August 10, 2017

“NIWE mkweli na muwazi katika kampeni zangu, moja vitu nilivyopanga kuanza navyo baada ya kuingia katika urais wa TFF cha kwanza nitakachokifanya ni kujenga akademi ya soka mkoani Dodoma.

“Ninaamini katika hilo nitafanikiwa kwani kila kitu kinakwenda kwa mipango na uzuri mimi ni mtu wa soka, hivyo ninaahidi kwa kushirikiana na wenzangu tutafanikiwa.
“Kwa nini nimechagua Dodoma? Ipo katikati ya nchi na kingine ni mji mkuu, hivyo basi ninaomba ushirikiano wenu.”

Huyo siyo mwingine bali ni, Shija Richard ambaye ni mgombea wa urais katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika uchaguzi utakaofanyika Jumamosi hii huko Dodoma.
Hapa ameelezea mikakati yake kama akifanikiwa kushinda urais wa TFF:

SERA
Mafanikio katika mpira siyo jambo la kufumba na kufumbua macho. Yanakuja baada ya kuweka misingi imara itakayosaidia kuchezeka kwa mpira.

Misingi hii huchukua muda mrefu kuweza kuijenga na kuikamilisha. Nchini Tanzania changamoto kubwa naiona katika mfumo rasmi wa kutambua na kuendeleza wachezaji pamoja na heshima ya TFF kama taasisi makini inayosimamia mpira.

Kuweza kutatua changamoto hizo kunaweza kuchukua miaka mingi, hivyo tunahitaji mpango endelevu kama ambavyo katika nchi tulivyo na ‘vision’ 2025 iliyoanza mwaka 1995 kipindi cha utawala wa Rais Benjamin Mkapa.Kwa kuzingatia hilo, nimegawa sera zangu katika mipango ya muda mrefu na mfupi. Mipango ya muda mfupi ni ile nitakayoitekeleza ndani ya utawala wangu wakati ile ya muda mrefu itakuwa ni mwendelezo wa vision ya miaka 20 ya mpira wa miguu.

MIKAKATI YA MUDA MREFU
1. MIUNDOMBINU YA KUTAMBUA VIPAJI VYA SOKA
Mchezaji wa soka anatakiwa kuandaliwa kuanzia umri wa miaka 6. Katika umri huo, watoto wa Kitanzania wanakuwa shuleni.

Kunatakiwa kuwepo mfumo rasmi wa kuweza kutambua wachezaji wakiwa wadogo. Kwa kuwa michezo imerudi mashuleni tutaweka mpango endelevu wa kutoa mafunzo kwa walimu wa michezo shuleni ili waweze kuwapa wanafunzi mafunzo stahili kwa umri wao.

Pia mpango huo utaelezea mfumo rasmi ambapo walimu hawa watakuwa wanaripoti kwa mratibu wa soka wa mkoa. Huyu atakuwa ni mwajiriwa wa TFF ataripoti kwa Mkurugenzi wa Ufundi Makao Makuu.

Atakuwa akiwasimamia walimu wa michezo shuleni akiwa na lengo la kutambua wanafunzi wenye vipaji na atahifadhi kumbukumbu na takwimu kuhusu wachezaji.
Pia atatoa mapendekezo ya wanafunzi wanaostahili kupelekwa shule maalum za vipaji vya soka (Sports Academy).

Miundo mbinu ya kuendeleza soka
Baada ya kuwa na mfumo wa kutambua vipaji, sasa vipaji hivyo vinatakiwa kuendelezwa na hapo ndipo tunapohitaji uwepo wa shule maalumu za vipaji vya michezo.

Wafunzi wenye vipaji vya soka wanatakiwa kuweka katika shule maalumu ili kupata muda kutosha kuendeleza vipaji vyao lakini pia kuwa na miundombinu rafiki karibu yao.

Kama taasisi tutaweka malengo ya kuwa na akademi katika kanda sita. Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

“Nataka katika kipindi cha miaka 20 ijayo huu ndiyo uwe mkakati wetu lakini pia katika kipindi changu cha uongozi nitahakikisha shule moja ya aina hiyo inajengwa mkoani Dodoma kwa ajili ya kuvipokea vipaji hivyo na kuviendeleza, nitakuwa tayari kuialika serikali pamoja na mashirika mbalimbali kufanikisha mpango huo.

Kuimarisha TFF
“Tunahitaji kuwa na taasisi imara yenye kuheshimika kwa Watanzania na ulimwenguni kote ili kuhakikisha tunakuwa na uwezo mkubwa wa kuwashawishi wadau mbalimbali kushirikiana na sisi katika maendeleo ya soka letu.


Mpira unabeba maslahi ya watanzania wengi sana, kwa hiyo taasisi inayosimamia mchezo huo inatakiwa kuwa makini na kufanya mambo yake kwa ufanisi mkubwa, kwa hiyo katika uongozi wangu nitaweka dira ili kila mwanafamilia wa soka kutambua uelekeo wetu kama taasisi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV