August 8, 2017
Klabu ya Simba yenye maskani yake Msimbazi jijini Dar es Salaam ina utaratibu wake wa kuenzi vitu vyake vya klabu kwa kuanzisha siku maalumu ambayo wanasimba wote hukusanyika pamoja kujadiliana mambo mbalimbali.

Agosti 8 ya kila mwaka huwa ndiyo siku hiyo iliyopewa jina la ‘Simba Day’, wameichagua wao Wanasimba kama sehemu ya kumbukumbu ambapo huchagizwa na mambo mengi ikiwemo kutoa misaada kwa jamii inayowazunguka, kubadilishana mawazo, na mwisho huchezwa mechi ambayo ndiyo huitimisha kila kitu.

Hivi vyote hufanywa na viongozi, wanachama, wachezaji na mashabiki wa kawaida ambao hukutana pamoja kujadiliana mambo mbalimbali.

Kama inavyofahamika siku hiyo pia huwa ni mapumziko kwa wafanyakazi kwani kiserikali ni Sikukuu ya Wakulima, hivyo watu hupata nafasi ya kupumzika.

Leo ninakuletea mechi za Simba Day ambazo zimeshachezwa na dondoo ndogondogo kuhusu michezo hiyo tangu kuanzishwa mwaka 2009:   

Simba 1-0 SC Villa (Uhuru, 2009)
Hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa Simba kusherehekea siku yao ya kumbukumbu za klabu hiyo, waliwatendea haki mashabiki wao kutokana na kupata ushindi mwembamba.

Simba ikiwa chini ya Kocha Patrick Phiri ndani ya Uwanja wa Uhuru, ilipata bao kupitia kwa kiungo Hillary Echesa. Msimu huo Simba ilimaliza Ligi Kuu Bara ikiwa haijafungwa mchezo wowote.

Simba 0-0 Express (Uhuru, 2010)
Langoni alisimama Ally Mustafa ‘Barthez’ akilindwa na Haruna Shamte, Juma Nyosso, Amri Kiemba, Patrick Ochan, Amir Maftah, lakini nyota hao walishindwa kuzitikisa nyavu za Waganda hao na kusababisha mashabiki wao waondoke vichwa chini.

Simba 0-1 Victors (Sheikh Amri Abeid, 2011)
Mchezo huu ulifanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha na Simba kuambulia kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Victors ya Uganda.
Bao pekee la washindi lilifungwa kwa njia ya penalti na Patrick Sembuya, siku hiyo pia Simba walitangaza uzi wao mpya.

Simba 1-3 Nairobi City Stars (Taifa, 2012)
Simba ikiongozwa na nyota kibao kina Juma Kaseja, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’, Uhuru Seleman na wengineo ilikubali kichapo hicho kutoka kwa Nairobi City Stars kutoka Kenya.

Simba ilikuwa chini ya Kocha Milovan Cirkovic raia wa Serbia. Mabao ya washindi yalifungwa na Duncan Owiti, Bruno Okullu, Boniface Onyango huku lile la Simba likiwekwa kimiani na Sunzu.

Simba 4-1 SC Villa (Taifa, 2013)
Safari hii walioipa Simba kampani kwenye siku yao ya kumbukumbu ni SC Villa kutoka Uganda. Kama kawaida Msimbazi waliiandaa timu yao na wakapata ushindi uliowapa burudani kubwa mashabiki wao.

Waliopeleka kilio siku hiyo Villa ni, Jonas Mkude, William Gallas na Betram Mwombeki ambaye alitupia mawili. Simba wakati huu ilikuwa chini ya Kocha Abdallah Kibadeni.

Simba 0-3 Zesco (Taifa, 2014)
Hapa Simba iliwanyima raha mashabiki wake baada ya kuambulia kichapo kwenye siku yao maalumu ya kumbukumbu za kuanzishwa kwa klabu yao.

Waliopeleka kilio siku hiyo Msimbazi walikuwa ni Jackson Mwanza dakika ya 14, Clatos Chane dakika ya 64 na Mayban Mwaka aliyefunga dakika ya 90. Siku iliisha vibaya kwa Simba iliyokuwa chini ya Kocha Zdravko Logarusic.

Simba 1-0 SC Villa (Taifa, 2015)
Wale mashabiki waliokuwa wakikaa mbali kutoka Uwanja wa Taifa pale tayari walikuwa wameanza kuondoka wakidhani mechi ingeisha kwa suluhu, lakini alikuwa ni Awadh Juma ambaye alifunga bao kwa shuti kali nje ya 18 dakika ya 89 na kuipa shangwe Simba. Siku ya ‘Simba Day’ ikaisha murua kabisa kwa ushindi wa usiku ambao huwa mtamu zaidi.

Simba 4-0 AFC Leopards (Taifa, 2016)
Mechi ilipigwa Agosti 8, mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ikiwa ni sikukuu ya kumbukumbu ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo. Simba ilipata mabao yao kupitia kwa Ibrahim Ajibu aliyetupia mawili, Jamal Mnyate moja na Shiza Kichuya pia moja.

Simba Vs Rayon Sports (Taifa, 2017)

Iitakuwaje? Acha tusubiri leo jioni.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV