August 14, 2017




Ikiwa ni siku chache tangu atue Yanga, beki mpya wa timu hiyo, Gadiel Michael amefunguka kuwa atahakikisha anawazima washambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya watakapokutana wiki ijayo.

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Agosti 23, mwaka huu, ambapo tayari presha imekuwa kubwa, Yanga wamefunga safari kutoka Dar es Salaam hadi Unguja kwa ajili ya kambi kujiandaa na mchezo huo.

Beki huyo wa kushoto amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Azam FC ambapo juzi Jumamosi katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi dhidi ya Ruvu Shooting alionyesha uwezo mkubwa wa kukaba na kupandisha mashambulizi.

Gadiel alisema kuwa  kwake mchezo huo utakuwa ni wa kawaida na amejipanga kuwadhibiti wachezaji hao watakaocheza kwenye eneo lake hadi kusahauliwa na mashabiki wa timu yao.

“Nadhani hiyo ndiyo mechi ambayo nitajitambulisha rasmi Yanga maana katika kucheza kwangu mpira sijawahi kuogopa mechi kubwa hata siku moja wala kuwahofia wachezaji, na hao ambao watakuwa wanafika kwenye eneo langu wajue kabisa nitawazima kabisa siku hiyo.

“Lakini hata wakati nacheza Azam, mechi za Simba na Yanga nilikuwa nikiaminiwa kupewa nafasi kwa sababu kuna kitu ninachokionyesha, sasa Yanga nahitaji kuaminika zaidi pia naamini Mungu ataniongoza kwa kila kitu katika maisha yangu mapya,” alisema Gadiel.

Katika siku za hivi karibuni, beki huyo amekuwa akionyesha uwezo wa juu hasa alipokuwa akiichezea timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kiasi cha kuaminiwa na kuwa na uhakika katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo licha ya kuwa ni chipukizi.

Usajili wake kutua Yanga uliambatana na ugumu baada ya awali Azam FC kugoma kumuachia kutokana na kuwa na mkataba ambao ulitarajiwa kumalizika Desemba, mwaka huu, lakini baada ya mazungumzo baina ya klabu hizo, akaachiwa kwa ada ya uhamisho wa shilingi milioni 10.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic