Na Saleh Ally
UCHAGUZI wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ulikuwa unasubiriwa kwa hamu kubwa, umefikia tamati juzi baada ya washindi kupatikana.
Wallace Karia amewagaragaza wenzake na kuwa mshindi wa kiti cha Urais wa TFF huku Michael Wambura naye akirejea TFF kwa kushinda nafasi ya makamu wa rais.
Wakati wawili hao wanashinda, wengi wamekwenda na maji. Hawakupata nafasi ya kushinda kwa kuwa ilikuwa ni lazima katika nafasi hizo mbili washinde watu wawili tu.
Katika picha kadhaa ukiziangalia, utaona kuna taharuki miongoni mwa waliokuwa wagombea hasa katika nafasi za makamu wa rais na ile ya rais.
Inaonekana kama hawakuamini hivi au ni jambo lililotokea kwa kuwashitua na hii inatokana na kwamba walikuwa na matumaini makubwa kupindukia.
Ukiuliza kwa nini walikuwa na matumaini makubwa, jibu litakuwa ni kwa vile katika kampeni wapiga kura waliwahakikishia kwamba wangepiga kura kwa ajili yao na kuhakikisha wanashinda.
Lakini sote tunajua namna ambavyo wapiga kura walivyo wajanja. Mara zote wamekuwa wakiwahakikishia hadi watu watano katika nafasi moja kwamba watawapa kura ya ndiyo.
Mwisho, wanamchagua mtu mmoja ambaye walikuwa wanahitaji kumchagua na alikuwa siri ya mioyo yao. Hivyo walioonekana kuwa na taharuki wana haki ya kufanya hivyo huenda wakati wa kampeni walipita sehemu mbalimbali na kujihakikishia rundo la kura. Mwisho, zikaota mbawa tena kwa kiasi cha kushangaza.
Wakati uchaguzi umeisha na wao kuangushwa, kawaida maisha yanaendelea na ndiyo wakati mwafaka wa kuendelea na maisha kama ilivyo siku nyingine.
Wao wataendelea na maisha yao na hautakuwa mwisho wa maisha yao katika mchezo wa soka kwa kuwa baadhi waliwahi kucheza, wako waliwahi kuongoza na wanaendelea kuwa watu wa soka au wadau muhimu.
Katika kampeni karibu kila mgombea alikuwa na jambo lake na hata kama lilifanana na mwenzake katika maana lakini kiutendaji wengi walitangaza njia tofauti za kulifanyia kazi lengo likiwa ni kusaidia kupatikana kwa maendeleo.
Sasa hawakupata nafasi ya kushinda, ushauri wangu utaangukia sehemu mbili. Moja kwa walioshinda, kutoa nafasi kwa wale ambao wanaona walishindwa kama wana nafasi ya kusababisha au kuanzisha na kuleta maendeleo, basi washirikiane nao na kufanya nao kazi, lengo ni kuleta mabadiliko na kuutengeneza mpira wa nchi yetu ambao kila kukicha unatutia aibu tu!
Pili, wale ambao walikuwa na mawazo yao naona haitakuwa sahihi kama wataendelea kukaa nayo wasubiri watakapogombea tena baada ya uongozi wa sasa kumaliza muda wake.
Naona pia haitakuwa sahihi kuufanya uongozi wa sasa ni kama washindani wa milele au uongozi kuwaona walioshindwa kama washindani daima, badala yake vizuri kuunganisha mawazo na yenye nafasi ya kutukuomboa yafanyiwe kazi.
Ukiangalia wagombea wengi ambao wamepoteza nafasi bila ya kujali ni nani, wana nafasi ya kuwa na mawazo mazuri ambayo yanaweza kuusaidia mpira wa Tanzania ambao unaendelea “kujichokea” tena na tena kila kukicha.
Kinachotakiwa sasa ni kuvunja yale makundi ya uchaguzi, kuvunja hisia za ushindani wa uchaguzi na kurudisha hisia za maendeleo kwa pamoja kwa kuwa wakati wagombea wakipiga kampuni ilikuwa ni kutaka kuendeleza mpira wa Tanzania na si mpira wa TFF.
Hakuna anayeweza kuukomboa mpira wa Tanzania isipokuwa Watanzania wenyewe. Hakuna anayekataa waliogombea wote ni Watanzania, hivyo ninaamini hakutakuwa na anayekataa kusaidia mipango ya maendeleo au anayepinga watu kusaidia mabadiliko.
0 COMMENTS:
Post a Comment