August 8, 2017


Na Saleh Ally
KIKOSI cha Mabingwa wa Rwanda, Rayon Sports kinashuka dimbani leo Jumanne kuwavaa Simba ambao ni Mabingwa wa Kombe la Shirikisho. 

Pierre Kwizera ndiye atakayeongoza nguvu ya Rayon Sports hasa katika eneo la katikati akipiga zile pasi zake za ‘moto’ ambazo mashabiki watapata burudani.

Kwizera raia wa Burundi aliondoka Simba akiwa hajapewa nafasi ya kutosha lakini ndiye akaenda kuongoza mapinduzi ya kuzima ufalme wa APR na kuifanya Rayon kurejea katika nguvu yake ya awali yeye akiwa mchezaji bora wa Ligi Kuu Rwanda, mara mbili.

Kwizera anasifika kwa pasi za mwisho zenye macho lakini akiwa na jicho la tai kuumiliki na kuubadilisha kabisa mchezo.

Simba wanapaswa kujua wanakutana na timu ya aina gani. Kawaida katika kila Tamasha la Simba Day, mara nyingi timu za kutoka Kenya au Uganda zimekuwa zikialikwa.

Safari hii, Rayon ni timu yenye watu wanaosisitiza umakini na wasingependa kurejea kwao wakiwa wamefungwa hata kama ni mechi ya kirafiki. Lazima wangependa kuondoka na ushindi.

Mechi ya kwanza kwa Simba mbele ya mashabiki wake ambao wanatarajia kuzidi 40,000. Simba watataka ushindi lakini ni lazima wajiweke vizuri hasa kuhakikisha wanashinda la sivyo itakula kwao na kuambulia kipigo.

Rayon Sports ambayo kwao hutamka “Rayo Spor”, itashuka dimbani ikiwa haina wachezaji wake sita wa kikosi cha kwanza kwa kuwa wako katika kambi ya timu ya taifa ‘Amavubi’ ambayo inajiandaa na mechi ya kuwania kucheza michuano ya Chan. 

Wachezaji ambao inawakosa Rayon ni pamoja na nahodha Ndayishimiye Jean maana yake nahodha wa mchezo wa leo kuna asilimia kubwa atakuwa Kwizera. Pia wana Luc Bakame maarufu kama Sungura.

Wengine walio Amavubi ni pamoja na beki wa kulia, Nyandwi Sadamu, mabeki wa kati Manzi Thierry na Mutsinzi Ange Jimmy. Pia viungo wawili, Seif Muhire Kelvin na Muhire Olviere.

Rayon wanakuja na kocha mpya ambaye kama atabadili mfumo sana anaweza kuwapa Simba nafasi ya kuwashinda kirahisi kama wao pia watacheza vizuri.

Olviere Karekezi ni mmoja wa wachezaji bora wa zamani wa APR, alitamba akisaidiana na Jimmy Gatete na mwaka 2004, ndiyo waliing’oa Simba katika nusu fainali ya michuano ya Kagame kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali kwa kuichapa kwa mabao 2-1 wakitokea nyuma baada ya Simba kutangulia kwa bao la Ulimboka Mwakingwe.

Karekezi alikuwa nchini Sweden akicheza soka la kulipwa, baadaye alifanya mafunzo ya ukocha na sasa amerejea na anasaidiwa na beki wa zamani wa timu hiyo Ndikumana Hamad maarufu kama Kataut ambaye ni mume wa muigizaji maarufu nchini, Irene Uwoya.

Pamoja na kuwakosa nyota hao sita, bado Simba watatakiwa kujipanga kuwaangalia watu kama kiungo kama Ally Niyonzima, huyu jamaa anakaba ile mbaya lakini pasi za uhakika na mashuti ya kushitukiza, ni hatari.

Niyonzima alisajiliwa kutokea Mukura na ameanza kuonyesha anastahili kuwa tegemeo la Rayon. Pia wana winga wa kulia, Niva Bayama ni mzuri kwa krosi na mashuti na ndiye anategemewa kuwapikia vizuri washambulizi wawili raia wa Mali ambao ni Tidiane Kone na Alhassane Yamboura.


Uchezaji wa Rayon kabla ya kocha mpya unaweza kuufananisha na ile Zanaco FC ya Zambia ambayo iliitoa jasho Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa maana ya ushindani, mechi itakuwa nzuri sana ukizingatia uchezaji wa Simba pia ni mchezo wa kugusa ingawa kwa mashabiki watakachotaka ni kuona timu yao inashinda bila ya kujali ni mechi ya kirafiki.

Simba ikishinda kwao kwa morali litakuwa ni jambo jema, lakini itakuwa fahari zaidi kwa Rayon kama watashinda mbele wakiwa bila ya nyota wao sita na wakarudi kwao Kigali na kuwaeleza Wanyarwanda namna walivyotibua sherehe ya Simba.


Kwa kifupi, Simba wanachotakiwa kuamini, Rayon Sports si timu ya kudharau na ndiyo timu kubwa zaidi yenye mashabiki wengi zaidi nchini Rwanda, hivyo itahitaji heshima hata kama kwenye sherehe ya leo, imealikwa tu. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV