Kuelekea mchezo wa Simba, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga amejinasibu kuwa kikosi chao kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo huo na wanaamini watapata ushindi.
Timu hizo zinakutana Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex ikiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo timu hizo zitaumana kwa mara ya kwanza uwanjani hapo baada ya Azam kuruhusiwa kuutumia uwanja huo katika mechi dhidi ya Simba na Yanga.
Akifafanua zaidi Jaffar alisema: “Tunawaheshimu wapinzani wetu, Simba ni timu nzuri na tunatarajia mchezo utakuwa mgumu, lakini tunaamini pia ubora wa kikosi chetu na maandalizi ni silaha yetu nzuri ya ushindi siku hiyo.”
Upande wa Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas akizungumzia mchezo huo alisema utachezeshwa na mwamuzi Ludovick Charles wa Tabora, akisaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Abdallah Mkomwa wa Pwani na Josephat Bulali atakayekuwa mezani huku kamisaa akiwa Ruvu Kiwanga wote wa Dar es Salaam.
KOCHA NAYE ANENA
Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, alisema kuwa mchezo huo wanauchukulia umuhimu licha ya kuwa ni kama michezo mingine wanayocheza kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
“Huu ni mchezo wetu wa pili wa ligi na tunahakikisha tunacheza nyumbani na uwanja wetu wa nyumbani tunataka tushinde kwa sababu toka tumefungua uwanja wetu huu tumewahi kupoteza mara tatu tu na hatutegemei kupoteza tena katika msimu huu.
“Kwa hiyo kwanza ni kitu cha umuhimu kwamba tuweze kushinda nyumbani, halafu mwaka huu tuna dhamira ya kufanya mambo makubwa zaidi,” alisema.
Cheche alisema kuwa ushindani ni mkubwa kikosini hali ambayo inawapa wakati mgumu wao kama makocha katika kukipanga kikosi hicho.
“Morali ni kubwa…wakati fulani inatupa wakati mgumu kufikiria nani nimweke wapi na nani nimweke wapi kwa sababu kila mtu ana hamu nayo, sasa hii inatupa kazi rahisi kwamba yule atakayepata nafasi ya kuanza atatupa yale mategemeo ambayo tunatarajia sisi,” alisema.
Safu ya ushambuliaji yaboreshwa
Kutokana na safu ya ushambuliaji kupoteza nafasi nyingi kwenye mchezo wa kwanza walioifunga Ndanda bao 1-0, Cheche ameweka wazi kuwa tayari wameshalifanyia kazi ikiwemo pia kuhakikisha safu zote zinakuwa imara katika mtanange huo.
“Mchezo wa mpira ulivyo ni mchezo wa makosa, hauwezi kuwa bora kila siku, tumeanza vizuri katika safu ya ulinzi na kiungo, matatizo katika ushambuliaji na sasa hivi tumelifanyia kazi sana hilo na kuhakikisha na yale tuliyofanya nyuma katika kiungo na ulinzi yasije yakabadilika, kwa hiyo tumehakikisha idara zote zinakaa vizuri ili kutupa matokeo mazuri katika michezo yetu kuanzia huu na mingine inayokuja mbele,” alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment