September 6, 2017



MUNICH, Ujerumani

KLABU za Ligi Kuu Ujerumani Bundesliga, ambayo imekuwa ikionyesha Mubashara na Kingamuzi cha Startimes, zimeweka rekodi ya usajili kwa kumwaga zaidi ya euro milioni 600 katika dirisha la usajili lililofungwa Alhamisi iliyopita huku hali hiyo ikimuacha mmoja wa mabosi wa Bayern Munich, Uli Hoeness, akiona hatari mbele kutokana na kuongezeka kiholela kwa bei za wachezaji.



Bayern iliweka rekodi mpya klabuni hapo pamoja na kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), ilipomsajili kiungo Mfaransa, Corentin Tolisso kutoka Lyon kwa kitita cha euro milioni 41.5 mwezi Juni.


Hata hivyo, kitita hicho kilipigwa chini na mahasimu wao Borussia Dortmund waliomuuza winga Ousmane Dembele kwenda Barcelona kwa dau la euro milioni 105.


Lakini kitita hicho cha Dembele ni chini ya nusu ya kitita ambacho kilivunja rekodi ya dunia kilichotolewa na Paris Saint-Germain kumnasa Neymar kutoka Barcelona. PSG ilitoa euro milioni 222.

“Hadi sasa, huu ni mchezo ambao hauna mipaka ambapo ni wachezaji pekee wanaofaidika," Hoeness aliliambia

jarida la Ujerumani, Sport Bild.


"Kweli sijui tunakoelekea ni wapi. Tulipofikia sasa tunatakiwa kuwa makini sana, kwa sababu hadi sasa mashabiki wameshasikia mengi mno.


"Ni lazima niseme wazi kuwa, huu ni wakati wa kurudisha mambo katika uhalisia.”


Hata hivyo, Bayern nayo imemwaga fedha ili kuboresha kikosi chake kwa lengo la kujaribu kutwaa ubingwa wa Bundesliga kwa mara ya sita mfululizo.


Imemsajili beki Mjerumani, Niklas Suele kutoka Hoffenheim kwa dau la euro milioni 20 wakati Kingsley Coman sasa amekuwa mchezaji wao rasmi baada ya kukamilisha uhamisho wake kwa kitita cha euro milioni 21 akitokea Juventus. Awali Coman alikuwa anacheza Bayern kwa mkopo.


Wapinzani wa Bayern, nao hawakuwa nyuma katika kuviboresha vikosi vyao.


Dortmund walitumia vizuri kitita walichopewa kwa ajili ya Dembele ambaye mwaka mmoja tu uliopita, walimsajili kwa euro milioni 15.


Kabla ya kufungwa kwa usajili, walimnasa kinda mwenye miaka 17, Jadon Sancho kutoka Manchester City kwa kitita cha euro milioni nane.


Kabla ya hapo, Dortmund ilikuwa imemsajili winga wa Ukraine, Andriy Yarmolenko kutoka Dynamo Kiev kwa dau la euro milioni 30, pamoja na beki wa kulia Mjerumani, Jeremy Toljan kutoka Hoffenheim.


Cologne, yenyewe ilimwaga kitita cha euro milioni 17 kwa ajili ya kuleta mbadala wa Anthony Modeste aliyekwenda China, kwa kumsajili Jhon Cordoba kutoka Mainz, hata hivyo, hadi sasa Mcolombia huyo bado anasotea kiwango.


Bayer Leverkusen yenyewe ilimwaga euro milioni 36.5 kwa beki kinda kutoka Olympiakos, Panagiotis Retsos, 19, na straika Muargentina, Lucas Alario, 24, kutoka River Plate.

Borussia Moenchengladbach ilimwaga kitita cha euro milioni 17 ili kumnasa Matthias Ginter kutoka Dortmund.


Hata hivyo, kitita kilichomwagwa na timu 18 za Ujerumani, ni pungufu ukilinganisha na vitita vilivyomwagwa katika ligi nyingine.



Ligi Kuu ya England inadaiwa imemwaga kiasi cha euro bilioni 1.3, Italia (takriban euro milioni 800) na Ufaransa (takriban euro milioni 650).

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic