu.
Mchezaji anasajiliwa na timu kubwa baada ya kuonekana. Kilichofanya aonekane ni huo uchezaji. Sasa inakuwaje anaubadilisha? Kawaida hatakiwi kuubadilisha badala yake ni kuuboresha zaidi na zaidi kwa kuuongezea vitu vinavyoweza kuufanya kuwa mtindo imara zaidi.
Kuna rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia wachezaji wa Bongo hawatabiriki, nakubaliana naye. Lakini kwa Martin unaweza kumtabiria kutokana na vitu vitano alivyonavyo; kazi, mwili mnyumbulifu, uwezo wa kupiga mashuti, uwezo wa kuruka juu kupiga vichwa licha ya kuwa na umbo dogo na uamuzi wa haraka wa mambo. Kwa haya, akifeli, basi atakuwa ameamua mwenyewe tu.
Absolutely!
ReplyDelete