August 11, 2017


Na Saleh Ally
MAKOCHA wenye presha kubwa msimu huu kama utazungumzia soka la Tanzania basi ni Hans van der Pluijm wa Singida United na Joseph Omog wa Simba.

Leo ningependa nimzungumzie Omog raia wa Cameroon ambaye msimu uliopita, unaweza kumchagua kuwa kocha bora wa msimu kwa kuwa amefanya mambo mawili makubwa.

Kwanza, ameiwezesha Simba kumaliza msimu ikiwa ya pili, nafasi ambayo ilikuwa ikihaha kuipata kwa misimu minne iliyopita. Kama haitoshi, Omog ameiwezesha Simba kumaliza na pointi 68 sawa na mabingwa Yanga kukiwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Yanga haikuwahi kumaliza na tofauti chini ya pointi tano dhidi ya Yanga kwa zaidi ya misimu minne. Hivyo hata kama ataonekana si kocha mwenye mbwembwe nyingi lakini kazi yake aliifanya kwa ufasaha mkubwa na hakika ni mtu anayestahili pongezi kwa kuwa amerejea Tanzania kwa mara ya pili baada ya kuipa ubingwa Azam FC na kuonyesha ni kocha anayeweza tena.

Hiyo ni katika Ligi Kuu Bara, lakini angalia ameirudisha uhai wa Simba kwa kuiwezesha kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho. Maana yake, Simba inarejea katika michuano ya kimataifa kwa mara nyingine baada ya zaidi ya misimu minne, jambo ambalo lilikuwa kero kubwa kwa Wanasimba. Ndiyo maana nasema, ni kocha anayestahili pongezi zake badala ya lawama pekee.

Lakini bado unaona, huenda msimu huu ukawa wenye furaha kubwa kwa Omog raia wa Cameroon lakini pia unaweza ukawa wa wenye machungu ya kupitiliza hali inayoweza kuzaliwa na presha.

Nasema presha kwa kuwa mashabiki wa Simba wamejenga imani kubwa, matumaini makubwa na matarajio ya juu kuhusiana na kikosi chao. Hii inakwenda pia kwa viongozi ambao wameamua kufanya kila kinachotakiwa kwa kusaini kikosi imara, chenye wachezaji wenye uzoefu na maandalizi ya kutosha.

Walichokifanya wao ni kama vile wamemaliza kazi iliyotakiwa na baada ya hapo, wameangusha kila kitu kwa Omog na sasa wanachosubiri wao ni matokeo ambayo yataendana na mafanikio.
Ninaamini kama niko sahihi, siku 29 zitaamua hatma ya Omog kama atakuwa ni mtu mwenye amani au raha ndani ya Msimbazi au safari itamkuta kwa kufungashiwa virago vyake.Achana na mechi ya Ngao ya Jamii, wikiendi ijayo. Hiyo inaweza kuleta shida kwake kama Simba itapoteza dhidi ya Yanga kwa mabao mengi. Kama haitakuwa hivyo, au ikapoteza kwa idadi ndogo kunaweza kusiwe na presha kubwa sana na badala yake ligi ikawa ni kigezo ingawa kwa timu kubwa kama SImba, bado hapaswi kujiamini.

Itakapoanza ligi, siku 29 ninazozisema ni zile mechi tano za kwanza Ligi Kuu Bara ambazo Simba itaanza kucheza Agosti 26 dhidi ya Ruvu Shooting ukiwa ni ufunguzi wa ligi hiyo hadi Septemba 23, itakapocheza mechi yake ya tano.

Kama Simba itakuwa imeshinda katika mechi ya Ngao ya Jamii, halafu ikaanza ligi vizuri na kuwa na matokeo mazuri hadi Septemba 23, basi inaweza kutabiri kwa kusema utakuwa msimu mzuri au maisha mazuri ya Omog ndani ya kikosi hicho.

Kama haitakuwa hivyo, mfano Simba ikapoteza kati ya mechi zake tano hizo dhidi ya Ruvu Shooting, Azam FC, Mwadui, Mbao FC na Stand United. Basi mambo yatakuwa magumu kwa Mcameroon huyo na huenda safari ikamkuta mchana kweupeee bila ya yeye kutarajia.

Kikosi ambacho Simba wamesajili ni cha gharama ya juu, wakiwa wamechukua katika kila wanayeamini ni bora na wamemkosa Donald Ngoma pekee ambaye baada ya wao kumalizana naye, Yanga waliamua kufanya umafia na kumbakiza Jangwani.

Pamoja na kushindwa kumpata Ngoma, Simba wamewasajili karibu kila wachezaji ambao waliamini watakuwa msaada kwao katika Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho Tanzania na Kombe la Shirikisho Caf.

Sasa Omog ndiye aliyeshika usukani, anaweza kuchagua alipeleke gari lake njia ipi, itakayompendelea yeye kuishi vizuri, kwa amani au kwa presha na kila mechi moja itakuwa ikiamua uelekeo wake ndani ya Simba, kwamba anabaki au safari imemkuta.

RATIBA YA SIMBA, MECHI 5 ZA LIGI KUU BARA 2017/18
Agosti 26, 2017
Simba                  Vs   Ruvu Shooting Taifa


KALENDA YA FIFA (AGOSTI 28 – SEPTEMBA 5)
Septemba 2, 2017
Azam           Vs   Simba          Taifa

Septemba 10, 2017
Simba          Vs   Mwadui       Taifa

Septemba 17, 2017
Mbao           Vs   Simba          Kirumba

Septemba 23, 2017

Stand           Vs   Simba          Kambarage

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV